Home » » Mvua yaua watoto sita

Mvua yaua watoto sita



WATOTO sita wakazi wa kijiji cha Mubanga wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, wamekufa baada ya kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha vijiji jirani na kijiji hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Marko Gaguti akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, alisema mauaji hayo yalitokea juzi Jumapili mchana.
Kanali Gaguti alisema watoto hao ambao walikuwa wanane, walikuwa wakitoka kanisani na wengine wakichunga mifugo ya wazazi wao.
Walikumbwa na mauti hayo baada ya kukumbwa na maji ya mvua iliyokuwa ikinyesha vijiji vingine.
Wakiwa kando ya mto, walikumbwa na dhoruba ya maji ambayo yalikuwa yakitokea maeneo ya mlimani na yaliwatumbukiza kwenye korongo ambako watoto wawili walijiokoa kwa kushika majani kando ya mto huo.
Aliwataja waliokufa katika ajali hiyo ya maji kuwa ni Joseph Daniel (10), Meris John (10), Wence Tryphone (11), Sedekia Philemon (9) huku akiwataja watoto wengine wawili ambao miili yao haijapatikana kuwa ni Kaleb Nashon (14) na Habil Gordwin (8).
Mkuu wa Wilaya alisema hadi jana mchana, ambako maziko ya watoto wanne yalikuwa yakifanyika miili ya watoto wanne ilipatikana na kuzikwa kwa jitihada za vikosi vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wananchi.

CHANZO GAZETI LAHABARI LEO
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa