MWALIM MKUU KAKONKO AJINYONGA AKIWA OFISINI KWAKE,AANDIKA UJUMBE UNAOMUHUSU MKURUGENZI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU wa Shule ya Sekondari Kakonko wilayani Kakonko mkoani Kigoma,Peter Rubonya amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kamba ofisini kwake mapema leo asubuhi.

Akielezea tukio hilo,Mwalim wa zamu wa shule hiyo Isaac Japhet amesema yeye alifika shuleni hapo saa 12:30 asubuhi ili kuwafundisha wanafunzi wa kidato cha nne masomo ya ziada baada ya kufunga shule wiki iliyopita na baada ya kufika aligundua kuwa hana chaki ambapo mkuu huyo wa shule alimpatia chaki mlinzi ili awape wananfunzi.

Amesema baada ya muda,Mratibu elimu kata pamoja na mmoja wa wazazi walifika ofisini hapo wakiwa na shida na mkuu wa shule na baada ya kuelezwa yupo ndani ofisini lakini baada ya kugonga mlango hawakuweza kujibiwa na ndipo wakaamua kufungua mlango na kukuta mwili wa marehemu ukining’inia dalini.

Mwalim Isaac amesema Mwalimu aliyejinyonga alikuwa akifundisha masomo ya Kemia na Fizikia shuleni hapo hawakuwahi kusikia mgogoro wowote wa kifamilia au kijamii, na mkewe ambaye ni mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM),alifika nyumbani kwake juzi akitokea Dodoma.

Kwa upande wa Mlinzi wa Shule hiyo Kajolo Kajabojabo amesema alikutana na Mkuu wa shule mapema asubuhi akiingia ofisini na kumuomba chaki ambazo alipewa na kuziwasilisha kwa walimu.

"Nilimuona kabisa tukasalimiana, nikamuuliza kama anaweza kuwa na chaki, akaingia ofisini akanipatia boksi moja la chaki.Nikachukua na kisha nikampelekea mwalim aliyehizihitaji, alikuwa kwenye hali nzuri tu, lakini baada ya muda ndo tukio hilo likatokea,"amesema Kajoro.

Akizungumza baada ya kufika shuleni hapo Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala amesema Polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kujua sababu ikiwa marehemu aliacha ujumbe wowote au laa.

"Hatujajua sababu lakini ni muhimu jamii ikajenga utamaduni wa kueleza matatizo ya ndani yanayoyasibu.Hiyo inasaidia kupunguza msongo wa mawazo na kuepusha madhara kama haya,"amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Martin Otieno amesema baada ya kupekuliwa kwa mwili wa marehemu walikuta karatasi imeandikwa ujumbe kuwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Kakonko Lusubiro Mwakabibi asipodhibitiwa ataua wengi.
Chanzo: Kijukuu

WATU SABA WAFARIKI AJALI YA LORI KIGOMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Na Rhoda Ezekiel- Malunde1 blog
Watu saba wamefariki dunia katika ajali ya gari aina ya Scania katika  Mlima wa Kasagamba kijiji cha Mkongoro barabara ya kutoka Manyovu wilaya ya Kigoma Vijijini kuelekea mkoani Kigoma.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma Maltini Otieno amesema ajali hiyo imetokea leo Machi 21, 2018 majira ya saa tatu asubuhi. 

Amesema gari aina ya Scania lori yenye namba T741 AAB  ilianguka na kusababisha vifo vya watu saba akiwemo dereva wa gari hiyo aliyefahamika kwa jina la Siri Hamis (43) mwenyeji wa Singida pamoja na utingo wake aliyefahamika kwa jina la Ramadhani Saidi (23) mkazi wa Manyoni.
Kamanda Otieno amesema katika gari hiyo walikuwa wamebeba mizigo na watu wanne mmoja mwanamke na wa tatu wanaume ambapo wote walifariki na majina yao hayakufahamika.

Aidha amesema ajali hiyo pia imesababisha kifo cha mwanafunzi aliyefahamika kwa jina la Eliakimu Samsoni (15 )aliyekuwa akitembea kwa miguu kuelekea shuleni na gari hilo kumgonga akiwa anatembea.


Amesema chanzo cha ajari hiyo ni dereva kushindwa kuimudu gari kwenye mteremko mkali na kusababisha gari hiyo kutelemka kwa mwendo mkali na kumshinda dereva huyo na kusababisha vifo hivyo.

Kamanda Otieno amewaomba madereva kuzingatia sheria za barabarani na kuhakikisha gari za mizigo hazibebi abiria ili kunusuru vifo vitokanavyo na ajali na kuhakikisha wanazingatia alama za barabarani.
Mabaki ya lori baada ya ajali ULEGA AIPONGEZA HALMASHAURI YA WILAYA YA UVINZA KWA MKAKATI MZURI WA KUINUA SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 Chaga za kisasa za kukaushia dagaa katika mwalo wa Muyobozi, uliyopo katika kijiji cha Mwakizega Wilayani Uvinza, Mwalo ambao ulijengwa na Mradi wa kuhifadhi mazingira ya ziwa Victoria LIVEMP , chaga hizo zinatumika na wavuvi kukaushia dagaa.
 Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega na Ujumbe wake wakitoka kukagua gati katika mwalwo wa Muyobozi uliyopo Wilayani uvinza katika kijiji cha Mwakizega ambapo Naibu Waziri Ulega alifanya ziara leo.
Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Uvinza Bw. Haroon Chande akimueleza Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega Anayeangalia Chaga kuhusu chaga hizo za kuanikia dagaa zilizojengwa na mradi wa kuhifadhi mazingira wa ziwa Victoria LIVEMP chaga ambazo ameeleza zimekuwa na msaada mkubwa kwa wavuvi wa dagaa wanaotumia mwalo wa Muyobozi uliyobo Wilayani uvinza katika kijiji cha Mwakizega.
 Katika Picha katikati Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega akipata maelezo kuhusu Mwalo wa Muyowozi toka kwa Afisa Uvuvi wa Wilaya ya uvinza Bw. Haroon Chande, wakati wa ziara yake mwaloni hapo leo.
 Wavuvi wakiteketeza wao wenyewe nyavu haramu zilizokamatwa katika oparesheni ya kupambana na uvuvi haramu katika ziwa Tanganyika Mbele ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega alipofanya ziara katika Mwalo wa Muyobozi Wilayani Uvinza leo
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega kushoto akizungumza na mfanyabiashara wa samaki aliyejulikana kwa jina la Bw. Ntakokola Issa katika Mwalo wa Kibirizi Mjini Kigoma kuhusu usafi wa vifaa maalum na gari la kubebea samaki, gari no T389 AZY linalotumiwa na Mfanyabiashara huyo lilipokuwa linaonekana  katika hali ya uchafu, Naibu Waziri Ulega alikagua Mwalo wa Kibirizi uliyopo Mjini Kigoma leo baada ya kumaliza Ziara yake wilayani Uvinza.
 


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Uvinza kwa kuwa na mikakati thabiti ya kupambana na uvuvi haramu na kutatua kwa kiasi kikubwa migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kuwekeza kwenye Ranchi za mifugo.
Ulega ameyasema hayo alipokuwa katika ziara ya kugagua Mwalo wa Muyobosi uliyopo Wilayani uvinza ambapo alisema jitihada hizo za wilaya zitachangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza mapato ya Halmashauri hiyo na serikali kwa ujumla, kwani ina mkakati wa kutenga maeneo ya Ranchi kwa ajili ya wafugaji.
“Nataka niwahakikishie mimi na wizara yangu tutakuwa tayari kuhamia hapa kulisimamia jambo hili mtakapo tenga hayo maeneo ya kufugia, ili kuwaweka tayari wafugaji katika maeneo hayo na huo ndiyo muharobaini wa kwenda kuondoa  matatizo ya wakulima na wafugaji katika nchi yetu kwa mipango ya namna hii inawezekana kabisa, hicho ni kipaumbele chetu mimi na waziri wangu Mhe. Luhaga Mpina katika uongozi wetu tutahakikisha kama siyo kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji basi tutaindoa kabisa, kwa kushirikiana vyema na Halmashauri zetu” Alisema Ulega.
Ulega alisisitiza suala la mapambano dhidi ya uvuvi haramu na ulinzi wa Rasilimali za uvuvi na suala zima la ufugaji wa samaki, nakuwaasa kuachana kabisa na utamaduni wa kuagiza samaki kutoka nje ya nchi.
Naibu Waziri Ulega  alisema kuwa fedha nyingi zimewekwa katika mwalo huo wa Muyobozi na kuwataka wavuvi katika eneo hilo kuutumia vizuri mwalo huo wenye hadhi ya kimataifa ambapo ameleza kwa mwaka wa fedha uliopita mwalo huo peke yake umechangia kiashi cha shilingi milioni 28 “ Ninaamini kama mtapasimamia vyema mahala hapa patachangia pato la taifa mara nne zaidi ya mwaka jana. Ninyi ndo muwe walinzi wa kwanza wa rasilimali hizi ili nchi yetu iweze kuinuka” Alisisitiza
Awali, akiongea katika ziara hiyo mwenyekiti wa kijji cha Mwakizega ambapo mwalo wa Muhyobozi umejengwa Bw. Jaffari Abdalah, alisema mwalo huo unakabiliana na changamoto mbalimbali ikiwa nipamoja na gati la mwalo huo kuwa na urefu wa mia 20 ambazo ni chache kwa boti kuegesha kupakua na kupakia kabla na baadha ya shuguli za uvuvi , hivyo ameiomba serikali kuongeza urefu wa gati hiyo ili mitumbwi mikubwa na midogo iweze kufanya shughuli za uvuvi vizuri.
Bw. Jaffar pia alisema wavuvi wa Muyobozi wanakabiliana na changamoto ya kukosa elimu kupitia mafunzo yanayoendana na wakati huu wa kisasa katika sekta ys uvuvi.
 

WATENDAJI WA SERIKALI,WANANCHI WAHIMIZWA KUSHIRIKIANA KULETA MAENDELEO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


 MKUU wa Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, Kanali Marco Gaguti akizungumza na Baadhi ya Watendaji wa Serikali na wananchi kushirikiana katika shughuli za maendeleo katika ukusanyaji wa mapato na kufanya kazi.
Na Rhoda Ezekiel Kigoma,

MKUU wa Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, Kanali Marco Gaguti amewataka watendaji wa Serikali na wananchi kushirikiana katika shughuli za maendeleo katika ukusanyaji wa mapato na kufanya kazi.
Lengo ni kuboresha huduma za kijamii katika Wilaya hiyo na kuinua uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.Mwito huo aliutoa juzi katika chakula cha pamoja na wazee wa Wilaya ya Buhigwe ,Watumishi wa serikali, viongozi wa dini na chama pamoja na kuhamasisha shughuli za maendeleo.
Ambapo aliwataka kila mwananchi mmoja mmoja, kwa makundi na kwa ujumla wao kuweka mikakati ya pamoja ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya elimu, afya, miundombinu na jinsi ya kupatikana haki za wazee.
Mkuu huyo aliwataka watendaji wa Halmashauri kwa kushirikiana na wananchi wote ndani ya Wilaya kusaidia jitihada za kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato."Lengo ni kuwezesha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa mafanikio makubwa ambapo mapato hayo yatasaidia vijiji ambavyo havina zahanati vipate huduma hiyo kutokana na mapato hayo," amesema.
Aidha Gaguti aliwataka watendaji wa Serikali kuhakikisha wazee wa Wilaya hiyo wanapata haki zao kama wengine ikiwa ni pamoja na kupatiwa matibabu bure, kwakuwa ni sera ya Taifa mzee asisumbuliwe na apatiwe huduma zote bila malipo.“Nawashukuru wazee, viongozi wa vya siasa, viongozi wa madhehebu ya dini na watumishi wote kwa kuonesha moyo wa kusimamia maendeleo yetu na kuhakikisha tunapata maendeleo kwa kasi."Ni imani yangu kuwa tutashilikiana kwa mambo mengi ili kuweza kuinua uchumi wetu", amesema Gaguti.
Katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilya ya Buhigwe Anosta Nyamoga alieleza Halmashauri ya Buhigwe inatoa huduma za afya kwa wazee katika vituo vyake vya kutolea huduma za afya bure kulingana na sera na miongozo ya Serikali.
Aidha wazee wanapewa kipaumbele katika matibabu kwa kutibiwa kwanza. Pia wazee 14,993 wametambuliwa katika wilaya yetu na wazee 1000 watapigwa picha na kupewa vitambulisho vya matibabu katika kata 5.Upigaji wa picha na utoaji wa vitambulisho utaendelea katika kata 15 ambazo bado hazijafikiwa halmashauri imeendelea kuhamasisha jamii ili kuona umuhimu wa kujiunga na mfuko wa afya wa jamii (CHF). 
Nao baadhi ya wazee wa wilayani Buhigwe, Loleye Ndalibhonye alimpongeza Mkuu wa Wilaya kwa kuwakumbuka na kuwasaidia katika huduma za kijamii na kuwasaidia katika kuwapatia huduma ya afya bure.
Amesema endapo wilaya hiyo ikiongeza vituo vya afya itasaidia wazee hao kupata huduma kwa urahisi na Wananchi kuweza kupata huduma hiyo na kupunguza vifo vitokanavyo na ukosefu wa huda.
 

KATIBU MKUU WA MIFUGO KUKABIDHI RASMI TAARIFA YA CHAPA YA MIFUGO LEO KWA WAZIRI MPINA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo nchini, Dkt Maria Mashingo (mwenye skafu) akiongea na wafugaji kuhusu upigaji chapa mifugo kwenye Kijiji cha Makere Mkoani Kigoma.Kipindi cha kupiga chapa kitaifa knaiisha rasmi leo Januari 31. (Picha na Ngailo Ndatta) 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo nchini, Dkt Maria Mashingo akishiriki zoezi la Upigaji chapa mifugo katika siku ya mwisho ya zoezi hilo leo huko Kigoma. Kipindi cha kupiga chapa kitaifa knaiisha rasmi leo Januari 31. (Picha na Ngailo Ndatta
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo nchini, Dkt Maria Mashingo(mwenye skafu) akiongea na baadhi ya wafugaji kuhamasisha upigaji chapa mifugo katika siku ya mwisho ya zoezi hilo leo huko Kigoma. Kipindi cha kupiga chapa kitaifa knaiisha rasmi leo Januari 31. (Picha na Ngailo Ndatta) 
Dereva wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bwana Athuman Ramadhani akishiriki katika zoezi la upigaji chapa katika Mkoa wa Kigoma. Kipindi cha kupiga chapa kitaifa knaiisha rasmi leo Januari 31. (Picha na Ngailo Ndatta) 

Na John Mapepele, Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo nchini, Dkt Maria Mashingo amewataka Wakuu Wote wa Idara katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha kwamba timu zote zilizosambaa kote nchini ziwe zimewasili mjini Dodoma leo na kwamba ifikapo saa kumi na mbili jioni ziwe zimewasilisha taarifa kuhusu zoezi hilo kwake ili akabidhi rasmi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh.Luhaga Mpina kwa ajili ya hatua zaidi baada ya zoezi hilo kuisha rasmi leo.

“Wakuu Wote wa Idara,Mhe Waziri anataka Timu za Chapa zirudi Dodoma.Leo saa 12 jioni apate taarifa ya mwisho ya upigaji chapa. Mkurugenzi wa Mipango ratibu timu ya kukamilisha taarifa ” alisisitiza Mashingo kwenye taarifa yake aliyoitoa jana kwa Wakuu wa Idara.

Aidha amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha wamemaliza zoezi la kupiga chapa mifugo yao yote katika muda wa nyongeza uliotolewa na Serikali ambao uliamuliwa kuwa Januari 31mwaka huu.

Akizungumza katika siku za mwisho wakati anahitimisha ukaguzi na uhamasishaji wa zoezi la kupiga chapa katika Mkoa wa Kigoma, Dkt. Mashingo amewaonya baadhi ya wafugaji kutojiingiza katika matatizo ya kupiga chapa mifugo ambayo inatoka nje ya nchi ambapo amesema wakibainika watachukuliwa hatua kali.

Aidha, Dkt. Mashingo amewataka wafugaji wote wasio raia wa Tanzania waliyoingia katika mikoa ya mipakani kuondoa mifugo yao mara moja kwa kuwa haitapigwa chapa badala yake watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Katika hatua nyingine Dkt. Mashingo ambaye pia ni mtaalam bobezi katika eneo la malisho ya mifugo amesema kufanikiwa kwa zoezi la kupiga chapa kutasaidia usimamizi wa Sekta ya Mifugo hapa nchini ambapo alisema awali inakadiliwa kwamba 30% ya malisho yote nchini yalikuwa yakitumiwa na mifugo toka nje ya nchi.

Ameutaka Uongozi wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) kutopingana na Serikali badala yake kuongeza ushirikiano na kuwaelimisha wenzao kufuga kisasa ili kuondoa migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Awali Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina wakati akihitimisha zoezi la upigaji chapa mifugo kitaifa lililofanyika katika wilayani Itilima mkoani Simiyu, Desemba 31mwaka jana aliongeza siku 30 kwa halmashauri zote nchini ili kukamilisha zoezi la kupigaji chapa mifugo huku akiwavua nyadhifa maafisa wawili wa Wizara kwa kushindwa kusimamia zoezi hilo kikamilifu na wengine wawili wakipewa onyo kali.

Alida kuwa licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto zilizosababisha zoezi hilo kufanyika kwa asilimia 38.5 tu kwa nchi nzima baadhi ya watendaji wa serikali na viongozi walichangia kulikwamisha ambapo Halimashauri ambazo zikamilisha zoezi la chapa chini ya asilimia 10 zilipelekwa majina ya watendaji wao kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu.

Siku kumi na tano baada ya muda wa nyongeza wa siku thelathini, Mhe. Mpina alitoa tathmini mbele ya Waandishi wa Habari mjini Dodoma, kuhusu tathmini ya utekelezaji wa zoezi la upigaji chapa mifugo ambapo Mpina alisema hadi kufikia siku hiyo ya Januari 16 mwaka huu jumla ya ng’ombe 10,306,359 sawa na asilimia 59.3 ya lengo walishapigwa chapa ikiwa ni ongezeko la asilimia 20 ya tathmini ya awali iliyofanywa Desemba 31 Mwaka jana .

Aidha alisema wafugaji wote nchini watakaoshindwa kupiga chapa mifugo yao ndani ya muda uliowekwa hatua kali zitachukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji Namba 12 ya mwaka 2010 ibara ya 4 kifungu cha 26.

MKAZI WA DAR NA KIGOMA WAJISHINDIA KITITA CHA MILIONI 10 KILA MMOJA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


.
Akizungumza na waandishi habari wakati wa kukabidhi hundi hizo kwa washindi hao , mapema leo mbelee ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani),Mmoja wa Maofisa Habari wa Tatu Mzuka, Millard Ayo alisema droo hiyo inachezwa kila siku,huku wenye bahati zao wakiendelea kujinyakulia vitita vyao vya Tatumzuka.Milard amewaasa Watanzania waendelee kucheza kwa wingi na mara kwa mara mchezo huo,kwani ukiibuka mshindi maisha yake huinuka na kuwa bora zaidi tofauti na alivyokuwa hapo awali.Mchezo wa kubahatisha wa TatuMzuka umetoa washindi wawili wa sh. Milioni 10 katika droo inayochezwa kila siku,mmoja akitokea jijini Dar na mwingine akitokea mkoani Kigoma
Mmoja wa Maofisa habari wa mchezo wa Kubahatisha wa Tatumzuka,Millard Ayo akimkabidhi mfano wa hundi ya sh.milioni 10 kwa mshindi wa droo ya Tatu Mzuka inayofanyika kila siku ,Harieth Steven (21) mkazi wa Kigoma ambaye anajishugulisha na kazi za ndani (housegirl),mapema leo kwenye mkutano na Wanahabari (hawapo pichani),uliofanyika leo jijini Dar .
Harieth Mwenye mtoto mmoja alifurahia kujishindia donge hilo kupitia mchezo wa kubahatisha wa Tatumzuka,kwani baada ya kutaarifiwa kuwa amejishindia kiasi hicho cha fedha,akajipa matumaini ya kuwa ndoto yake ya kufanya biashara ya vitenge sasa inakwenda kutimia rasmi,na kuacha kufanya kazi za ndani.
Mmoja wa Maofisa habari wa mchezo wa Kubahatisha wa Tatumzuka,Millard Ayo akimkabidhi mfano wa hundi ya sh.milioni 10 kwa mshindi wa droo ya Tatu Mzuka ,Ally Rashid (26) mkazi wa Yombo Buza ambaye anajishugulisha na biashara ya kuuza Mboga mboga jijini Dar,mapema leo kwenye mkutano na Wanahabari (hawapo pichani),uliofanyika leo jijini Dar .

ZITTO KABWE AZUIWA KUFANYA MKUTANO WA HADHARA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Jeshi la Polisi Kigoma limemzuia Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe kufanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Uwanja wa Mwanga Community Center, mkoani Kigoma ambao ulipaswa kufanyika leo Januari 16, 2018.

Taarifa iliyotolewa na OCD inasema kuwa kiongozi huyo hakufuata utaratibu wa kutoa taarifa ndani ya masaa 48 kabla ya kufanyika kwa mkutano huo jambo ambalo Mbunge Zitto Kabwe amelilamikia na kusema kuwa amezuiwa kufanya Mkutano kinyume na sheria ya Bunge ya mwaka 1988.

"Mimi sitaki kuwapa polisi sifa ya kupambana nasi. Tumeahirisha mkutano mpaka siku ya jumamosi Lakini tumewaandikia barua rasmi kuwa sheria waliyonukuu sio sheria halali na haihusiani na mikutano ya Mbunge kwenye jimbo lake la Uchaguzi. Sheria wanayopaswa kunukuu ni sheria namba 3 ya mwaka 1988 kifungu cha 4(1)". Alisema Zitto Kabwe

Kufuatia jambo hilo Zitto Kabwe amedai kuwa atamwandikia barua rasmi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai kuhusu suala hilo ili kutengeneza mazingira kwa siku za usoni lisije kumtokea Mbunge mwingine yoyote


KATIBU MKUU WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI(MIFUGO) DK MARIA MASHINGO AHIMIZA NGOMBE WENYE UMRI WA MIEZI SITA NA KUENDELEA KUPIGWA CHAPA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Maria Mashingo akishiriki upigaji chapa mifugo katika Kijiji cha Kabanga Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma ikiwa ni sehemu ya timu ya wataalamu wa wizara hiyo iliyoko katika mikoa 26 ya Tanzania bara kufuatia na kusimamia zoezi la upigaji chapa mifugo linalotarajiwa kukamilika Januari 31 mwaka huu.
 KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Maria Mashingo akiwaeleza na wafugaji wa Kijiji cha Kabanga Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma umuhimu wa zoezi la kupiga chapa ikiwa ni sehemu ya timu ya wataalamu wa wizara hiyo iliyoko katika mikoa 26 ya Tanzania bara kufuatia na kusimamia zoezi la upigaji chapa mifugo linalotarajiwa kukamilika Januari 31 mwaka huu. 
KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Maria Mashingo akishiriki upigaji chapa mifugo katika Kijiji cha Kabanga Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma ikiwa ni sehemu ya timu ya wataalamu wa wizara hiyo iliyoko katika mikoa 26 ya Tanzania bara kufuatia na kusimamia zoezi la upigaji chapa mifugo linalotarajiwa kukamilika Januari 31 mwaka huu.
Na Kumbuka Ndatta, KASULU
KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo) Dk. Maria Mashingo ameagiza ng’ombe wote wenye umri wa kuanzia miezi sita na kuendelea kuhakikisha wamepigwa chapa kabla ya kufikia tarehe ya mwisho ya upigaji chapa Januari 31 mwaka huu, kwani zoezi hilo sio la hiari bali ni la lazima na linatekelezwa kwa mujibu wa Sheria.

Dk. Mashingo ametoa kauli hiyo wakati akishiriki zoezi la upigaji chapa mifugo katika Kijiji cha Kabanga Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma ikiwa ni sehemu ya timu ya wataalamu wa Wizara hiyo iliyoko katika mikoa 26 ya Tanzania bara kufuatia na kusimamia zoezi la upigaji chapa mifugo linalotarajiwa kukamilika Januari 31 mwaka huu.  

Dk Mashingo aliwaambia wafugaji hao kutambua kuwa zoezi hilo linasimamiwa kwa mujibu wa Sheria ya utambuzi ,usajili na  ufuatiliaji wa mifugo  Na. 12 ya Mwaka 2010 na kuwasititiza kuwa haijulikani Serikali itaamua nini kwa mifugo itakayokuwa haijapigwa chapa hadi kufikia tarehe ya mwisho iliyowekwa ya Januari 31 mwaka huu.
Aidha Dk. Mashingo alitumia fursa hiyo kuwaelimisha wafugaji sehemu maalum ambayo  ng’ombe anapotakiwa kupigwa chapa mwilini mwake ili kutoharibu ngozi yake inayotegemewa kwa  matumizi mengine.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali  Mstaafu Emanuel Maganga amesema zoezi la upigaji chapa linaendelea vizuri na mwitikio ni mkubwa kutoka kwa wafugaji ambapo jumla ya ng'ombe 93,182 wameshapigwa chapa kati ya ng'ombe 345,469 waliotambuliwa ambao ni sawa na asilimia 27.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Fatima Laay amemweleza Katibu mkuu kuwa jumla ya ng'ombe 7,552 kati ya 10,000 wenye umri wa zaidi ya miezi sita na kuendelea tayari wameshapigwa chapa ambao ni sawa na asilimia 75.52.

Kwa upande wake Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwanko alikiri kuwepo tatizo la Ng'ombe kupata vidonda vikubwa wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo jambo lilochangiwa na wafugaji kutoelimishwa sehemu sahihi ya kupiga chapa mifugo.

"Mimi ng'ombe wangu bado hawajapigwa chapa,waliopigwa chapa walipata vidonda vikubwa kwa hiyo kama wataalam wetu ngazi ya vijiji wameelimishwa vizuri jinsi ya kupiga chapa basi haina shida nitawapeleka ng'ombe wangu wakapigwe chapa na kuhamasisha wananchi wengine kuunga mkono zoezi hili "alisema Nsanzugwanko.

VIDEO: DKT. NDUGULILE AITAMBULISHA PROGRAMU YA KIKUNDI MLEZI KWA WANAWAKE WAJASILIAMALI MKOANI KIGOMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

DKT. NDUGULILE ASHIRIKI UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI YA KIJIJI CHA NYANGANGA KATIKA ZOEZI LA KUAMSHA ARI YA WANANCHI KUCHANGIA SHUGHULI ZA MAENDELEO MKOANI KIGOMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile(Mb) akishirikiana na wananchi wa Kijiji cha Nyanganga kuchanganya zege kwa ajili ya kuweka ‘rental’ kwa ajili ya madarasa manne ya Shule ya Kijiji hicho katika zoezi la kuamsha ari ya wananchi kujitolea katika kufanya shughuli za maendeleo.
Mtendaji wa Kjjiji cha Nyanganga Bw.Erick Ruhomola akitoa taarifa ya Mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kijiji chao kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile(Mb) ambao uliibuliwa, kubainishwa na kutekelezwa wananchi wenyewe na wananchi kwa takribani.
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mhe. Mwanamvua Mrindiko akimshukuru Naibu Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile(Mb) kwa kuja kuonesha mfano wa kuamsha ari ya wananchi wa Uvinza kujitolea katika shughuli za maendeleo yao.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile(Mb) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyanganga mara baada ya kushiriki zoezi la kuamsha ari katika ujenzi wa Shule ya Kijiji hicho.
Wananchi wa Kijiji cha Nyanganga wakimsikiliza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile(Mb) mara baaada ya kushirikiana naye katika zoezi la kuamsha ari ya wananchi kufanya kazi katika ujenzi wa vyumba vine vya madarasa ya shule ya Sekondari ya Kijiji chao.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile(Mb) akikabidhi mifuko 37 ya Saruji kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za wananchi wa Kijiji cha Nyanganga wa kujitolea kwa nguvu zao kujenga shule ya Sekondari ya Kijiji chao.
Baadhi ya wananchi wakifanya kazi ya kumwaga ‘rental’ katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kijiji cha Nyanganga kilichopo Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma.Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile(Mb) akitia saini katika kitabu cha wageni mara alipowasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya Ziara ya siku mbili ya kikazi Mkoani hapo.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Paul Chaote akitoa taarifa ya Mkoa kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile(Mb) katika Ziara ya siku mbili ya kikazi ya Naibu Waziri huyo Mkoani hapo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile(Mb) akisalimiana na wananchi wa Kijiji cha Nyanganga mara baada ya kuwasili katika kushiriki ujenzi wa madarasa manne ya Shule ya Kijiji hicho katika kuamsha ari ya wananchi kujitolea katika kufanya shughuli za maendeleo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Uvinza Bw. Lutabola Weja akitoa ufafanuzi wa jambo wakati wa zoezi la kuamsha ari ya wananchi kujishughulisha katika shughuli za maendeleo ambapo wanachi wa Kijiji cha Nyanganga wamejitolea na kujenga vyumba vinne vya madarasa kwa ajili ya shule ya Kijiji chao.


Na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile(Mb) ameshiriki ujenzi wa Shule ya Kijiji cha Nyanganga iliyoko kata ya Kazuramimba, wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ikiwa ni jitihada za wananchi wa kijiji hicho kuharakisha upatikanaji wa huduma ya elimu kijijini hapo.

Akiwa katika Kijiji hicho Naibu Waziri Dkt. Ndugulile ameshiriki zoezi la kumimina zege kwa ajili ya kufunga ‘rental’ ya vyumba vya madarasa ya shule hiyo.

Dkt. Ndugulile amesema lengo la kuwepo ziara hiyo ni kufuatilia utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Jamii (1996), na Sera nyingine za Wizara amabzo zinasisitiza ushiriki wa jamii katika kuibua mahitaji, kupanga, kuamua, kutekeleza, kufuatilia na utathmini shughuli za miradi ya maendeleo ikiwemo uboreshaji wa huduma ya miundo mbinu ya kufundishia na kujifunzia katika maeneo ya mijini na vijijini.

Mhe. Ndugulile ameongeza kuwa Ili kurejesha ari ya wananchi kushiriki katika maendeleo yao kuelekea uchumi wa kati na wa viwanda, Wizara imeamua kufuatilia utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Jamii katika ngazi za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuhamasisha jamii kushiriki na kuchangia shughuli za maendeleo yao kwa kufanya kazi za bega kwa bega, kuchangia nguvu zao, rasilimali fedha, rasilimali vifaa na ufundi kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundo ya elimu, afya, kilimo, mifugo, barabara na viwanda vidogo vidogo. 

“Nimeambiwa kuwa mradi wenu wa ujenzi wa shule ya sekondari katika kijiji cha Nyanganga utasaidia kusogeza huduma ya elimu jirani na wananchi, na nimevutiwa na hamasa mliyonayo katika maendeleo name nimekuja kushirikiana nanyi kuendeleza ujenzi wa madarasa ya shule kazi amabyo ni kigezo thabiti cha cha dhamira ya dhati yawananachi wa kijiji hiki katika kutoa haki ya msingi ya kumwendeleza Mtoto katika ngazi ya kijiji na jamii kwa ujumla” alisisitiza Mhe. Dkt. Ndugulile.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kjjiji cha Nyanganga Bw.Erick Ruhomola amesema kuwa Mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya kijiji uliibuliwa na kubainishwa na wananchi wenyewe na kutekelezwa na wananchi kwa takribani asilimia mia moja hadi kufikia hatua ya kumwaga zege kwa ajili ya ‘rental’.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutuona na kuja kutuunga mkono katika jitihada zetu za kujiletea maendeleo katika kijiji chetu” alisisitiza Bw. Ruhomola.Naye Mkuu wa Wilaya yaUvinza Mhe. Mwanamvua Mrindiko amemshukuru Naibu Waziri kwa kuja kuonesha mfano wa kuamsha ari ya wananchi wa Uvinza kujitolea katika shughuli za maendeleo yao.

“ Hili ni Jambo la kipekee kwa Mhe. Naibu Waziri kutembelea na kushiriki na wananchi katika ujenzi wa shule hii” alisisitiza Mhe.Mwnanamvua

Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kijiji cha Nyanganga kilichopo Wilaya ya Uvinza Mkoa wa Kigoma itawasaidia watoto wa jamii hiyo kuwa na shule karibu na makazi yao ambapo hapo awali watoto hao walikuwa wanatembea umbali wa kilometa 14 kwenda shule ya jirani.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile yupo katika Mkoa wa Kigoma kwa ziara ya siku mbili ya kikazi kufuatilia utekelezaji wa Sera mbalimbali zinazosimamiwa na Wizara yake.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa