Home » » TAFSIRI YA ZITTO KUONDOKA CHADEMA

TAFSIRI YA ZITTO KUONDOKA CHADEMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


AWALI ya yote nichukue fursa hii kumpongeza kwa dhati ndugu Zitto Kabwe katika hatua hii nyingine ya safari yake ya kisiasa.
Nina bahati ya kumfahamu Zitto tangu akiwa kijana sana ndani ya siasa za upinzani na, hususan, ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Nakumbuka katika sehemu ya mazungumzo yetu ya Juni, 2004, tulizungumza kwa kirefu juu ya maana na umuhimu wa itikadi kwenye uongozi wa kuwatumikia wananchi.
Nilifahamu, kuwa Zitto alikuwa mjamaa mwenzangu. Kama leo amechagua chama anachokielezea kuwa kinasimamia misingi ya Ujamaa, hivyo, falsafa za Mwalimu Nyerere, basi, yumkini Zitto yuko kwenye njia sahihi. Maana, kwenye itikadi kuna Kushoto, Kulia, Katikati kuegemea Kushoto au Katikati Kuegemea Kulia. Siku zote, kiitikadi Kushoto ni kwa Wajamaa, na kulia ni kwa Waafidhina ( Mabepari).
Ninapokitafakari sasa chama cha ACT, najiuliza, kama kimesimama Kushoto zaidi ya kushoto au kushoto tu? Si muda mrefu majibu yataanza kupatikana. Hivyo, ndipo nami nitakapojua, kuwa Zitto Kabwe amesimama wapi hasa.
Vinginevyo, hii ni nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Nchi yetu inahitaji siasa za upinzani. Uwepo wa tofauti ya mawazo na mitazamo ni jambo jema. Na usiwe upinzani tu, bali upinzani ulio makini wenye kujiainisha kiitikadi na kuzisimamia itikadi hizo.
Hatuhitaji utitiri wa vyama, bali, vyama vichache vitakavyojipambanua kiitikadi, ili huko tuendako, vyama hivyo viweze kuunda Serikali za Mseto, kwa misingi ya kufanana kimtazamo ya kiitikadi. Vinginevyo, miseto mingine huzaa serikali dhaifu.
Na ujenzi wa chama kipya si kazi nyepesi. Nimepata kuandika, kuwa mti mmoja haufanyi msitu. Chama cha siasa ni wanachama. Na lengo ni kukubalika na wengi hata nje ya chama ili kiweze kushinda uchaguzi na kushika dhamana ya uongozi wa dola. Kazi ya kufikia malengo hayo kamwe haiwezi kufanikishwa na mtu mmoja.
Na kwa vyama hivi vya siasa, vifanye yote kuhakikisha kuwa dhana ya uongozi wa pamoja katika chama inabaki hai. Yumkini, wanaweza kutokea wanachama binafsi wenye kuonyesha nia za kutaka kuwa madiwani, wabunge hata urais.
Lakini, kamwe isifanywe kuwa isiyo na umuhimu, michakato ya pamoja ya ndani ya chama, katika kuwapata wagombea. Na wenye nia makini za uongozi, huwa ni wenye kutanguliza mapenzi kwa chama.
Huwa ni wenye kuangalia maslahi mapana ya chama chao, badala ya kutanguliza maslahi yao binafsi na ya makundi yao.
Dhana ya wagombea binafsi ndani ya vyama nayo haijapata kujadiliwa kwa mapana. Maana, wagombea binafsi kimsingi wangesaidia kuimarisha demokrasia ya ndani ya vyama (intra-party democracy).
Njia hii itavinusuru pia vyama vya siasa katika hatari ya kusambaratika zaidi. Kimsingi, kwa kuruhusu wagombea binafsi kuwania nafasi za uongozi nje ya vyama kutawafanya wagombea hao wasione umuhimu wa kushiriki katika siasa za vyama.
Kuna umuhimu pia wa mgombea kuwa na utambulisho wa chama.
Mgombea anayewakilisha wananchi bungeni au kwenye baraza la madiwani anafanya shughuli ya siasa.
Hivyo basi, ni vema mtu huyu nyuma yake akawa na
chama ambacho itikadi, madhumuni, malengo na sera zake anakubaliana nazo.
Asipokiona chama chenye itikadi, sera na malengo yanayomridhisha yeye, basi mtu huyu apewe uhuru wa kushirikiana na wenzake wenye mawazo yenye kufanana ili aanzishe chama chake cha siasa.
Tusikubali kujenga utaratibu utakaoruhusu wagombea binafsi
waharibu dhana nzima ya siasa na itikadi za vyama vya siasa. Kama taifa, tumeazimia kujenga na kuimarisha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.
Hata tukiwa na wagombea wengi, basi, watokane na vyama vingi. Kuruhusu wagombea binafsi bila sharti la ushiriki wa siasa za vyama si tu ni kukaribisha vurugu za kisiasa, bali pia tunawaweka wananchi kwa maana ya wapiga kura
wetu katika wakati mgumu.
Badala ya kuangalia mgombea na sera za chama chake, wengi wa
wapiga kura watajikita zaidi katika kumwangalia mgombea, umaarufu wake, sura yake, namna anavyosaidia kutoa michango ya hapa na pale na kadhalika.
Umaarufu wa mtu na kwa kusaidiwa na fedha na labda vyombo vya habari unaweza kutangulizwa mbele badala ya kuangalia umahiri wake ikiwamo sera na misingi ya kiitikadi aliyosimamia mgombea husika.
Utaratibu wa mgombea binafsi ndani ya chama umwezeshe mgombea aliye mwanachama wa chama cha siasa kupewa haki ya kisheria.
Haki ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya uongozi wa kuchaguliwa na wananchi hata kama hakupitishwa na vikao halali vya chama husika. Tutoe mfano: mgombea X ni mwanachama wa chama Y. Amechukua fomu ya kugombea ubunge kwa tiketi ya chama chake Y.
Lakini chama chake hakikumpitisha kuwania nafasi anayoitaka ya kuwatumikia wananchi. Basi, mgombea X awe na haki ya kikatiba na kisheria ya kuchukua fomu ya kugombea kama mgombea binafsi kwa tiketi ya chama Y.
Mgombea huyu X akiwa majukwaani aonekane kuwa ni mgombea binafsi lakini ni mfuasi na mwanachama wa chama Y. Hata akiingia bungeni atatetea sera na itikadi za chama Y.
Endapo ikitokea katika kipindi chake cha ubunge mgombea X atadhani ameshindwa kubaki bungeni kutetea sera na itikadi za chama hicho, basi anaweza kufikia uamuzi wa kujivua unachama.
Inawezekana pia mgombea X akavuliwa uanachama na chama chake. Basi, mgombea X abaki kikatiba na kisheria, kuwa ”mbunge pori” hadi kipindi cha uwakilishi wake wa wananchi bungeni kitakapofikia ukomo.
Endapo mgombea X atapenda tena kutetea kiti chake cha ubunge katika uchaguzi utakaofuatia, basi, atalazimika
kujiunga na chama kingine cha siasa au kujiundia chama chake cha siasa.
Maana, katika hili la wagombea binafsi tusije tukatoka kwenye dhana nzima ya chama na umuhimu wake. Tukumbuke, mojawapo ya tafsiri ya chama cha siasa ni kama hii ifuatayo; chama cha siasa ni mkusanyiko wa watu wenye itikadi, madhumuni, shabaha na malengo yenye kufanana.
Ni chama kilichojiwekea kanuni za kufuatwa kwa viongozi na wanachama wake. Katika hilo la hapo juu ni vigumu kukawa na chama cha siasa kitakachodumu muda mrefu kikiundwa na watu wenye itikadi tofauti na wasiokubaliana katika madhumuni na malengo ya msingi.
Kikishindwa kuwa na hivyo muhimu, hakiwezi kuwa na kanuni zitakazofuatwa. Hicho ni chama kwa nadharia, lakini kimatendo, ni mkusanyiko wa vikundi vya watu wenye malengo, madhumuni na shabaha tofauti chini ya kivuli cha “chama nadharia”.

Chanzo:Raia Mwema

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa