Home » » KAFULILA AIPAISHA KICHWA IPTL

KAFULILA AIPAISHA KICHWA IPTL

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila
Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL) imewasilisha maombi mahakamani ya kuomba zuio la muda dhidi ya Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila la kuendelea kutangaza maneno ya kashfa dhidi yake.
 IPTL iliwasilisha maombi hayo mwishoni mwa wiki iliyopita katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, ikiiomba itoe zuio hilo hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Kampuni hiyo imefungua kesi hiyo dhidi ya Kafulila kwa kuituhumu kuchota fedha katika akaunti ya Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) isivyo halali.

IPTL kwa kushirikiana na kampuni ya Pan African Power Solutions (T) Limited (PAP) na Mtendaji Mkuu wa kampuni hizo, Harbinder Sign Seth, waliwasilisha maombi hayo mahakamani hapo chini ya hati ya kiapo cha dharura na yameungwa mkono na Seth.

Maombi hayo namba 306 ya mwaka huu, yalitajwa mahakamani hapo Alhamisi iliyopita, mbele ya Jaji Rose Teemba, ambaye aliahirisha shauri hilo hadi Agosti 28, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa.

Kwa mujibu wa hati ya maombi hayo, wadai kupitia wakili wao, Augustine Kusalika, wanaiomba mahakama itoe zuio la muda kwa Kafulila kuendelea kutangaza maneno ya kashfa kwa IPTL, PAP na Seth hadi shauri lao la msingi litakapoamuliwa.

Pia wanaiomba mahakama kutoa zuio la muda kwa Kafulila asiendelee kutangaza maneno ya kashfa dhidi ya IPTL na PAP na aamriwe kulipa gharama za maombi hayo.

Awali, IPTL, PAP na Seth kupitia wakili wao, Kusalika walimfungulia kesi ya madai Kafulila mahakamani hapo wakiiomba mahakama aamriwe kuwalipa fidia ya Sh. bilioni 310 kutokana na kutangaza taarifa za kashfa dhidi yao.

Katika kesi yao ya msingi, wadai hao wanaiomba mahakama kuu katika hukumu yake, imwamuru Kafulila awalipe Sh. bilioni 210 kama fidia kutokana na kashfa hizo na hasara ya taswira ya biashara na hadhi yao.

Aidha,  imwamuru kuwalipa Sh. bilioni 100, kama fidia ya madhara ya jumla kutokana na usumbufu walioupata kutokana na taarifa za kashfa zilizotolewa dhidi yao na awaombe radhi kutokana na taarifa hizo,  gharama ya kesi, riba kwa kiasi cha fedha yote wanayodai kwa kiwango cha  asilimia cha mahakama kutoka tarehe ya hukumu hadi tarehe ya mwisho wa malipo hayo.
Pia, wanaiomba  mahakama kutoa amri nyingine itakazoona zinafaa.

Kwa kupitia hati yao ya madai ya kesi ya msingi, wadai hao wanadai kwa nyakati tofauti ndani na nje ya Bunge na kupitia mitandao ya kijamii, Kafulila ametoa maneno ya kashfa dhidi yao kwamba wamejipatia fedha katika akaunti ya Escow iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa njia zisizo halali.

Wadai hao wanadai IPTL iliingia mkataba na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) la kuisambazia umeme na imekuwa ikitekeleza majukumu yake kama walivyokubaliana.

Inadaiwa IPTL ilikuwa na mgogoro na kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited na Tanesco ambapo Sh. bilioni 200 zilihifadhiwa katika akaunti ya Escow iliyofunguliwa BoT, kusubiri kumalizika kwa mgogoro huo uliokuwa mahakama kuu.

Kwa kupitia hati hiyo inadaiwa kuwa baada ya kumalizika na kuhimitishwa kwa mgogoro huo, mahakama ilitoa amri ya IPTL kukusanya fedha hizo na BoT kutakiwa kuziachia.

 Wadai hao wanadai katika hali ya kushangaza na bila ya uhalali wowote, Kafulika katika shughuli mbalimbali nje na ndani ya Bunge na kupitia mitandao ya kijamii ya Jamii Forum, Twitter na Facebook alimua kusambaza taarifa za kashfa kwa IPTL na Mkurugenzi Mtendaji wake.
Inadaiwa Juni, 2014, Kafulila alichapisha taarifa za kwamba IPTL na Seth walijipatia fedha kutoka katika akaunti ya Escrow isivyo halali, wakati si kweli na imehusika katika vitendo viovu vya kuchukua fedha katika akaunti hiyo.

Kupitia hati hiyo, inadaiwa Kafulila amekuwa akitoa taarifa za kashfa, kwa kumtaja Seth kwa jina la Singasinga, jambo ambalo siyo sawa na hivyo kumharibia sifa yake na kumsababishia uendeshaji wa biashara zake zinazotekelezwa na IPTL na PAP kudorora.

Inadaiwa kutokana na taarifa zilizotolewa na Kafulila, ameisababishia jamii kuamini kuwa ni kweli IPTL imejipatia fedha hizo katika akaunti ya Escow bila uhalali na zimesababisha hasara au kupungua kwa hadhi ya kampuni hizo.

Hata hivyo, wadai hao wanadai Kafulila akiwa mbunge ana kinga ya kutochukulia hatia za kisheria kwa masuala ambayo ameyasema bungeni, lakini amekuwa akitoa taarifa za kashfa dhidi ya wadai ndani na nje ya shughuli za bunge.

Wadai hao wanadai taarifa zilizosambazwa na Kafulila mbali ya kuwashushia hadhi pia zimesababisha hasara ya kibiashara na ameendelea kufanya hivyo licha ya kupewa  taarifa ya maneno na ya maandishi.

Ilidaiwa kutokana na taarifa hizo, Kafulila amesababisha hadhi ya kampuni hizo kushuka sio tu nchini bali hata kimataifa, hivyo kuwasababishia hasara kibiashara na  madhara ya kisaikolojia na usumbufu kwa menejimenti.

Wadai hao wanadai kitendo cha Kafulila kuelezea mambo yaliyotokea katika mahakama za kisheria kuhusu maombi baina ya IPTL na kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited kimesababisha si tu kuingilia uhuru wa mahakama bali pia hasara kwa IPTL, wakati alikuwa akijua kilichoendelea mahakamani.

Inadaiwa IPTL inatoa huduma ya kuisambazia umeme Tanesco, hivyo kutokana na taarifa za mdaiwa zimehatarisha uhusiano baina yake na shirika hilo hivyo kusababisha kudorora kwa uchumi na biashara yao.
 
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa