Home » » JAJI BOMANI AMWAGIA SIFA KUBENEA

JAJI BOMANI AMWAGIA SIFA KUBENEA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Jaji Mark Bomani (kulia) akimpa tuzo Mkurugenzi wa Hali Halisi Publishers, Saed Kubenea
Jaji Mark Bomani (kulia) akimpa tuzo Mkurugenzi wa Hali Halisi Publishers, Saed Kubenea 
 
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Dream Success Enterprises, waasisi wa Tuzo ya Shujaa Kati Yetu, wamewatunuku tuzo Saed Kubenea, David Kafulila na Vick Mtetema kwa mchango wa kazi zao zilizotukuka katika maendeleo na ujenzi wa taifa.
Kubenea, mwandishi wa habari za uchunguzi, mmiliki wa mtandao wa MwanaHALISI Online na gazeti la MwanaHALISI lililosimamishwa na serikali kwa muda usiojulikana ametunukiwa tuzo ya “Uwazi na Ukweli.” 
Naye Kafulila, mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR – Mageuzi), ametunukiwa tuzo ya “Maono Mapevu,” huku Mtetema, akitunukiwa tuzo ya “ubunifu.”
Mtetema ni murugenzi mtendaji wa shirika la Under The Same Sun, linalofanya kazi za utetezi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Kafulila ametunukiwa tuzo hiyo kutokana na kuibua na kusimamia ufisadi wa zaidi ya Sh. 300 Bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow, ndani ya Bunge la Jamhuri.
Tuzo hizo zinalenga katika kuleta mapinduzi ya kimaadili na kifikra nchini.
Akizungumza wakati akikabidhi tuzo hizo jijini Dar es Salaam, mwasheria mkuu wa kwanza nchini, Jaji Mark Bomani, alisema ni heshima kubwa kwake kutoa tuzo kwa Kubenea, Kafulila na Mtetema, kutokana na machango wao mkubwa kwa taifa.
“Ni watu makini. Wanafanya kazi nzuri kwa taifa lao. Kubenea amefanya kazi nzuri. Gazeti lake ni moja ya magazeti yanayoandika na kusema ukweli bila kuogopa, kujipendekeza, kutoonea wala kupendelea. Hicho ndicho kinachohitajika,” amesema Jaji Bomani.
“Kafulila ni mbunge kijana, lakini ametoa mchango mkubwa katika kutetea rasilimali za taifa kwa kufichua maovu yanayoendelea serikalini. Kazi ambayo inahitaji uelewa, umakini, ujasiri na kusema kweli,” ameeleza.
Naye Mtetema, Jaji Bomani amesema, amejitolea kutetea na kuzungumzia kwa undani suala la mauji ya Albino, hali inayotia moyo mapambano hayo.
Amesema, “Wote ambao wamejitahidi kufikisha ujumbe kwa wananchi, lazima wapongezwe na kupewa tuzo kwa jitihada zao. Juhudi kubwa ifanyike kuwasaka wengine mabao wamejitahidi kufichua maouvu ili nchi iwe ya amani.
“Tumezoea kuona watu wakitunukiwa Tunu za taifa kila mwaka katika sherehe za Muungano au Uhuru. Hiyo haitoshi. Hizo ni kazi za serikali. Lazima na watu nao wawe na vyombo vyao ambavyo vinawatambua watu ambao wasingetambukika huko serikalini,” amesema.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo,  Kubenea amesema, “…nikiri kwamba nilishutuka sana nilipopata taarifa ya kutunukiwa tuzo hii.”
Alisema, “tuzo hii, ni faraja kwangu. Sijutii kuwa mkweli. Gazeti langu la MwanaHALISI limefungiwa na serikali. Jingine linaweza kufungiwa kesho. Karamu yangu inaweza kuvunjwa. Mdomo wangu unaweza kuzibwa, lakini sitanyamaza.”
Ameifananisha jina la tuzo hiyo la “Uwazi na Ukweli” na kauli ya serikali ya awamu ya tatu ambayo amesema, “…baadae iligeuka na kuficha ukweli na kukumbatia usiri.”
“Nyumba zote za serikali zimeuzwa katika kipindi ambacho serikali hii, ilikuwa madarakani. Mgodi wa Kiwila, nyumba za serikali kwa wasiostahaili na kwa bei ya kutupwa, mashamba ya mkonge, ufisadi katika Benki Kuu ya Tanzania na Benki (NBC).
Kwa upande wake Kafulila amesema, “…nimejisikia fahari kubwa kuwa miongoni mwa watu ambao wamechangia chochote katika taifa letu, hata kupewa tuzo hii. Nikifa kesho duniani wanangu, wajukuu, ndugu zangu na watu wengine watanikumbuka kwamba nilifanya chochote.”
Naye Kafulila amesema, “taifa letu lina tatizo kubwa la watu kukosa uadilifu na kujaa uoga. Hii inatokana na ukosefu wa bidii na maarifa….nachoweza kuwaahidi watu, nitaendelea kuwatumikia. Nakwenda kugombea tena. Nikishidwa, nikishinda sitoacha kutumikia nchi yangu.”
Kwa upande wake, Vicky Mtetema amesema, “….ni heshima kubwa kutunukiwa hii tuzo. Vitendo vya albino kuuwawa vinakithiri wakati huu wa uchaguzi. Naomba nimteue David Kafulila awe baba na kuwasemea watu wenye albinism bungeni,”
Mtetema amemtaka Kafulila kama atafanikiwa kuchaguliwa katika Bunge la 11 kuhakikisha kunakuwepo na sera ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), Sheria ya kuwaondoa wanganga wanaopiga ramli na mazingira mazuri kwa Albino.
Joshua Lawrence, afisa mikakati toka Dream Success Enterprises amesema maendeleo ya taifa lolote duniani hutengenezwa na raia na viongozi wenye habari, maarifa na maono sahihi. Na ili kufanikisha hayo, uhuru wa kupata habari ndani ya muktadha ni muhimu kuwepo.
“Na, hili linawezekana tu pale raia wanaopewa uhuru wa kuogelea ndani ya bahari ya fikra huru, huku muktadha wa sheria zinazolinda kingo za uhuru huo ukiwa ni kuzinawilisha fikra pevu na kuzinyong’onyeza fikra bwete, wala si vinginevyo,” amesema Lawrence.
Amesema hiyo ni awamu ya pili tuzo hizo kutolewa. Awamu ya kwanza ilikuwa 22 Disemba, mwaka 2014 ambapo Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh alitunukiwa.
Chanzo:Mwanahalisi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa