Home » » ARDHI OEVU MALAGARASI HATARINI KUTOWEKA

ARDHI OEVU MALAGARASI HATARINI KUTOWEKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


ENEO la ardhi oevu la Malagarasi liko hatarini kutoweka kutokana na ongezeko kubwa la matumizi ya ardhi na maji linalosababisha uharibifu wa mazingira.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa maji katika bonde hilo uliofanyika mjini Kigoma hivi karibuni Meneja wa Bonde la Maji la Ziwa Tanganyika, Chobariko Rubwabwa, mpango mkakati unahitajika kwa haraka ili kunusuru eneo hilo.
Rubwabwa alisema kuwa utafiti unaonesha kuwa kwa sasa eneo hilo la ardhi oevu ya Malagarasi limeelemewa na matumizi makubwa ya watu na uharibifu wa mazingira.
Alisema ifikapo mwaka 2020, hali itakuwa mbaya zaidi kama hatua hazitachukuliwa sasa.
Rubwabwa alisema ongezeko kubwa la watu kuzunguka eneo hilo, ongezeko la matumizi ya shughuli za binadamu ikiwamo kilimo na ufugaji na uharibifu mkubwa wa mazingira ni miongoni mwa athari zinazotishiwa kutoweka kwa eneo hilo.
Alisema kuwa kwa sasa eneo la ardhi oevu ya Malagarasi linakabiliwa na msongo wa maji kutokana na matumizi ya maji hayo kutotosheleza mahitaji huku matumizi yakiwa makubwa sambamba na uanzishwaji wa miradi mikubwa ya kilimo.
Alisema taarifa za utafiti na ushauri wa kitaaluma unaotolewa haufanyiwi kazi vya kutosha na Halmashauri husika.
Akizungumzia hali hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Emmanuel Kalebero, alisema kuanzia sasa ni lazima ofisi za mabonde ya maji nchini yaridhie na kutoa kibali kwa matumizi yoyote ya maji na maeneo yanayotaka kufanyika kwenye maeneo ya mabonde nchi.
Kalebero alisema ongezeko kubwa la watu na ongezeko kubwa la matumizi ya mabonde ni lazima yafanyiwe tathmini na ofisi za mabonde kuona mipango ya matumizi endelevu ya miradi inayotaka kufanyika sambamba na utunzaji wa mazingira ya maeneo hayo.
Alisema kuwa mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameyakumba maeneo ya mabonde nchini yanatokana na matumizi holela ya maeneo hayo na uharibifu mkubwa wa mazingira yamefanya kupungua kwa kiwango cha maji katika mabonde mbalimbali nchini.

Chanzo Gazeti la Habari leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa