Home » » KIGOMA WATAKIWA KUCHANGAMKIA MAONYESHO YA WAJASIRIAMALI

KIGOMA WATAKIWA KUCHANGAMKIA MAONYESHO YA WAJASIRIAMALI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
WANANCHI wa Manispaa ya Kigoma Ujiji wametakiwa kutumia fursa waliyoipata ya maonyesho ya wajasiriamali wadogo na wa kati Kanda ya Kati kwa kujitangaza kibiashara na kujifunza kutoka kwa wenzao ndani na nje ya nchi.
Akizungumza mjini hapa jana katika kikao kilichohusisha viongozi wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo vidogo (Sido), na Waandishi wa Habari, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kanali mstaafu Issa Machibya, alisema maonyesho hayo yatafanyika Community Centre kuanzia Agosti 27 hadi Septemba Mosi na kujumuisha mikoa mbalimbali ya hapa nchini pamoja na nchi za Kenya, Uganda, DRC na Burundi.
Alisema kuwa maonyesho hayo hufanyika kwa mwaka mara moja nchini na mwaka huu Mkoa wa Kigoma umepata nafasi hiyo, hivyo wananchi wanatakiwa kutumia fursa hiyo kujitangaza na kujifunza, kwani itachukua miaka mingi kujirudia tena.
Machibya, alisema kutakuwepo na waonyeshaji 302 ambao wamethibitisha kushiriki kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania na nje ya nchi, pia Taasisi mbalimbali za serikali na binafsi zitakuwepo kama TBS, NMB, Tanapa, Benki ya Posta na nyinginezo.
Aliongeza kuwa lengo la maonyesho hayo ni kuwawezesha wajasiriamali wadogo wa hapa nchini, kupata fursa ya kukuza soko la bidhaa zao hususan mikoa ya kanda ya kati na nje ya nchi, pamoja na kujifunza kutoka kwa wenzao wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, Machibya aliongeza kuwa kauli mbiu ya maonyesho hayo ni ‘Buni, Boresha, Fanya Biashara Kupitia Sido’.
Naye Meneja wa Sido mkoani hapa, Macdonard Maganga, alisema pamoja na wajasiriamali kuja katika maonyesho hayo kwa lengo la kuonyesha bidhaa zao, lakini pia ni fursa nzuri kwa wananchi wa hapa nchini kujitangaza, pia kuchukua ujuzi kutoka kwa wageni.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa