Home » » Askofu Mkuu wa Tabora Kuongoza ujumbe wa Tanzania kumuona Papa Francis Uganda.‏

Askofu Mkuu wa Tabora Kuongoza ujumbe wa Tanzania kumuona Papa Francis Uganda.‏

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Na Joseph Ishengoma, MAELEZO
26/11/2015
Askofu Mkuu wa jimbo kuu la Tabora Mhashamu Paulo Ruzoka kesho (tarehe 27.11.2015) anatarajia kuongoza ujumbe wa Tanzania kwenye ziara ya Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Baba Mtakatifu Francis nchini Uganda.

Baba Mtakatifu Francis anatarajia kuwasili nchini Uganda kesho kwa ziara ya siku mbili akitokea Kenya kabla ya kuelekea Afrika ya Kati.

Hii ni ziara ya kwanza kwa kiongozi huyo Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani kutembelea Bara la Afrika tangu alipoliongoza Kanisa Katoliki mwaka 2013.

Katibu wa Baraza la Maaskofu (TEC) nchini Padre Raymond Saba amesema  Mabaraza ya Maaskofu ya Kenya na Uganda kwa pamoja yalitoa mwaliko kwa TEC kushiriki katika ziara ya Baba Mtakatifu katika nchi hizo.

“Tulipata mwaliko kutoka Kenya na Uganda, lakini tumeangalia nafasi yetu na jinsi ya kushiriki katika ziara hii. Hatukuweza kutuma mwakilishi Kenya, lakini Askofu Ruzoka ataiwakilisha TEC Uganda,” amesema.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, jana mabasi mawili ya waumini wa dini ya Kikristo yaliondoka mjini Mwanza kuelekea Namugongo, Uganda ambapo Baba Mtakatifu atakapofanyia ibada.

Eneo la Namugongo ndipo Mfalme Kabaka Mwanga II alipowachoma na kuwaua mashahidi 22 wa Uganda waliofia dini katika karne ya 18.

“Natoa wito kwa waumini wa Kanisa Katoliki nchini, wafuatilie na kusikiliza kwa makini ujumbe wa Baba Mtakatifu aliouleta katika Barani Afrika kwa sababu unagusa moja kwa moja amani na ushirikiano miongoni mwa jamii,” amesema.

Kwa mujibu wa Padre Saba, Baba Mtakatifu hufanya ziara kufuatia mwaliko wa kanisa na serikali ya mahali husika au tukio la kimataifa linalohusiana na imani Katoliki.

Amesema, “Kanisa pekee yake haliwezi kufanikisha ziara ya Baba Mtakatifu. Ndio maana alipofika Kenya alipokelewa na Rais Uhuru Kenyatta na hata alipokuwa Marekani alipokelewa na Rais Baraka Obama ingawa sio rahisi kwa kiongozi wa Marekani kumpokea mgeni uwanja wa ndege.” 

Ziara ya Baba mtakatifu nchini Marekani ilipangwa kabla hajawa kiongozi Mkuu wa kanisa Katoliki. Ziara hiyo ilitokana na kongamano la kimataifa la familia lililofanyika mjini Filadelphia.

Papa Francis anatarajia kuhudhulia kongamano la vijana ulimwenguni nchini Poland mwaka 2016.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa