Home » » RADI YAUA WANAFUNZI SITA, MWALIMU DARASANI.

RADI YAUA WANAFUNZI SITA, MWALIMU DARASANI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
.

wanafunzi wawili wa shule ya msingi kibirizi manispaa ya kigoma/ujiji, najimu rajabu (9) na khatibu (9), wakipewa huduma na muuguzi wa hospitali ya mkoa maweni baada ya kujeruhiwa na radi jana. picha/ joctan ngelly

Wanafunzi sita wa shule ya msingi, wamefariki dunia kwa kupigwa na radi na wengine 15 wamejeruhiwa miongoni mwao vibaya kufuatia mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali na radi kunyesha katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji jana.
Tukio hilo lilitokea jana saa 5:00 asubuhi katika Shule ya Msingi Kibirizi iliyopo kwenye manispaa hiyo.
 
KAULI YA MGANGA 
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni, Dk. Fadhili Kibaya, alisema alipokea maiti za watu wanane zikiwamo za wanafunzi sita wa Shule ya Msingi Kibirizi na moja ya mwalimu wao jana saa 6:00 mchana.
 
Alisema maiti nyingine ni ya mwanaume mkazi wa Bangwe katika manispaa hiyo. Alisema mbali ya maiti, pia alipokea majeruhi 15.
Dk. Kibaya aliyataja majina ya wanafunzi waliofariki dunia kuwa ni Yusuf Athumani (8), Hassani Ally (9), Fatuma Silei (7), Zamuda Seif (8), Warupe Kakupa (10) na Shukurani Yohana (7) ambao ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Kibirizi.
 
Alisema wengine waliofariki dunia katika tukio hilo la kusikitisha ni mwalimu wa shule hiyo, Elieza Mbwambo (25) na Focus Ntahaba (35), mkazi wa Bangwe katika manispaa hiyo. 
 
Dk. Kibaya alitaja wanafunzi waliojeruhiwa katika tukio hilo na ambao wamelazwa wodi namba nane hospitalini hapo kuwa ni Mahamoud Sijafiki (10), Najimu Rajabu (9) na Khatibu Amani (9).
 
Aidha, alisema wengine watano wako kwenye chumba cha uangalizi maalum (ICU) na wengine walitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani kwao.
 
MWALIMU ANENA
Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Msingi Kibirizi, Emmanuel Wilbert, alisema mwalimu aliyefariki dunia alitoka darasa la tatu na kuingia ofisi ya walimu na kukaa akiendelea na shughuli zake kama kawaida.
 
Wilbert alisema baada ya muda mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali na radi huku walimu wengine wakiwa madarasani wakiendelea na vipindi, ilipiga radi iliyosababisha kifo cha mwalimu na wanafunzi hao waliokuwa madarasani.
 
Alisema baada ya tukio hilo, wanafunzi na walimu walikimbia ovyo na mwalimu mwingine Merina Serilo, alipigwa na radi na kujeruhiwa. 
 
Hata hivyo, alisema hali yake inaendelea vizuri.
 
KAULI YA KAMANDA
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa masuala ya radi hayazungumziki.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa