MAHAKAMA ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora imemhukumu kutumikia
adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Sh 200,000
aliyekuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Igogo, Kata ya Nanga,
Elinkaila Isaya baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya
madaraka.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Igunga, Ajali Millanzi
alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka umemuona aliyekuwa
mwenyekiti wa serikali ya kijiji ana hatia hivyo atalipa faini Sh
200,000 au akishindwa kulipa atakwenda jela miaka miwili. Hata hivyo,
mshtakiwa alilipa na kuachiwa huru na mahakama huku washtakiwa watatu
wakiachiwa huru.
Awali, ilidaiwa mahakamani na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Nzega, Aidani Samali
mbele ya Hakimu Millanzi, kwamba Oktoba 13, 2014 akiwa Mwenyekiti wa
Serikali ya Kijiji cha Igogo pamoja na viongozi wengine wa Serikali ya
Kijiji akiwemo Mtendaji wa kijiji hicho, Henry Masanja na wajumbe wawili
wa Kamati ya Fedha, Boniphace Jagadi na Helena Maduhu walitumia vibaya
madaraka yao.
Kwamba walishindwa kujenga matundu ya vyoo 12 katika shule ya msingi
Igogo na kujipatia fedha Sh milioni 5.1 kwa manufaa yasiyostahili.
Mwendesha Mashitaka huyo wa Takukuru aliendelea kuiambia Mahakama
kuwa shitaka la pili Novemba 24, 2014 mshitakiwa na wenzake walishindwa
kujenga choo cha ofisi ya mtendaji wa kijiji hicho na kujipatia fedha Sh
milioni 3.1 kwa manufaa yasiyostahili.
Aidha, shitaka la tatu ufujaji na ubadhirifu wa fedha za umma kati ya
Oktoba 13 na Novemba 24, 2014 jumla ya fedha Sh milioni 8.2 walizitumia
kwa maslahi yao binafsi. Mwendesha Mashitaka alibainisha shitaka la nne
kuisababishia serikali hasara katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga.
Alidai washtakiwa walitenda kosa hilo kinyume cha kifungu 31 cha
Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007 inayozuia
kutenda makosa kama hayo.
Baada ya kusomewa mashitaka, washtakiwa walikana shitaka ambapo
upande wa mashitaka ulipeleka mashahidi 10 ambapo wote walitoa ushahidi
mahakamani dhidi ya washtakiwa.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment