Home » » VIJANA NCCR-MAGEUZI WATAKA WAREMA AJIUZULU

VIJANA NCCR-MAGEUZI WATAKA WAREMA AJIUZULU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema
Vijana wa Chama cha NCCR-Mageuzi wamemjia juu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, wakimtaka ajiuzulu au Rais Jakaya Kikwete amwajibishe, kwa madai kwamba, ameidhalilisha ofisi anayoitumikia na mamlaka na taasisi iliyomteua, kwa kumwita Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila tumbili.
 Pia wamemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, kuacha kile walichokiita vitisho, ubabe na ulevi wa madaraka.

 Tamko hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa Kitengo cha Vijana cha NCCR-Mageuzi Taifa, Deo Meck, alipozungumza na waandishi wa habari, makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam jana.

Alisema wanajiandaa kuanza ziara kuzunguka nchini kote kuendesha kampeni ya kuwahamasisha wananchi kuwabana viongozi hao wawajibishwe na fedha zote za umma zilizoibwa zirejeshwe.

Meck alisema ni aibu kubwa kwa Jaji Werema, ambaye anapaswa kuonyesha staha, kuheshimu haki za binadamu, kutambua na kuheshimu uumbaji wa Mungu, kuheshimu utu na ubinadamu, kuudhalilisha kwa kumuita binadamu tumbili.

“Hiyo ni dharau kubwa na tusi kubwa kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba hata tumbili anahudhuria na kuwa sehemu ya vikao vya Bunge na kuwa sehemu ya mjadala,” alisema Meck.

Aliongeza: “Si hivyo tu, bali ni kuwadhalilisha na kuwafedhehesha wakazi na wapigakura wa Kigoma Kusini kuwa wawanawakilishwa na tumbili bungeni. Tafsiri yake ni kuwa nao ni tumbili na wamemchagua tumbili mwenzao kuwawakilisha bungeni.”

“Tunamtaka mwanasheria mkuu wa serikali, Jaji Frederick Werema ajiuzulu au awajibishwe na mheshimiwa Rais kwa kuidhalilisha ofisi anayoitumia na pia mamlaka na taasisi iliyomteua.”

Aidha, alimtaka Maswi kufahakuwa majibu ya hoja siyo ngumi na kwamba, kama ana fikra hizo, basi hajui dhamana na wajibu aliopewa na kuaminiwa kuwa anaweza kuubeba.

Alisema ni aibu kubwa kwa mwanasheria mkuu wa serikali na katibu mkuu wa wizara ya nishati na madini kutokujali kwa kiwango kikubwa utu wa Mtanzania.

Pia alisema ni aibu kwa viongozi hao kutokuwa hata na chembe ya uzalendo, kudhalilisha familia zao, kudhalilisha ofisi wanazosimamia, kudhalilisha elimu na taaluma zao, kuonyesha jinsi gani elimu hazijawasaidia kujitambua na kudhalilisha shule na vyuo walivyosoma na kudhalilisha walimu waliowafundisha.

 Hivyo, aliwataka kujua kuwa vitisho havina uwezo wa kufifisha harakati za kuwawajibisha na kwamba, wanapaswa kujua kuwa hawana uwezo wa kuwapiga ngumi Watanzania wote.

Alisema kama kudai na kutetea maslahi na rasilimali za umma ni kuitwa tumbili, basi wako tayari kuitwa hivyo, lakini fedha za wananchi zirudishwe.

Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono katika ziara zinazotarajiwa kufanywa na chama hicho nchini kote.Juni 25, mwaka huu, wakati akitoa ufafanuzi wa mwongozo ulioombwa na Kafulila bungeni kuhusu fedha zilizokuwa katika akaunti ya Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambazo zimelipwa kwa kampuni ya PAP inayomiliki mitambo ya kampuni ya umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Jaji Werema aliteleza ulimi kwa kumuita mbunge huyo tumbili.

 Naye Maswi alimtaka Kafulila kuonyesha kile alichokiita uanaume wake kwa kuzungumzia tuhuma zake akiwa nje ya Bunge.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa