Home » » SEFUE AWACHEFUA WABUNGE

SEFUE AWACHEFUA WABUNGE


Wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitarajiwa kumkabidhi Spika wa Bunge, Anne Makinda ripoti ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG) kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow kufuatia madai ya uchotwaji wa Dola za Marekani milioni 200 (Sh. bilioni 320), jana wabunge walichachamaa wakiituhumu serikali kuingilia uhuru wa Bunge.

Wabunge hao walionyesha wasiwasi juu ya uwezekano wa kutowasilishwa bungeni kwa ripoti za uchunguzi wa kashfa hiyo kwenye akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) uliofanywa na CAG na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Ilidaiwa na baadhi ya wabunge kwamba kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ya kuwakemea wabunge kuingilia suala linalohusu kashfa hiyo kwa kutaka liharakishwe ni kuingilia Bunge.

Wameshutumu kitendo hicho cha Balozi Sefue wakikiita kuwa ni kuingilia maamuzi ya Bunge ambalo ni mhimili ulio huru unaojitegemea.

Wasiwasi huo uliibuliwa na Peter Serukamba (Kigoma Mjini-CCM) na Mohammed Habib Mnyaa (Mkanyageni-CUF) kupitia miongozo waliyoiomba kwa Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, bungeni jana.

SERUKAMBA
Wa kwanza kuomba mwongozo huo alikuwa ni Serukamba, ambaye alisema kashfa inayoihusu  IPTL ni kubwa, ambayo imesababisha wahisani kusimamisha kuisaidia Tanzania fedha, miradi ya maendeleo inasuasua, hali ya nchi kwenye masoko ya fedha duniani ikiwa mbaya kwa sababu ya jinai hiyo.

“Nimesimama hapa mheshimiwa mwenyekiti niliombe Bunge lako, nina amini pamoja kwamba jambo hili umekuwa ukisema liko kwenye ratiba, kwa wale waliosikia TBC leo (jana) asubuhi, serikali wanasema bado wanaendelea na ripoti,” alisema na kuongeza:

 “Na maana yake ni nini? Tutafika mpaka tarehe 26 serikali watasema ripoti bado. Na mimi ningewashangaa wangesema iko tayari.”

Kutokana na hali hiyo, aliliomba Bunge kuchukua mamlaka yake ya kibunge pamoja na wabunge wamuombe Spika aunde kamati teule ili washughulikie suala hilo.

“Tukitegemea serikali italeta ripoti hapa, tutaondoka Bunge hili limekwisha ripoti haijaja,” alisema Serukamba.

Aliongeza: “Tutakuwa watu wa ajabu sana, watu wanakufa mahospitalini, miradi ya maendeleo imesimama, jina letu linachafuliwa duniani, halafu sisi na Bunge lako liendelee kukaa kimya, tukisema tunasubiri tutaletewa ripoti, wakati tunao uwezo wa kikanuni kuunda tume teule wenyewe, twende tulichunguze hili jambo, ili jambo hili liishe tuendelee na kazi ya maendeleo.”

MNYAA
Mnyaa akiomba mwongozo huo, alisema mhimili wa Bunge unatakiwa uwe huru unaojitegemea na kwamba, kwa kitendo chochote cha kuingiliwa maamuzi yake, linatakiwa lisimame liwe kali na kutoa maamuzi.

Alisema ishara juu ya Bunge ya kuingiliwa katika maamuzi yake alizozizungumza juzi bungeni, zimeanza kutokea jana.

“Kwamba, jana (juzi) Katibu Mkuu Kiongozi anawakemea wabunge wasiingilie suala hili la Escrow,” alisema Mnyaa.

Aliongeza: “Naomba kiti kitoe ufafanuzi, kwamba mbona sasa badala ya Bunge kuisimamia serikali kwa ibara ya 63 (ya katiba ya nchi), leo serikali inatoa maagizo kwanini (wabunge) tuliharakishe suala hili, tuliache wakati kiti chako kupitia Spika wa Bunge alitoa siku 45 kwa ripoti kuwasilishwa. Leo zimeshapita mara mbili na nusu."
“Naomba mwongozo kwa nini Bunge sasa linaingiliwa na haliko huru?”

Akijibu miongozo hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Zungu aliiagiza Kamati ya Uongozi ya Bunge kukutana na kujadili jambo hilo na kuitaka serikali kujiandaa kutoa majibu.

“Waheshimiwa wabunge haya mambo yamekuwa makubwa na inaelekea yanaendelea kuwa makubwa. Bunge lina nafasi yake katika kuisimamia serikali,” alisema Zungu.

 “Kwa hiyo, mwongozo wangu kwa yote haya mliyoyasema, naagiza kamati ya uongozi ikutane saa 7, kuyajadili haya yote ambayo yamesemwa hapa, na serikali mjiandae kutoa majibu kwenye kamati ya uongozi, na ikibidi kamati ya uongozi ifuate katiba basi saa 11 jioni tutakupeni taarifa ya kamati ya uongozi.”

Tayari nchi wahisani zimetangaza kuikatia misaada serikali ya zaidi ya Sh. trilioni 1 kutokana na kashfa hiyo.

Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa kutokana na kutoelewana kuhusu gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na IPTL na kuuzwa Tanesco.


Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID), katika uamuzi wake wa Februari 2014, ilitoa hukumu kuonyesha kwamba Tanesco walitozwa kiwango cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa kwa IPTL.

Kwa uamuzi huo, ni dhahiri kwamba fedha zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye akaunti ya Escrow zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na Tanesco baada ya hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali, lakini badala yake fedha hizo zilitoweka ghafla 

WAZIRI MKUU KUMKABIDHI SPIKA RIPOTI YA CAG
Akitoa taarifa ya kikao cha Kamati ya Uongozi wa Bunge kuhusu mwongozo ulioombwa na Serukamba wa kutaka iundwe Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow, Zungu aliliambia Bunge katika kikao cha jioni kuwa kamati hiyo ilikutana jana mchana na kujadili mwongozo huo.

Alisema katika kikao hicho, kamati hiyo ilikukubaliana na taarifa ya serikali kuwa leo Waziri Mkuu atakabidhi kwa Spika wa Bunge ripoti ya CAG kuhusu suala hilo.
Zungu alisema baada ya ripoti hiyo kupokelewa, utaratibu wa kawaida wa kibunge utafuata kuipatia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

MAUAJI YA KITETO
Kuhusu mwongozo ulioombwa na Silinde kutaka Bunge lijadili mauaji yanayoendelea kati ya wakulima na wafugaji wilayani Kiteto, Zungu alisema Kamati ya Uongozi wa Bunge ilijadili mwongozo huo.

Alisema katika kujadili mwongozo huo, kamati imeazimia kwamba, serikali kupitia Waziri Mkuu itoe maelezo kwa kamati hiyo leo jioni juu ya jambo hilo na namna lilivyoshughulikiwa katika kipindi cha nyuma hadi sasa na kisha taarifa kamili kuhusu suala hilo itatolewa bungeni.

MWENENDO WA SERIKALI
Kuhusu mwongozo wa kutaka Bunge lijadili mwenendo wa kusuasua wa serikali ulioombwa na Rajab bungeni, Zungu alisema katika kujadili suala hilo, Kamati ya Uongozi wa Bunge iliazimia kwamba, suala hilo lijadiliwe katika kikao cha kamati hiyo pamoja na Waziri Mkuu kitakachofanyika leo jioni.

Hoja hiyo ilitolewa na Mbunge wa Ole (CUF), Rajab Mbarouk Mohammed, na kuungwa mkono na wabunge wote wa upinzani kwa kusimama bungeni.
Rajab alitoa hoja hiyo kupitia mwongozo wa spika aliouomba bungeni jana.

Aliomba mwongozo huo chini ya ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ibara hiyo inatamka: “Sehemu ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.”

Kwa kuzingatia ibara hiyo ya katiba ya nchi, alisema "Lazima tukubali kwamba, katika kipindi hiki, ambacho serikali hii inamalizia muda wake, kwa kweli serikali inaonekana ime-paralise (imepooza).”

Aliongeza: “Nakiomba kiti chako na nawaomba wabunge tusimame kama taasisi, tujadili mwenendo wa serikali. Malalamiko yamekuwa mengi, matatizo yamezidi.”


Alisema hali hiyo imekuwa mbaya kiasi kwamba, imefikia leo bungeni waziri mmoja anajibu maswali ya wizara nne.

Pia alisema jana Alhamisi kikanuni za Bunge, ilikuwa ni siku, ambayo Waziri Mkuu alitakiwa awepo bungeni kujibu maswali ya papo kwa papo ya wabunge, lakini hajaonekana na hakuna sababu zilizotolewa.

Alisema zaidi ya hivyo, jana Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, alidiriki kusimama bungeni na kauli ya serikali, ambayo haikuwamo kwenye orodha ya shughuli za wabunge za jana.

“Haya mambo yakoje?” alihoji Rajab.Aliongeza: “Mheshimiwa mwenyekiti, naomba niliombe Bunge lako na niwaombe wabunge, muungane na hoja yangu ya kwamba, sasa Bunge lifikie pahala lisimame kama Bunge lijadili mwenendo wa serikali, ili sasa kutimiza matakwa ya katiba kuweza kuishauri serikali.”

“Mheshimiwa mwenyekiti, naomba nitoe hoja ili Bunge lijadili mwenendo wa serikali.”
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa