Na Mwandishi wetu,KIGOMA.

Maafisa wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu
 (Idara ya Menejimenti ya Maafa) kwa kushirikiana na
 Shirika la Kimataifa linaloshughulikia uhamaji (IOM) wameendesha 
semina ya kujenga uelewa juu ya upunguzaji wa madhara ya 
maafa katika jamii.

Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 25 Machi 2025 katika
 Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo yamehudhuriwa na
 washiriki 50 ikiwemo Watendaji wa Kata, Watendaji wa
 Vijiji, Watendaji wa Mtaa Kamati za Maafa za Kata na
 Vijiji pamoja na mtaa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo kwa
 niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Bi.Petronila Gwakila 
ambaye ni Afisa Mazingira ndani ya Manispaa hiyo amesema, 
mafunzo hayo yameletwa wakati sahihi ambapo manispaa
 inatarajiwa kupata mvua ambazo mara nyingi mvua
 hizo husababisha maafa mbalimbali na kufanya wananchi
 kutofanya shughuli zao za kila siku za kuwapatia kipato hivyo
 mafunzo haya yataweza kuleta muamko katika kukabili 
maafa pindi yatakapotokea.

"Kwa hiyo ndugu zangu tumepata wakufunzi hawa juu ya 
masuala ya Maafa ningependa sana tuwe makini kusikiliza
 kutokana na kwamba hili jambo ni muhimu maana si mara
 moja wala mara mbili maafa hasa ya mafuriko yanatukuta
 sana katika maeneo yetu hata sasa mvua zimeshaanza na tumeanza 
kuona athari zake hivyo tusikilize ili tujue namna ambavyo tunaweza 
kujinusuru na jambo hili” amesema