Home » » KISWAHILI KWA WANAFUNZI.

KISWAHILI KWA WANAFUNZI.

 Tungo ni neno au kikundi cha maneno ambacho hudokeza taarifa fulani ambayo huweza kuwa kamili au isiyo kamili.
Tungo hujengwa na vipashio vidogovidogo kama vile mofimu, kirai, sentensi. Msingi wa tungo huanzia katika neno. Tungo neno huundwa na vipashio vidogo zaidi ya neno ambavyo ni mofimu au fonimu. Mfano a-na-kimb-i-a.
Tungo kirai ni kipashio cha kimuundo chenye neno moja au zaidi lakini kisicho na muundo wa kiima - kiarifu. Mfano; Kijana mtanashati, kitoto kichanga.
Kirai huwa ni kipashio cha kimuundo kisichokamilika; yaani ni kipashio kisichokuwa na muundo wa kiima – kiarifu kama zilivyo sentensi ambazo zinahusisha mtendaji wa tendo na tendo linalotendwa. Pia, kirai huainishwa kimuundo kulingana na neno kuu la kirai husika.
Kirai ni tungo, yaani ni aina mojawapo ya tungo, aina nyingine za tungo ni neno, kishazi na sentensi.
Kirai huweza kutokea upande wowote wa kiima au kiarifu katika sentensi.
Aina za virai ni kama ifuatavyo; Kirai nomino (KN), chenyewe neno lake kuu ni nomino. Ni kirai ambacho muundo wake umekitwa kwenye nomino.
Kirai kitenzi (KT) ni kirai ambacho kimekitwa katika kitenzi au katika uhusiano wa kitenzi na neno au mafungu mengine ya maneno.
Kirai kivumishi (KV) muundo wake umekitwa katika kivumishi. Kwa kawaida muundo huu huwa ni wa kivumishi na neno.
Kirai Kielezi (KE) haielekei kukitwa kwenye uhusiano wa lazima baina ya neno kuu la Kielezi isipokuwa miuundo inayohusika hapa ni ya maneno ambayo hufanya kazi pamoja katika lugha kama misemo, neno au maneno yanayofuata neno lililotangulia yakifafanua zaidi neno hilo.
Virai viunganishi (KV) muundo wake umekitwa katika uhusiano na neno kuu la kwanza ambalo huwa kivumishi.
Mathalan, kishazi ni tungo yenye kitenzi ambacho chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea chenyewe.
Namna ya kubaini vishazi; Kishazi hupatikana katikaa au ndani ya sentensi. Lazima kishazi kiwe na kitenzi, sehemu yoyote ya sentensi isiyo na kitenzi, haiwezi kuwa kishazi. Kishazi huru hutawaliwa na kishazi kikuu na kishazi tegemezi hutawaliwa na kishazi tegemezi.
Baadhi ya vishazi huweza kujitegemea kama sentensi hata vikiondoshwa katika muktadha wa sentensi kuu. Kishazi kinachoweza kujisimamia kama sentensi huitwa kishazi huru kikiwa ndani ya sentensi kuu na huitwa “sentensi sahili” kikiwa sentensi inayojitegemea.
Kishazi kwa kawaida, hasa kishazi huru huwa na kitenzi kimoja kikuu. Kitenzi hicho huweza kuandamana na kitenzi kisaidizi. Pia, kitenzi katika kishazi huweza kuwa kitenzi kishirikishi.
Tofauti ya kishazi na sentensi ni kwamba kishazi hupatikana ndani ya sentensi lakini sentensi hujisimamia kimuundo na kimaana. Kishazi huwa na kiarifu kimoja na kiima kimoja, lakini sentensi huweza kuwa na kiima kimoja.
 Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa