Home » » MSAJILI ACHUNGUZA VYAMA VYA SIASA

MSAJILI ACHUNGUZA VYAMA VYA SIASA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
 
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imeanza kupitia katiba za vyama vya siasa ambavyo havijafanya uchaguzi, ili kubaini hatua za kuchukua.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alisema ingawa kila chama kina katiba yake na taratibu za kujiendesha, wako katika hatua ya uhakiki wa vyama kwa nia ya kuhakikisha sheria ya vyama vya siasa inazingatiwa.

“Kuna zoezi la uhakiki wa vyama, tunaangalia kama chaguzi zimefanyika kwa mujibu wa katiba za vyama husika … tunafahamu wengi bado hawajamaliza, lakini kila mmoja ana sababu zake,” alisema.Bila kutaka kuingia kwa undani aliongeza kuwa: “Kwa sasa tupo kwenye kazi nzito ya kupitia katiba za vyama ili kujua wapi wamekiuka na wapi wapo ndani ya mstari.”

Ofisi ya Msajili inajipanga kuhakiki vyama, serikali imekwisha kutangaza kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika Desemba 14, mwaka huu ambao wadau wakubwa ni vyama vya siasa.

 Taarifa za uchunguzi zinasema kuwa baadhi ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu vinavyotarajiwa kushiriki uchaguzi huo, havijafanya uchaguzi wa viongozi wake kinyume cha sheria ya usajili wa vyama vya siasa ya mwaka 1992.

Kifungu cha 258 cha Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992, Sehemu ya  8 (1)  inasema: “Hakuna chama cha siasa kitakachostahili kupata usajili wa muda kama…..”,Sehemu ya 8 (2) kifungu kidogo cha kwanza kinasema; “Hakuna chama kitakachostahili kupata usajili wa muda kama katiba au sera yake … hairuhusu uchaguzi wa kidemokrasia na wenye kipindi/muhula unaoeleweka wa viongozi wake.

Sharti  la usajili wa muda ndilo linalotoa sifa ya kupata usajili wa kudumu kwa chama cha siasa, na kwa hali hiyo vyama visivyofanya uchaguzi wa viongozi katika muda unaoelezwa na katiba ya vyama vyao vinakuwa vimepoteza  sifa ya kuendelea kuwa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria hii.

Vyama vingi vya siasa nchini vimejiwekea utaratibu wa kufanya chaguzi baada ya miaka mitano.

Uchunguzi wa NIPASHE unaonyesha kuwa baadhi ya vyama hivyo ambavyo havijafanya uchaguzi kinyume cha sheria ya vyama vya siasa inayovitaka kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano ni pamoja na Sauti ya Umma (Sau), United Democratic Party (UDP), Tanzania Labour (TLP), National Reconstruction Alliance (NRA), Union for Multiparty Democracy (UMD), Democratic Party (DP) na APPT Maendeleo.

Vyama vingine ni Chama cha Wakulima Tanzania (AFP), United People’s Democratic Party (UPDP) na National League for Democracy (NLD).

Sheria namba 5 ya vyama vya siasa inavitaka vyama vyote vyenye usajili kuhakikisha vinafanya uchaguzi wake wa viongozi ndani ya kipindi cha miaka mitano na visipofanya hivyo Msajili wa Vyama vya Siasa ana mamlaka ya kisheria kuvichukulia hatua vyama husika.

Vyama ambavyo huko nyuma vilifutwa kutokana na pamoja na mambo mengine kushindwa kufanya chaguzi ni Tanzania People’s Party (TPP) kilichokuwa kinaongozwa na Dk. Alec Humphrey Chemponda na Popular National Party (Pona) kilichokuwa kinaongozwa na Hayati Wilfred Kwakitwange.

Vyama hivyo vilifutwa na aliyekuwa msajili wa wakati ule, Hayati George Liundi.Mwenyekiti wa Taifa wa APPT Maendeleo, Peter Kuga Mziray, akizungumza na NIPASHE akiwa nje ya nchi ambako amekwenda kwa ajili ya matibabu, alisema ni kweli chama chake hakijafanya uchaguzi.

 “Kila chama cha siasa kina utaratibu wake wa kipindi cha uongozi. Hakuna sheria yoyote kwa sasa kuhusu kipindi cha uongozi kwa vyama. Ila sheria ya vyama vya siasa inasema vyama vifuate katiba zao,” alidai Mziray.

 Mziray ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, alisema chama chake uongozi wake ni miaka sita hivyo kwa kuwa mkutano mkuu ulifanyika mwaka 2009 miaka sita inaisha mwakani.

“Tumefanya hivi ili mkutano mkuu uendane na uteuzi wa mgombea urais kwa kuwa chama hakina fedha kama CCM, CUF na Chadema, kwa hiyo tuko sawa sawa, muda ukifika tutatoa taarifa,” alisema.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila, alisema chama chake hakijafanya uchaguzi kwa sababu viongozi wake waliopo sasa wana shughuli nyingi.“Sisi kwanza tunashugulikia kesi, hatuna haraka, ni kesi ya kudai uhuru wa Tanganyika ndiyo kipaumbele chetu ndani ya chama,” alisema.

Mtikila, alisema kiutaratibu chama chake kilitakiwa kifanye mkutano mkuu wa uchaguzi Julai mwaka huu, na kwamba kesi hiyo ikiisha uchaguzi wa viongozi utafanyika mara moja. Hata hivyo, hakueleza ni lini kesi hiyo itakwisha.
Aliongeza kuwa pamoja na kutofanyika uchaguzi ndani ya chama, chama hicho kitashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa wa Desemba mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani kwa kuwa kinaamini kuwa chaguzi hizo siyo lazima kuwa na safu ya mpya ya viongozi bali ni mbinu tu zinazotumika kukiwezesha chama husika kupata ushindi.

Naye Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema, alipoulizwa kuhusu chama chake kitafanya lini mkutano mkuu wa uchaguzi, alisema suala hilo aulizwe Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu wa TLP, Jeremia Shelukindo, alipotafutwa hakupatikana, lakini Naibu Katibu Mkuu, Nancy Mrikaria, alisema ni kweli chama hicho bado hakijafanya uchaguzi wa viongozi kutokana na matatizo fulani.

 “TLP bado hatujafanya uchaguzi kutokana na masuala fulani ndani ya chama chetu, hayo mambo yakiisha tutafanya uchaguzi ndani ya mwaka huu,” alisema huku akishindwa kuweka wazi ni matatizo gani yaliyopo ndani ya chama.

Hata hivyo, wiki iliyopita Mrema alipolalamikiwa na baadhi ya wanachama wanaodai kupeleka barua kwa msajili wa vyama kupinga uongozi wa sasa kutokana na kukiuka katiba ya chama hicho kwa kutofanya uchaguzi tangu Januari mwaka huu, alisema katiba inaonyesha kuwa ukomo wa uongozi wake uliishia Aprili, mwaka huu.

Hata hivyo, Jaji Mutungi alisema chama cha TLP walimuandikia barua ya kuomba kusogeza mbele uchaguzi wao, na baada ya muda baadhi ya wanachama wa chama hicho walipeleka barua ya kutaka chama hicho kufanya uchaguzi.

Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, hakutaka kutoa ufafanuzi zaidi ya kusema: “Siyo kila kitu kinachofanywa na Chadema ni lazima na wengine wafanye, sikia sisi uongozi wetu unaishia mwaka 2016, na hizo chokochoko zote ni Chadema.”

Alipoulizwa uchaguzi wa mwisho wa chama hicho ulifanyika mwaka gani, Cheyo alisema huo ni upumbavu kisha kukata simu.

Katibu Mkuu wa AFP, Rashid Rai, alisema wanatarajia kufanya uchaguzi mwaka 2017, kwa kuwa uongozi wa chama hicho uliopo madarakani hivi sasa unatarajiwa kumaliza muda wake Aprili mwaka huo (2017).

Alisema uchaguzi wa mwisho uliowaingiza viongozi waliopo madarakani hivi sasa, ulifanyika mwaka jana.Mwenyekiti wa NLD, Dk. Emmanuel Makaidi, alisema chama chake tayari kimekwisha kufanya uchaguzi wa viongozi wake waliopo madarakani hivi sasa tangu Agosti, mwaka jana.

 Hivyo, akasema wataitisha tena uchaguzi mwingine baada ya viongozi wa sasa watakapomaliza muda wao wa uongozi baada ya miaka mitano ijayo kama sheria inavyotaka.
“Sisi kwa hilo tuko makini sana,” alisema Dk. Makaidi.

UPDP kimesema hakina mpango wa kufanya uchaguzi wake wa ndani kwa lengo la kujiandaa na uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa.Badala yake chama hicho kimedai kuwa kinaendeleza mapambano dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na Chama cha Wananchi (CUF) ili kuviangusha, kwa madai kuwa vyama hivyo ndivyo kikwazo cha demokrasia nchini.

Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa, alisema kuwa Chadema na CUF vinakwamisha maendeleo ya demokrasia nchini hivyo chama chake hakitashiriki uchaguzi wowote mpaka kwanza kifanikiwe kuviangusha vyama hivyo.

“Suala la kufanya uchaguzi wetu wa ndani halipo, sisi kwanza tumeamua kupambana na Chadema na CUF mpaka tuviangushe kwa sababu tumegundua vyama hivyo ndiyo kikwazo kikubwa cha demokrasia nchini,” alisema Dovutwa.

Hata hivyo, alipotakiwa kueleza ni namna gani ataviangusha vyama hivyo, Dovutwa alisema kuwa hawezi kuanika hadharani mbinu za mabambano yake kwa vile mbinu hizo zikijulikana dhamira yake haitafanikiwa
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa