Home » » CHANGAMOTO KUU YA CHAMA CHA ACT SI CHADEMA NA YA CHADEMA SI ACT

CHANGAMOTO KUU YA CHAMA CHA ACT SI CHADEMA NA YA CHADEMA SI ACT

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

KOSA moja kubwa ambalo chama kipya cha siasa ambacho kinatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwishoni mwa juma cha Alliance for Change and Transparency (ACT) kinaweza kufanya ni kudhania kuwa changamoto kubwa dhidi ya maendeleo yake ni Chama Kikuu cha Upinzani nchini, Chadema.
Na kinyume cha hili pia ni kweli; kwamba, litakuwa kosa – na naamini tayari limekuwa kosa – kwa Chadema kudhania hata kwa sekunde chache kuwa changamoto yake kubwa zaidi ni chama hiki kipya ambacho wiki iliyopita kimetangaza zaidi jina lake baada ya aliyekuwa Mbunge wa Chadema, Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini) kwa kujiunga nacho.
Nalisema hili kwa sababu kwa muda sasa, vyama hivi viwili vinaonekana vimeshikana mapembe kiasi kwamba sioni ni namna gani vitaachiana ili viweze kushiriki Uchaguzi Mkuu vikiwa ni tishio kubwa zaidi kwa watawala wa sasa. Kuanzishwa kwa ACT kwa wanaokumbuka inaonekana moja kwa moja ilikuwa ni majibu kwa kile ambacho waanzilishi wake walikiona ni kuminywa kwa Demokrasia ndani ya Chadema.
Ndio sababu baadhi ya watu waliokuwa nyota na viongozi wakubwa ndani ya Chadema waliweza kujiunga nacho mara moja na tukiweka rekodi kwa usahihi walihusika vyema katika uanzilishi wa chama hicho.
Ni wazi basi haiwezekani kutenganisha uhusiano kati ya vyama hivi viwili; kimoja kikiwa ni chama ambacho mwangaza wake umeangaza vya kutosha na kuwa tishio na kingine kikijaribu kuingia na nuru yake mpya kuangaza na kwa namna kuweka kivuli kwa hicho kingine. Vyama vyote viwili naamini vinaweza kabisa kuangaza na yawezekana mwangaza wa vyote viwili unaweza kuwa ni mzuri zaidi katika kuondoa giza ambalo limetawala taifa letu kisiasa.
Hili hata hivyo kufanyika siyo rahisi mpaka pale vyama hivi na hasa ACT kutambua kwanza kabisa changamoto yake kubwa ni nini. Ni rahisi kwa Chadema kujivunia na kutangaza kila mwanachadema anayejiunga nacho ili kuonesha kuwa Chadema sasa kimefifia. Hili linaweza kuwa ni mkakati mzuri kwa muda lakini ni mkakati ambao tunaofuatilia siasa za Tanzania, tunajua matunda yake kwani tumekwishawahi kuuona huko nyuma na haujaisha.
Tangu kurudi kwa vyama vingi vya siasa tumeshuhudia ninachoweza kukiita sanaa ya kutafuta ujiko pale ambapo wanachama wasioridhika kutoka chama kimoja hurudi au hujiunga na chama kingine kwa mbwembwe nyingi. Hili si geni kabisa katika siasa zetu. Tangu Augustine Mrema alipojiondoa CCM na kujiunga NCCR-Mageuzi, siasa zetu zimeshuhudia wanasiasa wengine maarufu kweli kweli wakijitoa ama CCM au kutoka vyama vingine na kujiunga na vyama vingine. Kwa muda mrefu hilo limekuwa tu ni suala la kisiasa na wanasiasa zaidi kuliko suala la vyama.
Na hili siyo la watu ambao ni viongozi tu; tumeshuhudia karibu kila mahali ambapo kunafanyika mikutano ya vyama vya siasa wananchi wakirudisha kadi za chama kimoja na kujiunga na chama kingine na siwezi kushangaa inawezekana kabisa wananchi hao hao hujiunga na kuondoka kwenye vyama hivi kama vipepeo. Leo akija Nape Nnauye na Abdulrahaman Kinana, basi wananchi hurudisha kadi zao za Chadema au CUF na kujiunga CCM huku wakivishwa magwanda ya kijani na njano halafu siku chache baadaye, Slaa na Mbowe wakipita wanarudisha zile za CCM na kujiunga Chadema. Na wakati mwingine kinyume cha hilo pia hutokea.
Lakini katika hili la sasa ukiondoa haya ya wanachama vipepeo ambao hufuata maua popote yanapochanua upo hasa mgogoro wa ndani wa kisiasa. ACT inaamini – au inajionesha kuamini – kuwa siasa za Chadema hazina nafasi tena huku Chadema wakiona ACT imekuja kutibua harakati zake za kuing’oa CCM. Matokeo yake ni haya ambayo tumeyaona na sitoshangaa hadi siku ya kuzinduliwa ACT wiki hii, mengine mengi tutayaona. Sitoshangaa nikisikia kina John Shibuda naye ametoka Chadema na kuingia ACT (ila sidhani kama anaweza kufanya sasa kabla ya Bunge la Bajeti!) au kuvunjwa kwa Bunge rasmi baadaye mwaka huu.
Tayari ACT imetumia muda mwingi sana na rasilimali nyingi kushindana na Chadema na tumeona Chadema nayo wanajitahidi kila ilivyo kuhakikisha kuwa ACT haing’ai na wanajaribu kuifanya duni mbele ya wananchi na labda ni kitu hicho hicho kinawafanya watu wengine kujiunga nayo. Kama nilivyosema hapo juu haya ni makosa na ninaamini yatakuwa makosa makubwa kwa ACT.
Vyama hivi ni lazima vitambue kuwa kikwazo kwao kikubwa zaidi ni utawala wa Chama Cha Mapinduzi. Muda na rasilimali ambazo vyama hivi vinatumia kushindana vyenyewe ni muda ambao ulipaswa kutumiwa dhidi ya Chama Cha Mapinduzi. Bahati mbaya sana inaonekana hili ni gumu sana na linaweza kuwa gumu kwa sababu kwa muda mrefu watu ambao wameonekana wamefurahia kuja kwa ACT wengine wana CCM – sitarajii wana CCM wengi watakimbilia kujiunga ACT kwa sababu wanaipenda sana kuliko Chadema! Nina uhakika ACT wakianza kushambulia CCM na kuachana na Chadema, CCM wale wale ambao walikuwa wanaonekana wanamuonea huruma Zitto na ambao walikuwa wanaunga mkono kuondoka kwake Chadema watageuka tena na kuanza kumyumbisha Zitto. Hata wale ambao wameonekana wakitoa kauli za huruma, hao hao wanaweza wakawa wakali kweli kweli Zitto akianza kuwazodoa na kuwagusa maslahi yao ya kutawala.
Ni kwa sababu hiyo viongozi wa vyama hivi wanahitaji kufikiria jambo kubwa zaidi hasa kuelekea kwenye kampeni. Kama wataweza kukaa pamoja na kuamua kutangaziana amani ama wataamua kuoneshana nani ni nani na kwa nini. Viongozi hawa ambao wamewahi kugongana huko nyuma umefika wakati waweke sifa na viburi vyao chini, ili waweze kuona kama wanaweza kushirikiana na kuwa hata wanachama watakapoondoka upande mmoja kwenda mwingine basi isiwe sababu ya kutumia muda mwingi sana kushambuliana.
Hili kwa kiasi kikubwa linahitaji Chadema kama Chama Kikuu cha Upinzani kukubali kuwa Zitto katoka na wapo watakaondoka naye. Badala ya kujaribu kuwabeza na kuwaita kila majina Chadema inahitaji kutoa kauli moja ya kuwatakia safari njema wale wote wanaotaka kutoka na kuachana na mada hiyo kwa ujumla wake, kwani inawapotezea nafasi nyingine nyingi ya kujipanga wenyewe kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Aneyataka kutoka atatoka. Na kwa ACT wanahitaji kutumia muda wao kujijenga lakini wakifikiria watajijenga zaidi kwa kutumia waliokuwa wanachama wa Chadema watashangaa kuwa watajikuta wamechukua wachache maarufu lakini hawatoweka msingi (base) mkubwa wa chama. Kwenye bahari yenye samaki wengi kugombania waliovuliwa na mwenzio siyo tu ni jambo la kusikitisha lakini pia linaweza kuwa jambo la kusababisha watu kuuliza, labda mwenzetu hujui kuvua baharini; unajua kuvua zaidi kwenye mitumbwi ya wenzako.
ACT ikitaka isimame ni lazima itengeneze wanachama wake nje ya wale walioko kwenye vyama vingine; labda hapa ndio umahiri wa Zitto na wenzake unaweza kupimwa. Hatuwezi kupima kwa marafiki na jamaa waliokuwa pamoja kuja kujiunga kwani hilo ni rahisi sana kufanyika na tumeshaliona likifanyika huko nyuma.
Wakijua tatizo lao ni CCM na utawala wake ambao umechomeka kucha zake kali kwenye migongo ya Watanzania labda, na ninasema labda watatambua kuwa vijimigogoro vyao ni kama kupigana kwa dagaa wawili kwenye bahari inayotawaliwa na nyangumi. Inawezekana hata ugomvi mzima wa dagaa hao unafanyika kwenye tumbo la nyangumi!

Chanzo:Raia Mwema

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa