Leo nina furaha kubwa sana
kwani baada ya safari ndefu na yenye changamoto nimerudi nyumbani
kuwasalimu wananchi wenzangu! Na hii si salamu za kawaida bali
nawasalimu kwa salaam za demokrasia, uadilifu, uzalendo na uwajibikaji.
Nawasalimu si kama mbunge bali kama mwana wenu wa Kigoma! Na popote
niendapo najivunia kujitambulisha kama Mtanzania; kama mwenyeji wa mkoa
wa Kigoma na zao la Ujiji.
Tuna mengi ya kujivunia kama
taifa lakini Ujiji na watu wake mna nafasi ya pekee katika historia.
Watu wa Ujiji mlipokea harakati za kudai uhuru wa nchi yetu mapema
kabisa mapambano ya uhuru yalipoanza. Watu wa Ujiji mlikuwa wa kwanza
kabisa kupokea mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Na Jimbo la Kigoma Mjini
ilikuwa miongoni mwa majimbo ya mwanzo kabisa kutoa mbunge wa CHADEMA
mwaka 1995.
Kabla ya hapo mlitoa madiwani
wengi mwaka 1994. Wakati Watanzania wengine wakiwa wanajiuliza mara
mbili mbili kuhusu kujiunga na vyama vipya vilivyoanzishwa, watu wa
Ujiji, watu wa Kigoma hamkusita kupokea mabadiliko. Wengi wamepoteza
maisha yao, wengine kazi zao na wengine hata ndoa zao katika kupata
mbegu ya mabadiliko katika nchi yetu. Nawataka msichoke. Wekeni nguvu
mpya katika kusimika mabadiliko kwani bado kazi ya kuimarisha demokrasia
katika nchi yetu haijaisha na inahitaji uvumilivu, kusameheana na
kuaminiana.
Na nchi yetu Tanzania ni nchi
inayoonyesha uwezo mkubwa katika kupendana, kuaminiana, kuvumiliana na
hata kusameheana. Na haya si maneno tu ambayo ninayazungumza kama
mwanasiasa.
Hii ni hali halisi na maisha
niliyoyaishi kwa mifano nilipokuwa ninakua na kusoma katika shule ya
Msingi Kigoma na baadaye Shule ya Sekondari Kigoma. Malezi yangu
yalikuwa yanaongozwa na jamii nzima ya Kigoma. Nimekuwa nikiwaeleza
rafiki zangu niliokutana nao kwenye masomo na kwenye siasa kwamba
nimeanza kuvaa viatu kwa mara ya kwanza nikiwa darasa la tatu. Viatu
hivyo viliitwa 'asante Salim' vilivyokuwa vinatengenezwa na Kampuni ya
Bora Shoes. Vililinunuliwa na mama Coretha Furugunya ambaye tulikuwa
tunakaa mtaa mmoja wa Kisangani Mwanga.
Mama Coretha hakuninunulia
viatu kwa sababu alikuwa ana uwezo mkubwa, la hasha! Alifurahishwa na
matokeo yangu ya mitihani ya darasa la pili kwenda la tatu. Ninaamini
kitendo cha mama huyu ni ushahidi wa uungwana, upendo na hata
uwajibikaji ambao tunao sisi watanzania.
Uwajibikaji kwani alichukua
jukumu kunilea ingawa hakuwa mzazi wangu, lakini aliona kuwa kama
mwanajamii ana nafasi kubwa katika kuwaendeleza watoto wote. Jamii hii
ya watu wa Kigoma ilinifunza kuwa nikijitahidi na kukazana kwa bidii
kwenye masomo na majukumu, nitafanikiwa. Siwezi kusahau somo hili katika
maisha yangu na ni somo hili ndilo limenifanya nijitahidi kwa kadiri ya
uwezo wangu kuwatumikia kwa uadilifu na mafanikio ya hali ya juu sana.
Nikiwa nimejaa matumaini haya
kuhusu wananchi wenzangu, leo nataka niwakumbushe kwa nini kama jamii
tulichagua kufuata njia ya demokrasia. Demokrasia ina maana pale ambapo
inatumika kuleta mabadiliko chanya kwenye maisha ya wananchi. Maisha
yanayotakiwa ni yale yanayomwezesha mwananchi kupata huduma zake stahili
kama Elimu, Afya, Maji na miundombinu. Demokrasia haina maana pale
wananchi wanakufa njaa kwa kukosa ajira na kukuza umasikini.
Demokrasia inahusu maendeleo.
Tumejitahidi kwa upande wetu kuondoa mkoa wa Kigoma kutoka mikoa isiyo
na miundombinu kabisa ya maendeleo mpaka kuwa mkoa unaotumika kama mfano
kwa miradi mingi ya Maendeleo ikiwemo Daraja la Malagarasi, Uwanja wa
ndege wa Gombe-Mahale, barabara za lami na upanuzi wa Bandari, ujenzi wa
bandari ndogo mpya na ujenzi wa kituo cha Usafirishaji Mwandiga.
Asije mtu akasema yeye ndio
kafanya haya. Haya ni matunda ya nyinyi watu wa Kigoma kupokea
demokrasia na bila woga kuchagua viongozi wenu bila kujali vyama bali
kwa kuangalia uwezo. Haya ni matunda ya viongozi wenu kupaza sauti yenu
kwenye baraza la Taifa, Bunge. Haya ni matunda ya uvumilivu wenu na
uamuzi wenu wa kutaka maendeleo. Juhudi hizi lazima ziendelezwe kwa
nguvu zote ili kuhakikisha kuwa nafasi ya mkoa wa Kigoma katika uchumi
wa Tanzania inaonekana dhahiri na hivyo kuchochea maendeleo ya nchi yetu
kwa kuwa kituo cha biashara katika nchi za maziwa makuu.
Lakini tukumbuke pia kuwa
Demokrasia ni Uwajibikaji. Katika kipindi cha utumishi wangu
kwenu,kutokana na malezi niliyoyapata kutoka kwenu,nimekuwa mstari wa
mbele kuhakikisha kuwa Serikali inawajibika kwa Wananchi. Nakumbuka
wakati napambana kuhusu sheria mbovu ya madini kuna watu hapa nyumbani
walisema 'sasa huyu kawa mbunge wa Taifa' lakini watu wengi zaidi
wakasema tumemtuma Dodoma kusemea Watanzania wote na sio Kigoma tu.
Tuliweza ndani ya miaka mitano
kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye sera ya Madini na sheria ya
madini ambapo baadhi ya mambo ambayo yalikuwa hayafikiriki sasa
yametungiwa sheria ikiwemo Serikali kuwa na hisa kwenye migodi,
Tanzanite kumilikiwa na Watanzania sio chini ya asilimia 50 na kuzuia
kabisa wageni kuchimba vito vya thamani. Uwajibikaji ulipelekea
kumshinikiza Rais kufanya mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri kwa
kuwafukuza mawaziri wanane mwaka jana.
Hii ilitokana sio tu na hoja ya
kutokuwa na imani na Waziri Mkuu bali pia ushiriki mkubwa wa wananchi
kupitia simu na mitandao ya kijamii ambapo wabunge walishinikizwa kuweka
saini kwenye karatasi za kumtoa Waziri Mkuu. Toka wakati huo kumekuwa
na utaratibu sasa ambapo wabunge hawaoni taabu kutaka uwajibikaji
waziwazi ili kuzuia ubadhirifu wa fedha za Umma. Ni hivi jana
tumeshuhudia mawaziri wanne wamejiuzulu na kufukuzwa kazi kutokana na
kashfa ya operesheni Tokomeza ujangili iliyoibuliwa na ripoti ya kamati
ya bunge. Mabadiliko haya ni hatua muhimu katika kuimarisha demokrasia
yetu.
Pamoja na matunda haya mengi mazuri lakini bado kuna changamoto katika juhudi zetu.
Changamoto kubwa tuliyonayo wananchi ni kukosekana kwa imani katika demokrasia yetu.
Kutoaminiana. Ni
dhahiri kuwa kutoaminiana katika nchi yetu kumekuwa kwa kiasi kikubwa.
Taarifa za kitafiti zinaonyesha kuwa katika kila Watanzania kumi, wanane
hawaaminiani. Ni changamoto kubwa sana. Wananchi wameacha kutuamini
wanasiasa na wanasiasa wameacha kuaminiana wenyewe kwa wenyewe.
Hivi sasa uongo umegeuzwa kuwa
ukweli na ukweli umekuwa ni uongo. Hivi sasa ukitaka kuwa mwanasiasa
maarufu inabidi ujue kudanganya na ukitaka kuitwa mwanasiasa msaliti
inabidi uwe msema kweli. Kukosekana kwa uaminifu na kuaminiana imekuwa
ni kansa katika siasa zetu. Itachukua muda mrefu sana kujenga demokrasia
imara katika nchi yetu kama hatutapata jibu la changamoto hii ya
kutoaminiana na kugeuza uongo kuwa ukweli na ukweli kuwa uongo.
Hivi sasa ukweli umekuwa
unatengenezwa badala ya kutafutwa. Ni majanga! Juzi bungeni Mwanasheria
Mkuu wa Serikali alielekeza shutuma kwangu kwamba sikushirikiana na
kamati maalum iliyoundwa na Bunge kufuatilia mabilioni ya uswisi na
kwamba chini ya kiapo nilisema sina majina ya watu wenye akaunti huko
Uswisi. Huu ulikuwa ni uongo. Ni uongo kwa sababu niliitika wito wa
kamati hata nilipokuwa katika mafunzo ya mgambo huko Tanga na nilikutana
nao mara nne.
Ni uongo kwa sababu niliwapa
wajumbe wa Kamati Maalaum maelezo na taarifa nyingi sana kuhusu
utoroshwaji wa fedha nje ya nchi na umiliki wa mali nje ya nchi
kinyumecha sheria. Ni uongo kwa sababu mimi kutotaja majina haya haina
maana sina majina, bali ni kwamba ninaheshimu utaratibu na nimeachia
vyombo husika vikamilishe uchunguzi. Kwani mimi kama mtu binafsi
nikianza kuchukua majukumu ya taasisi ninaweza kutia dosari harakati
hizi muhimu na hata kupelekea mchakato mzima kuvurugika.
Sitaingia mtego huu! Lakini
hatua hii ya Mwanasheria Mkuu imenipelekea kujiuliza maswali mengi kwa
mfano uongo kama huu ulifanywa kwa malengo gani? Na ninajikuta hata mimi
ninaingia katika hali ninayoilalamikia ya KUTOAMINIANA.
Lakini mtambue pia kuwa
kutoaminiana kunaleta kutovumiliana. Hivi sasa kuwa na mawazo tofauti
katika vyama vya siasa au hata asasi za kijamii ni uhaini. Lakini bila
kuenzi tofauti za mawazo hatuwezi kujenga vyama imara wala Taifa imara.
Demokrasia imara ni zao la tofauti za mawazo na uhuru wa mawazo. Kama
hatuwezi kujenga vyama vinavyorutubisha uhuru wa mawazo na tofauti za
mawazo, tutajenga Taifa lenye watu wenye kuogopa na waliojaa woga. Wanachama wanapoogopa uongozi ni udikteta, lakini uongozi unapoogopa wanachama ni demokrasia.
Bila demokrasia ya uwazi na kuvumiliana tutakuwa Taifa la kidikteta.
Lazima vyama vya siasa, viongozwe kwa namna ile ile ambayo Taifa
litaongozwa.
Demokrasia bila kuaminiana, demokrasia bila kuvumiliana sio demokrasia ya kweli.
Juzi nilipoingia Bungeni kwa
mara ya kwanza baada ya matukio kadhaa yanayoendelea ndani ya chama
chetu nilikaa pamoja na mbunge Tundu Lissu. Wabunge wengine walidhani
tutarushiana ngumi na badala yake ikawa ni vicheko na mazungumzo.
Hii ni kwa sababu sina chuki na
mtu yeyote yule. Mmenifunza kutojenga chuki na watu na badala yake
kuchukua kila tukio kama changamoto ya maisha. Siasa ni kupambanisha
mawazo tofauti na hatimaye kutafuta suluhu ya pamoja. Na siasa ina
misingi yake ambayo sisi wanasiasa huwa tunasahau kwa maksudi. Msingi wa
siasa ni kuwa inapaswa kuleta unafuu wa maisha ya wananchi na sio
malumbano tu ya kurushiana maneno na kuzushiana ili kujijengea umaarufu
wa kisiasa. Siasa si kuwekeana chuki na kuonyeshana ubabe.
Na hapo ni muhimu muelewa
wanaKigoma mnapoambiwa kuwa eti ninapofuatilia mabilioni ya Uswisi
ninatafuta umaarufu, ni uongo! Mnaposikia eti kukataa kwangu kuchukua
posho ni unafiki na kujitafutia umaarufu, ni uongo! Kinachonisukuma
kufanya vyote hivi ni ninyi.
Ninasukuwa kila ninapowaona
watoto bado wanatembea bila viatu;kila ninapoona akina mama wanapoteza
maisha yao katika uzazi;kila ninapoona vijana ambao hawana uhakika wa
kupata hata mlo moja kwa siku kwa kukosa kazi; ninapoona wazee wa Kigoma
kukosa hata shilingi mia moja kununua chai asubuhi. Ninawaona si
wanaKigoma bali mamilioni ya watanzania wakiishi katika hali hii. Alafu
nalinganisha na taarifa tunazozipata kuhusu ufujaji na utoroshwaji wa
pesa zetu.
Hebu sasa linganisheni na
ukweli kuwa ripoti ya kimataifa iliyotolewa hivi karibuni imeonyesha
kuwa mwaka 2010 pekee, jumla ya dola za kimarekani milioni 1315 (bilioni
1.3), yaani shilingi trilioni 2,113,930,000,000 (sh
trilioni 2.1) zilitoroshwa kutoka nchini Tanzania. Mwaka 2011 kiasi cha
dola za kimarekani milioni 817 yani shilingi za kitanzania zipatazo
trilioni 1,315,370,000,000 (trilioni 1.3) zilitoroshwa. Ripoti hiyo
inaeleza kuwa jumla ya fedha za Watanzania zilizotoroshwa nje ya nchi
katika miaka kumi iliyopita zilifikia dola za kimarekani milioni 4526
(bilioni 4.5) sawa na shilingi za kitanzania trilioni 7,286,860,000,000
(trilioni 7.3).
Nimewatajia hapa namba chungu
nzima na matrilioni na mabilioni hayaleti maana. Lakini hii ina maana
kwamba kiasi cha pesa zilizotoroshwa katika miaka 10 pesa - robo yake
tuingeweza kujenga barabara ya lami ya kiwango cha juu kabisa kutoka
Kigoma mpaka Dar-es-salaam! Pesa hizi zingeweza kuajiri na kuwalipa
vizuri walimu, madaktari na wafanyakazi wengine ili kuhakikisha tunapata
huduma bora na kutengeneza ajira bora kwa vijana wetu. Pesa hizi
zingeweza kununua madawa muhimu na kuokoa maisha ya maelfu ya akina mama
tunaowapoteza kila mwaka wakati wa uzazi.
Pesa hizi zingeweza kuwanunulia
watanzania wote si watoto tu angalau pea 10 ya viatu. Sasa nikitafakari
haya siwezi kuchapa usingizi mnono na kufumbia macho utoroshwaji wa
fedha au matumizi mabaya ya fedha za umma kwa njia ya sisi wabunge
kujilipia posho! Hapana! Nafsi yangu hainiruhusu kukaa kimya kwa kuogopa
kuitwa mbinafsi au msaliti!
Lakini naomba niwasihi kuwa
katika nyakati kama hizi za changamoto za kisiasa jambo la msingi kuliko
yote ni kutulia maana hakuna linalotokea bila sababu. Licha ya kwamba
kuna watu wengi wanapaza sauti zao katika mambo haya lakini pia kuna
wengi zaidi ambao wapo kimya lakini wana mawazo yao, ndani na nje ya
chama chetu;ndani na nje ya Serikali na ndani nanje ya nchi yetu. Ndio
maana lazima kuibadili nchi yetu ili kuweza kuhakikisha kila raia
anakuwa na fursa ya kutoa mawazo na fikra zake zinakuwa huru.
Maisha ni mabadiliko;
mabadiliko hayana ukomo; mabadiliko hayazuiliki kwa sababu bila
mabadiliko hakuna ukuaji, bila mabadiliko hakuna maendeleo. Mabadiliko
ni kiu kikubwa cha Tanzania kwa sababu mabadiliko huleta matumaini. Na
kiu hii ni kubwa zaidi kwetu sisi vijana wa kizazi hiki kipya. Siasa za
kizazi kipya cha viongozi ni siasa za majawabu ya kero za wananchi.
Siasa za mabadiliko ni siasa za kujenga na kuimarisha; ni siasa za
kuaminiana na kuheshimiana hata pale mnapopingana kimawazo. Ninataka
tujenge siasa mpya Tanzania;siasa za mabadiliko; siasa zinazojenga
matumaini ya kweli;siasa zinazowajali na kuwajengea uwezo wananchi wa
Tanzania. Mungu ibariki Tanzania.
0 comments:
Post a Comment