Home » » MACHINJIO YA UJIJI YAFUNGWA

MACHINJIO YA UJIJI YAFUNGWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
MAMLAKA ya Chakula Dawa na Vipodozi  nchini (TFDA), imetoa amri ya kufungwa kwa machinjio ya Kibirizi endapo haitafanyiwa marekebisho huku ile ya Ujiji ikifungiwa kutokana na kutokukidhi vigezo vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za afya ya mwaka 2003.
Hatua hiyo imetokana na ziara ya mamlaka kuona upungufu uliyopo, ambako kuna uwezekano mkubwa wa kusababisha athari za kiafya kwa wananchi kutokana na magonjwa ya mlipuko.
Akitolea ufafanuzi hatua hiyo, Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mganga wa Mifugo, Dk. John Shauri, alisema hatua hiyo imechukuliwa Septemba 15 mwaka huu baada ya kubaini upungufu na kutoa onyo la kutotumika hadi hapo marekebisho yatakapofanyika.
Alitaja baadhi ya sababu zilizosababisha kufungwa kwa machinjio ya Ujiji kuwa ni pamoja na kuchakaa kwa jengo, kutuama kwa maji katika sakafu kutokana na mashimo, kutokuwepo kwa uzio, kukosekana kwa shimo la kutupia nyama iliyozuiliwa kutumiwa, kutokuwepo kwa choo pamoja na maji.
“Kutokana na vigezo hivyo kutokuonekana pale, wao kama mamlaka iliyopewa jukumu la kisheria wamefunga machinjio yale kuendelea kutumika hadi pale yatakapojengwa upya kwa kuzingatia vigezo vinavyotakiwa kitaalamu kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2003,” alisema Dk. Shauri.
Aidha, Shauri akitolea ufafanuzi machinjio ya Kibirizi, alisema kutokana na kasoro ndogo ndogo zilizopo ikiwemo uzio, ilitolewa amri ya kufanyiwa marekebisho ya haraka ili wananchi waendelee kupata huduma ya mboga kama kawaida.
“Machinjio ya Kibirizi yaliachwa kwa sababu mapungufu yake yalikuwa madogo ukilinganisha na machinjio ya Ujiji, ambayo yana mapungufu mengi na tayari uzio umeshawekwa ili kuzuia mbwa na wanyama wengine wasiingie sambamba na marekebisho mengine,” alisema.
Naye Laini Ramadhani, ambaye ni wakala wa usambazaji wa nyama, alisema kuwa kufungwa kwa machinjio ya Ujiji hakuna haki iliyotendeka, kwani imekuwa ghafla na cha kushangaza ni kuacha eneo la Kibirizi kuendelea kufanya kazi na wakati mazingira yanafanana.
“Kama wanafuata haki… basi wangetoa barua kabla ya kuja kufunga ili sisi tujue cha kufanya baada ya kufungwa na kutafuta namna ya kurekebisha  mapungufu yanayoonekana,” alisema Ramadhani.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mnazi Mmoja ambako machinjio ya Ujiji inapatikana, Nuru Sadiki, alisema anaunga mkono kufungwa kwa machinjio hiyo kutokana na kukosa sifa za usafi.
“Kutokana na mapungufu mengi yaliyoko katika machinjio hii, ilikuwa ni lazima ifungwe kwani hatuko tayari kuona wananchi wakipata magonjwa, pia hata ile ya Kibirizi kama nayo ina hali hii basi nayo inatakiwa kufungwa ili kupisha marekebisho ambayo yatawafanya wananchi kupata nyama iliyotoka katika mazingira masafi” alisema Sadiki.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa