Home » » WAKIMBIZI WANAVYOISHI ‘ROHO MKONONI’ KIGOMA

WAKIMBIZI WANAVYOISHI ‘ROHO MKONONI’ KIGOMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Nyarugusu. Licha ya taasisi za kimataifa, Serikali na wadau wengine wa maendeleo kutoa misaada, hali katika kambi za wakimbizi mkoani Kigoma ni mbaya kutokana na mlipuko wa magonjwa, uhaba wa chakula, malazi na mavazi.
Hali hiyo inasababishwa na idadi kubwa ya wakimbizi walio katika Kambi za Nyarugusu, Kagunga na Uwanja wa Lake Tanganyika.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kanali Mstaafu Issa Machibya anasema katika Kambi ya Kagunga, iliyo uwanda wa Pwani ya Ziwa Tanganyika kuna watoto 75,000, wanawake 6,000 na wanaume 7,000 ambao wanahitaji maji, chakula na malazi.
“Hali ni mbaya sana kuna idadi kubwa ya wakimbizi, wote wanahitaji kula, kulala na kutibiwa wanapougua,”  anasema Kanali Machibya.
Hata hivyo, takwimu halisi za idadi ya wakimbizi walio katika kambi hizo inatatanisha kwani Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi(UNHCR), linasema kuwa idadi ya wakimbizi katika kambi zote ni 49,388 kwa sasa, huku kukiwa na tetesi kuwa baadhi hawajulikani walipo.
Wakati huo huo, Ofisa Uhamiaji katika mpaka wa Kambi ya Kagunga, Albert Jeremiah anasema tangu Aprili 29, wakimbizi zaidi ya 90,585 wamesajiliwa kwenye kambi hiyo na baadhi wameelekea Nyarugusu.
Jeremiah anasema kwa siku moja, meli za MV Liemba na Mv Malagarasi hubeba wakimbizi 1800 na kuwapeleka Uwanja wa Lake Tanganyika.
Walazwa vitanda vya miti, 3993 waathirika kwa kipindupindu
Idadi kubwa ya wakimbizi, imesababisha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambapo takwimu kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dk Leonard Subi, zinaonyesha kuwa hadi sasa kuna jumla ya wagonjwa 3993. Kati ya wagonjwa hao, 25 ni Watanzania.
Saa 10:35 jioni wakati Mwananchi ilipoingia ndani ya Kambi ya Nyarugusu, ilikuta kuna wagonjwa wa kipindupindu na kuhara wakipewa chakula chao cha mchana, ambacho ni ugali na maharage huku ikielezwa kuwa huo ndiyo mlo wa mwisho kwa siku hiyo, baada ya kunywa uji asubuhi.
Ndani ya wodi hiyo kumefurika wagonjwa, wengine wakiwa wamelala chini na wachache walio mahututi wakiwa wamelazwa kwenye vitanda vya miti.
Mganga anayehudumia wagonjwa wa kipindupindu katika kambi hii kubwa ya Nyarugusu, Dk Lawrence Mhina anasema hadi sasa kambi hiyo ina wagonjwa 115 wanaotibiwa.
Hata hivyo, anasema kuwa tangu wakimbizi kutoka Burundi waanze kuingia nchini mapema mwezi uliopita, mpaka sasa hospitali hiyo imetibu wagonjwa zaidi ya 500 wa kuhara na kipindupindu.
“Takwimu hizi za wagonjwa zinapanda na kushuka, lakini mara nyingi tunapokea wagonjwa wengi usiku, wakati ambapo wakimbizi kutoka Kagunga na Uwanja wa Lake Tanganyika huletwa kwa mabasi,” anasema
Anabainisha kwamba changamoto kubwa katika kambi hiyo ni idadi kubwa ya wagonjwa, vyumba vichache vya kuwaweka, uhaba wa vitanda, mashuka na wahudumu wa afya.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani(WHO) nchini, Dk Rufaro Chatora anasema kuwa shirika lake litaongeza wahudumu wa afya na misaada ya dawa kwani huenda hali ikawa mbaya zaidi kwa sababu wakimbizi bado wanamiminika kutoka Kagunga.
“Lazima tuhakikishe tunazuia maambukizo mapya, tuangalie uwezekano wa kuepusha watu kuambukizwa wakati wanaposafirishwa kutoka kambi moja kwenda nyingine,”anasema
Dk Chatora anasema kuwa WHO itahakikisha dawa zinapatikana kwa wingi katika maeneo yote yaliyoathiriwa na kipindupindu na malaria.
“Huenda malaria nayo ikawa tatizo kubwa kwa sababu hawa watu wanalala nje na wanaumwa na mbu, “ anabainisha.
Hata hivyo, Dk Subi ameagiza dawa za malaria aina ya Alu, ili zipelekwa katika kambi hizo na kwamba kuna kiasi cha kutosha cha dawa kwa wakimbizi wote.
Wakati huo huo, kipindupindu katika Kambi ya Kagunga kimeathiri watu 1984, huku kukiwa na wagonjwa wapya 109 mpaka sasa.
Daktari wa Wizara ya Afya anayesimamia kambi hiyo, Cyst Mosha anasema kwamba ingawa wagonjwa wanapata tiba na kuhudumiwa, lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa chakula.
“Wagonjwa wanatibiwa, lakini hawana chakula cha maana cha kuwapa nguvu, matokeo yake wanajikuta wakila vidonge vya virutubisho kama chakula,” anasema.
Wagonjwa, hata wasio wagonjwa katika kambi hiyo hujikuta wakikosa chakula kwa zaidi ya wiki, hali inayowasababishia wengine kuzimia na kutundikiwa maji ya ‘glucose’ ili kuwapa nguvu.
Mwananchi lilishuhudia baadhi ya wakimbizi wakipika ugali wenye ‘rangi’ nyeusi mithili ya mkaa na walipoulizwa ni aina gani ya ugali walijibu; “ni mihogo iliyooza.”
Wagonjwa wa kipindupindu katika Kambi ya Uwanja wa Lake Tanganyika ni 1496, hata hivyo changamoto kubwa katika kambi hiyo ni maji na chakula.
Wajawazito, wazazi wanavyoteseka
Safari ya kutoka nchini Burundi hadi kambi kuu ya Nyarugusu si nyepesi. Ni ni ngumu na ya hatari zaidi kwa wajawazito.
Wajawazito hawa hutumia wiki nzima kufika katika kambi hii, ingawa baadhi hutumia siku nne hadi saba kutembea kutoka katika mikoa yao nchini Burundi hadi Kagunga.
Wafikapo Kagunga, hutakiwa kupelekwa katika Kambi ya Uwanja wa Lake Tanganyika iliyopo Kigoma mjini kabla ya kwenda kambi kuu ya Nyarugusu.
Familia za polisi na wanajeshi
Mwananchi limedokezwa kuwa wengi wa wakimbizi hao ni familia za wanajeshi na polisi, ambazo zimeamua kuwatanguliza nchini ili kuwaepusha na vita, baada ya kupata uhakika wa uwezekano wa kuibuka vita kubwa zaidi ya ile ya mwaka 1994.
Mratibu wa Tiba kutoka Shirika la Kimataifa la Uhamiaji(IOM), Dk Beda Mwita anasema kuwa kutokana na itifaki, uhaba wa wafanyakazi na vitendea kazi, wakimbizi hutumia siku tatu kutoka Uwanja wa Lake Tanganyika kwenda Nyarugusu.
Hali hiyo imesababisha baadhi kufariki wakiwa kwenye vyombo vya usafiri na wengine kupata maambukizo wakiwa kwenye mabasi au meli.
Wajawazito hupata wakati mgumu zaidi kwani hulazimika kusafiri kwa saa mbili hadi nne kwa meli kutoka Kagunga hadi Kigoma mjini.
Baada ya hapo, hutakiwa kwenda Nyarugusu kwa mabasi, safari ambayo huchukua saa nne hadi tano. Hata baada ya kufika Nyarugusu, huwachukua saa nyingine sita hadi saba kusajiliwa na kupata maturubai ya kujihifadhi (tent).
Mmoja wa wakimbizi waliojifungua ndani ya Kambi yaUwanja wa Lake Tanganyika, Neema Adera,25, anasema alisafiri kwa wiki mbili hadi kufika katika kambi hiyo kutokana na hali yake kuwa ya ujauzito, akiwa pia na watoto wengine wanne.
“Siku niliyofika, sikukaa sana, baada ya siku moja nikajifungua. Hata hivyo, namshukuru Mungu kwa kuwa nipo salama mimi na watoto wangu,” anasema.
Neema, ambaye sasa ana watoto watano, anasema kwamba mume wake ameamua kubaki Bujumbura(Burundi) ameamua kuitanguliza familia yake nchini kwa kuhofia kuibuka kwa vita.
Neema alieleza hayo akiwa amelala chini na kichanga chake, huku amezungukwa na watoto wake wanne, Neris, Deris, Tom, Ibara na Ndengaza.
Hata hivyo, ni heri ya wajawazito na waliojifungua na sasa wapo katika Kambi ya Uwanja wa Lake Tanganyika kwani wana uhakika wa kulala ingawa ni chini lakini kwenye ‘tent’, kuliko wajawazito wakimbizi walio Kagunga ambao wengi wanalala chini, bila tent na hawana uhakika wa kula.

Mwandishi wa Mwananchi anakutana na Cecil Jean-Pierre, binti wa miaka 17 aliyejfungua wiki moja iliyopita katika Kambi Kagunga, ambaye ingawa amejifungua salama, lakini anakabiliwa na changamoto ya mavazi, malazi na chakula.
Akiwa amelala chini ya mti bila chochote cha kutandika zaidi ya nguo alizovaa pamoja na wanawae wengine wanne wenye vichanga, Cecil Jean-Pierre, anamwogesha mtoto wake na baada ya kumaliza anamfunga kwa ‘nepi’ ambayo ni kitambaa cha leso.
Mavazi pekee aliyonayo ni khanga mbili, moja amejifunga mwenyewe na nyingine anaitumia kumfunika kichanga wake, mwenye wiki mbili.
“Nimeenda kuomba wanipe maji ya vitamini kwa ajili ya wagonjwa wa kuhara ili nipate maziwa kwani maziwa hayatoki kwa sababu sijala na mtoto analia sana,” anasema.
Kambi ya Nyarugusu yafurika
Takwimu kutoka UNHCR zinaonyesha kuwa Kambi ya Nyarugusu kwa sasa imezidiwa na idadi kubwa ya wakimbizi, wanaokaribia 100,000
Mratibu wa Tiba wa UNHCR, Kambi ya Nyarugusu, Dk Demis Lega anasema kuwa idadi ya wakimbizi ni kubwa na inawapa changamoto katika kuwahudumia.
Idadi hii inaifanya UNHCR kuanzisha kambi mpya katika eneo hilo hilo iliyopewa jina la Nyarugusu B, ili kuhifadhi wakimbizi wapya wanaoendelea kumiminika kutoka Kagunga na Uwanja wa Lake Tanganyika wakitokea nchini Burundi.
Dk Mhina anasema kwamba kwa siku wakimbizi 10 hadi 20 huweza kujifungua katika hospitali iliyopo kwenye Kambi ya Nyarugusu na kati ya hao,wapo wanaohitaji upasuaji na wanaohitaji kuongezwa damu.
Kwa mujibu wa takwimu za hopitali hiyo, kwa idadi ya wakimbizi iliyopo, watoto kati ya 200 hadi 250 wanaweza kuzaliwa kila mwezi.
Mashirika ya kimataifa yamiminika
Tangu Aprili 29, baada tu ya wakimbizi kuanza kuingia kwa wingi nchini wakipitia mipaka ya Manyovu, Kagunga, Gungu, Kibiriza na Kihalu, mashirika ya kimataifa nayo yameendelea kumiminika katika kambi hizo yakitoa misaada mbalimbali.
Miongoni mwa mashirika hayo ni WHO ambalo limeshirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini kuleta wahudumu wa afya, usambazaji wa dawa na vifaa tiba.
Shirika la Kimataifa la Plan Tanzania, limetoa Sh 27 milioni kwa wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu ambao wanawahudumia wakimbizi hao.
Nalo shirika la Plan Tanzania limetoa Sh19.4 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya usafi katika makambi hayo.
Kwa upande mwingine UNHCR, wana wajibu mkubwa wa kuwasafirisha wakimbizi kutoka Kagunga hadi Uwanja wa Lake Tanganyika, kisha Nyarugusu na kuwasafirisha wanaopitia mpaka wa Manyovu kwenda Nyarugusu.
Madaktari Wasio na Mipaka(MSF) tayari wamefika Kigoma na wameanza kazi kwa kuwapa tiba baadhi ya wakimbizi wenye magonjwa.
Mashirika mengine yaliyowasili katika kambi hizi ni Shirika la Chakula Duniani(WFP), Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji(IRC), Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM)na Shirika la Watoto(UNICEF).
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa