Home » » POLISI WATAKIWA KUWA WAKALI USALAMA BARABARANI

POLISI WATAKIWA KUWA WAKALI USALAMA BARABARANI


JESHI la Polisi mkoani hapa limeombwa kuwa wakali katika kusimamia sheria za barabarani na kuepuka kupokea rushwa ili kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, David Lyamongi, ambako alibainisha kuwa ajali nyingi zinazotokea barabarani ni kwa sababu ya uzembe wa madereva kutokufuata sheria za barabarani.
Alisema kuwa, kosa moja linalofanyika barabarani husababisha vifo vya watu wengi, hivyo Jeshi la Polisi halina budi kuwa wakali kwa wote ambao hawafuati sheria, liwachukulie hatua kali itakayowafanya wajutie makosa yao.
“Nchi jirani ya Uganda ni kosa kubwa kabisa kwa dereva au abiria kuvunja sheria za barabarani, kwani hatua ni kali na huchukuliwa pale pale bila kusubiri taratibu nyingine,” alisisitiza Lyamongi.
Akizungumzia ajali zinazosababishwa na pikipiki (Bodaboda), Lyamongi alisema ni kundi ambalo sasa linakuja kasi kwa kuongoza ajali, vifo na majeruhi, kutokana na watumiaji wa vyombo hivyo kutofuata sheria za barabarani ikiwamo kutovaa kofia ngumu (Helmet), kwa dereva na abiria wake.
“Kila mmoja hapa ameshashuhudia kifo au vifo ambavyo vinatokana na ajali za pikipiki, dereva na abiria wanapoteza maisha kutokana na kutokuvaa kofia, hivyo nawaomba madereva na abiria wote wa pikipiki wasipuuze kuvaa kofia kabla ya kuanza safari, kwani huzuia vichwa kuumia mara ajali inapotokea,” alisema.
Hata hivyo, Lyamongi aliwataka wananchi kutambua jukumu la kulinda sheria za barabarani si la Jeshi la Polisi pekee, bali Watanzania wote kuacha kufanya vitendo vinavyohatarisha maisha wanapokuwa barabarani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Usalama Barabarani mkoani hapa, Kamishna Msaidizi (ACP), Michael Deleli, alisema kuwa ajali za barabarani zimekuwa kero na hatari kubwa  katika maendeleo ya Taifa, kwani wananchi wengi wanapoteza maisha na wengine kubaki na ulemavu wa kudumu kutokana na uzembe wa baadhi ya madereva.
Alisema kuwa, Jeshi la Polisi linayatumia maadhimisho haya ya wiki ya usalama barabarani ili kufikisha ujumbe maalumu kwa watumiaji wote wa barabara, pia kutoa elimu lengo likiwa ni kuwahamasisha na kuwakumbusha wajibu wa kila mmoja anapokuwa barabarani ili kuepuka ajali.

 Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa