Home » » MIKATABA UNUNUZI VICHWA, MABEHEWA YA TRENI KUPITIWA UPYA.

MIKATABA UNUNUZI VICHWA, MABEHEWA YA TRENI KUPITIWA UPYA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa
Serikali imeliagiza Shirika la Reli Tanzania (TRL) kupitia upya mikataba ya ununuzi wa vichwa vya treni na mabehewa ili kubaini kasoro zilizojitokeza na kuchukua hatua stahiki kabla ya maboresho ya reli ya Tanga-Moshi-Arusha. 
 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki mkoani Kigoma, wakati akikagua miundombinu ya reli na kusisitiza nia ya serikali kufufua reli ya Kanda ya Kaskazini ili kuimarisha huduma za uchukuzi katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha. 
 
“Kama serikali tumewekeza vya kutosha katika TRL, hivyo tunawataka mfanye biashara itakayolipa nasi tutahakikisha popote reli ilipo inatoa huduma iliyokusudiwa na kuchangia kukuza uchumi wa nchi," alisema. 
 
Aidha, Prof. Mbarawa aliwataka wafanyakazi wa TRL kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kupata bidhaa na abiria wengi wa kuwasafirisha nchini kote. 
 
Alisema serikali imedhamiria kuiongezea nguvu TRL na kwamba baadhi ya mitambo kutoka Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) itakabidhiwa kwa shirika hilo, hivyo kulitaka kuwa na mpango madhubuti wa kufanya biashara na kurudisha hadhi ya usafiri wa reli hapa nchini. 
 
“Fanyeni bidii ili mpate mizigo ya kusafirisha kutoka Tanga kwenda Moshi na Arusha ili kufikia lengo la kubeba mizigo tani milioni moja kwa mwaka,”  alihimiza.  Prof. Mbarawa pia alizungumzia umuhimu wa TRL kufanyakazi kwa karibu na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), ili kuongeza kasi ya huduma za uchukuzi nchini, kuongeza fursa za ajira na kukuza pato la shirika na taifa. 
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRL, Masanja Kadogosa, alisema shirika hilo limejipanga kutafuta masoko ndani na nje ya nchi ili kuboresha huduma za uchukuzi na kukuza pato lake. 
 
Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa alikagua Meli ya MV Liemba na kuitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), kuhakikisha meli za MV Liemba na MV Mwongozo zinakaguliwa na kufanya kazi inavyostahili katika Ziwa la Tanganyika. 
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa