Home » » Serikali yatahadharisha matumizi ya simu feki.

Serikali yatahadharisha matumizi ya simu feki.

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
06/09/2016
Serikali imetahadharisha na kuendelea kuelimisha umma juu ya matumizi ya  simu feki ili kuepuka madhara yatokanayo na matumizi ya simu hizo na kulinda afya kwa watumiaji.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa wakati akijibu swali la Mhe. Bahati Ali Abeid kuhusu Serikali kutoa Elimu kwa Umma juu ya matumizi ya simu hizo.

Prof. Mbarawa amesema kuwa Serikali inaendelea kutoa tahadhari pamoja na kutoa elimu kwa umma waweze kujiepusha na matumizi ya simu hizo ikiwa ni pamoja na kuzikusanya na kuziteketeza kwa mujibu wa utaratibu uliopo.

Aliongeza kuwa wananchi wanaoendelea kutumia simu hizo zisizokidhi viwango vya kulinda afya za watumiaji ama zenye namba za utambulisho (IMEI) bandia, wanaweza kudhurika na matumizi yake kwani hazikutengenezwa kwa mfumo unaotakiwa.

“Nitoe wito kwa wananchi wote kabla ya ununuzi wa simu, kuikagua kwa kuiwasha na kuona kama ina namba ya utambulisho (IMEI) ili kujua kama ni feki au ni halali,” alifafanua Prof Mbawara. 

Aidha, akijibu swali la Mhe. Balozi Dkt. Diodorus Kamala kuhusu kulipa fidia kwa wananchi waliotoa maeneo kupisha Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Omukijunguti, Prof Mbarawa alisema kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kuanza kulipa fidia wananchi wa Omukajunguti mkoani Kagera mara baada ya taratibu za marejeo ya uthamini zitakapokamilika.

Zaidi ya hayo Prof Mbarawa amesema kuwa Serikali itaendelea na maandalizi ya awali kwa ajili ya Kiwanja cha Omukajunguti kwa kukamilisha ulipaji wa fidia, kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali ili kubaini makadorio ya gharama za uwekezaji.

Ujenzi huo wa kiwanja kipya cha ndege mkoani Kagera uliopo katika eneo la Omukajunguti ni mpango wa maendeleo wa Serikali wa muda mrefu katika kurahisisha huduma ya usafiri wa anga nchini.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa