Home » » HIZI NDIZO SIFA ZA MWALIMU BORA- 2

HIZI NDIZO SIFA ZA MWALIMU BORA- 2

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Katika makala iliyopita tuliangalia baadhi ya sifa anazotakiwa kuwa nazo mwalimu. Katika makala haya tutaendelea na sifa nyingine.
Moja kati ya sifa kubwa ambayo mwalimu anatakiwa kuwa nayo ni ushirikiano kati yake na walimu wenzake, wanafunzi na wazazi kwa jumla.
Ushirikiano na walimu wenzake utamwezesha kufanya kazi yake vizuri, lakini pia kuboresha upeo wa fikra na taaluma kwa jumla.
Ama kwa upande wa wanafunzi, ushirikiano utaondoa kizuizi kati yake na wanafunzi na utawaweka huru wanafunzi kuweza kumhusisha pale wanapokuwa na matatizo mbalimbali.
Wazazi pia wanatakiwa washirikishwe katika kujua maendeleo ya watoto wao shuleni. Katika kufanikisha hili mwalimu ana nafasi kubwa.
Pia, mwalimu anatakiwa awe muumini mkubwa wa nidhamu. Mwalimu anatakiwa asifumbie macho vitendo vya utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi na avikemee bila kupepesa macho.
Hivi sasa kuna changamoto kubwa katika kudhibiti nidhamu za wanafunzi ukizingatia kuwa adhabu ya viboko imekatazwa shuleni. Lakini pamoja na kukatazwa huku kwa adhabu ya viboko bado mwalimu ana wajibu wa kutumia mbinu mbadala katika kudhibiti nidhamu za wanafunzi.
Ikumbukwe kuwa nidhamu ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya taaluma. Katika kudhibiti nidhamu mwalimu anatakiwa yeye mwenyewe ajiheshimu. Haipendezi kumwona mwalimu akiwa amevaa mavazi yasiyo na stara yanayoonesha utupu kwa wanawake au kuvaa mlegezo kwa wanaume.
Pia, kujichora katika mwili au kuvuta bangi na dawa za kulevya. Huwezi kudhibiti nidhamu za wanafunzi kama wewe mwenyewe hujiheshimu.
Mwalimu hatakiwi kuwa mwoga na kuogopa kukosolewa katika masuala yanayohusu taaluma. Uthubutu ni katika sifa zilizotukuka za mwalimu. Mwalimu anatakiwa awe na uwezo wa ziada wa kuchagiza maendeleo ya wanafunzi na kutatua matatizo mbalimbali yanayohusu taaluma na wanafunzi kwa jumla.
Anatakiwa awape moyo wanafunzi wake nao wajifunze kutoka kwake ili waweze kufanikiwa kitaaluma na kimaisha.
Mwalimu anatakiwa awe na uwezo wa kuwahusisha wanafunzi wake ili waweze kufuatilia masomo darasani. Wanafunzi wana maarifa mbalimbali ambayo mwalimu pia anaweza kunufaika nayo akitaka.
Usiwachukulie wanafunzi wako kama watu wasio na kitu kichwani na usitawale darasa kana kwamba wewe ndiye mjuzi wa kila jambo. Washirikishe na wajengee wanafunzi wako uwezo wa kujiamini na kutenda na huu ndiyo msingi mkubwa katika maendeleo ya taaluma.
Kuwa na moyo wa huruma na kusamehe ni sifa iliyotukuka ya mwalimu. Mwalimu si mtu wa kuendekeza malumbano yasiyo na tija kwa wanafunzi wake na walimu wengine. Mazingira ya amani na utulivu shuleni ni muhimu kwa maendeleo ya taaluma.
Sifa ni nyingi, lakini ningependa tutosheke na hizi chache ambazo zinaweza kuwakumbusha walimu thamani yao na umuhimu wao katika kuendeleza taaluma.
Ni vizuri nikiwakumbusha walimu kuwa ualimu ni mojawapo ya kazi tukufu kabisa katika historia ya mwanadamu na hakuna jamii yoyote iliyofanikiwa bila ya kuwa na walimu bora.
Hivyo, pamoja na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo, wajithamini na watambue kuwa wana mchango mkubwa katika kuikomboa jamii kutokana na adui ujinga na hatimaye kuiletea maendeleo.
Rajabu Kipango ni mwalimu na mtaalamu wa rasilimali watu.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa