06/09/2016
Serikali imetahadharisha na kuendelea kuelimisha umma juu ya matumizi ya simu feki ili kuepuka madhara yatokanayo na matumizi ya simu hizo na kulinda afya kwa watumiaji.
Kauli
hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa wakati akijibu swali la Mhe. Bahati Ali
Abeid kuhusu Serikali kutoa Elimu kwa Umma juu ya matumizi ya simu
hizo.
Prof.
Mbarawa amesema kuwa Serikali inaendelea kutoa tahadhari pamoja na
kutoa elimu kwa umma waweze kujiepusha na matumizi ya simu hizo ikiwa ni
pamoja na kuzikusanya na kuziteketeza kwa mujibu wa utaratibu uliopo.
Aliongeza
kuwa wananchi wanaoendelea kutumia simu hizo zisizokidhi viwango vya
kulinda afya za watumiaji ama zenye namba za utambulisho (IMEI) bandia,
wanaweza kudhurika na matumizi yake kwani hazikutengenezwa kwa mfumo
unaotakiwa.
“Nitoe
wito kwa wananchi wote kabla ya ununuzi wa simu, kuikagua kwa kuiwasha
na kuona kama ina namba ya utambulisho (IMEI) ili kujua kama ni feki au
ni halali,” alifafanua Prof Mbawara.
Aidha,
akijibu swali la Mhe. Balozi Dkt. Diodorus Kamala kuhusu kulipa fidia
kwa wananchi waliotoa maeneo kupisha Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Omukijunguti, Prof Mbarawa alisema kuwa Serikali imetenga
kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kuanza kulipa fidia wananchi
wa Omukajunguti mkoani Kagera mara baada ya taratibu za marejeo ya
uthamini zitakapokamilika.
Zaidi
ya hayo Prof Mbarawa amesema kuwa Serikali itaendelea na maandalizi ya
awali kwa ajili ya Kiwanja cha Omukajunguti kwa kukamilisha ulipaji wa
fidia, kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali ili kubaini
makadorio ya gharama za uwekezaji.
Ujenzi
huo wa kiwanja kipya cha ndege mkoani Kagera uliopo katika eneo la
Omukajunguti ni mpango wa maendeleo wa Serikali wa muda mrefu katika
kurahisisha huduma ya usafiri wa anga nchini.
0 comments:
Post a Comment