Home » » ‘Nilijitahidi, sikumuwahi Ballali akiwa hai’

‘Nilijitahidi, sikumuwahi Ballali akiwa hai’

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Margaret Mpango akizungumza na mwandishi wa gazeti la Mwananchi, nyumbani kwake mkoani Kigoma. Na Mpigapicha Wetu  

Margaret Ballali ambaye ni dada mdogo wa aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Ballali ameeleza jinsi alivyojitahidi kumuwahi kaka yake kabla ya kukutwa na mauti, lakini alishindwa na badala yake akaambulia kutoa heshima za mwisho na kushiriki mazishi.
Margaret alisema alikwenda Marekani kutokana na wito alioupokea Mei 12, 2008, saa 11:00 jioni kutoka kwa wifi yake (mke wa Ballali, Anna Muganda), akimtaka afanye haraka kwenda nchini humo kwani hali ya kaka yake (Ballali) haikuwa nzuri na kwamba alikuwa akihitaji kuzungumza naye.
“Taarifa hiyo ilinishtua sana maana wifi aliniambia nifanye nifanyavyo kutafuta ndege mapema kadri inavyowezekana ili niende, maana hali ya kaka ilikuwa mbaya, kwa hiyo nilijipanga na kwa sababu Mzee (Askofu Dk Gerald Mpango) alikuwa huko kwa shughuli za kikazi, nilimwarifu ili ikiwezekana tukutane (Washington) DC,” alisema Margaret ambaye ni mke wa Askofu Mpango wa Kanisa la Anglikana.
Alisema kutokana na kwamba alikuwa Kigoma wakati huo, ilimchukua siku tatu kuanza safari, hivyo alisafiri kwa ndege ya Swiss Air, Mei 15, 2008 na kutua Uwanja wa JF Kennedy, New York Marekani Mei 16, saa 4:00 asubuhi, siku ambayo Ballali alifariki dunia.
“Nikiwa njiani na hata baada ya kutuas JFK, nilikuwa nawasiliana na wifi. Alionekana kama mtu aliyekata tamaa na alikuwa akiniuliza niko wapi kila wakati, nilikuwa nikisubiri ndege hapo kwa saa kama mbili. Bahati mbaya ni kwamba baada ya kucheck inn (kuidhinishwa kusafiri na kuingia sehemu ya kusubiria ndege), gurudumu lake moja lilipasuka,” alisema.
“Hili jambo halikuwa la kawaida kwasababu ilibidi sasa tushuke na tusubiri tena kwa saa kama mbili ili tubadilishiwe ndege, na wakati nikiwa bado uwanjani hapo JFK, ilikuwa kama saa 8:00 mchana, nilipata simu kutoka kwa wifi akiniambia ‘Mage we have lost Daudi’ (Margaret, tumempoteza Daudi (Ballali).”
Alisema hakuwa na cha kufanya zaidi ya kuendelea na taratibu za safari na kwamba alipowasili Washington muda wa jioni alikwenda moja kwa moja kwenye nyumba ya kuhifadhia maiti ya Vo Funeral Home ambako aliwakuta wanafamilia, akiwamo Mama Muganda, watoto wa Marehemu Rahel na Octavio pamoja na wauguzi wawili na madaktari wakiwa wamezunguka kitanda cha marehemu, kabla ya mwili wake kuhifadhiwa.
Alisema baada ya hapo walirejea nyumbani na kuanza kupanga taratibu za mazishi, ambayo yalifanyika Mei 23, 2008 katika makaburi ya Gate of Heaven eneo la Silver Spring, Maryland, Marekani, huku mumewe, Dk Mpango akiwa miongoni mwa walioongoza ibada ya maziko ya kiongozi huyo.
Umahututi wake
Baadhi ya ndugu wa Ballali wanasema kubadilika ghafla na kuwa mahututi kuliwashtua kutokana na kutokuwapo kwa taarifa za mapema kuhusu ugonjwa wake.
Wanasema Ballali aliondoka Agosti 2007 kwenda Marekani akiwa mzima na hawakuwa na taarifa zozote kwamba ni mgonjwa, lakini walishtushwa na taarifa za kuugua kwake ghafla kiasi cha kuambiwa kwamba alikuwa mahututi.
Ballali alilazwa katika Hospitali ya Massachusetts, Boston mwishoni mwa Agosti 2007, wakati alipokwenda kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake na tangu wakati huo afya yake haikuimarika hadi alipofariki dunia, Mei 16, 2008 akiwa nyumbani kwake Washington DC.

Kabla ya kifo chake, alilazwa kwa mara ya katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Georgetown lakini alirejeshwa nyumbani baada ya madaktari wa hospitali hiyo kumwambia kwamba asingeweza kupona. Alifariki wiki mbili baadaye.
Margaret, kwa upande wake, alisema awali walishtushwa na taarifa kwamba Ballali yu mahututi na kwamba ilikuwa vigumu kuamini kwa sababu kabla ya hapo hawakuwa na taarifa zozote za ugonjwa wake.
 “Mimi nilipata taarifa kwamba kaka (Ballali) amekwenda Boston kwa ajili ya medical checkup (uchunguzi wa afya), lakini ghafla niliarifiwa amelazwa na muda mfupi tukapewa taarifa nyingine kwamba yuko mahututi, kweli nilishtuka,” alisema Margaret.
Kwa upande wake, Pascal, ambaye ni mdogo wa Ballali alimwambia mwandishi wa Mwananchi nyumbani kwake katika Kijiji cha Luganga wilayani Mufindi, Iringa akisema: “Taarifa za kuumwa kwake zilitushtua, maana nilikutana naye siku chache kabla ya safari yake ya kwenda Marekani na wakati huo alikuwa ametoka Dodoma, kwa jinsi nilivyomwona hakuwa mgonjwa.”
Ballali aliondoka nchini wakati kesi za wizi wa takriban Sh122 bilioni kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) zikiwa zimeshamiri. Ballali alitajwa kwenye kashfa hiyo kwa kuidhinisha fedha kinyume na taratibu. Kuondoka kwake kulizua maswali yake, hali kadhalika kuumwa na mazingira ya kifo chake ambayo yamefanya watu wengi wahoji.
ameachwa maswali mengi.
“Tulipokaa muda si mrefu tulipata tena taarifa kwamba kaka ni mgonjwa sana na yupo mahututi. Hapo wasiwasi wetu ulizidi maana kama unavyotuona huku ni mbali, hivyo taarifa kutufikia zilikuwa ni kidogo sana, kila tulipojaribu kufuatilia hatukupata taarifa zinazotosheleza”.
 Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa