Home » » ATOA SOMO KUHUSU POLISI JAMII

ATOA SOMO KUHUSU POLISI JAMII

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KAMISHNA wa Polisi Jamii nchini, Mussa Alli Mussa, amewataka wadau wa ulinzi na usalama, maofisa wa polisi na askari kote nchini, kuhakikisha wanaielewa dhana ya polisi jamii kwa ufasaha.
Amesema dhana hiyo ni msaada mkubwa katika kupambana na matukio ya uhalifu na wahalifu na ikiwa wadau hawaielewi, haiwezi kufanikiwa.
Alitoa kauli hiyo juzi alipokutana na baadhi ya watendaji wa Jeshi la Polisi mkoani Kigoma katika Wilaya ya Buhigwe na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo. Alisema hayo katika kikao cha pamoja kuhusu utendaji kazi katika dhana ya Polisi Jamii.
Mkutano huo ulilenga pia jinsi jeshi hilo linavyoweza kutoa huduma bora kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na jinsi wananchi wanavyoshirikishwa kutambua viashiria vya uhalifu na wahalifu katika maeneo yao.
Mussa alisema tangu ilipoanzishwa, dhana ya Polisi Jamii ina lengo la kushirikisha kila mtu katika kazi ya kulinda amani na usalama.
Alisema mafanikio makubwa yamepatikana hadi sasa, ambapo makundi kadhaa ya uhalifu, yamegundulika na kuchukuliwa hatua za kisheria na kumalizwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Jafari Ibrahim, aliwataka wakazi wa wilaya hiyo kushiriki kikamilifu katika kutekeleza dhana ya polisi jamii, kulingana na nafasi zao ndani ya jamii.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa