Home » » CHADEMA: Serikali inachangia umaskini

CHADEMA: Serikali inachangia umaskini


na Sitta Tumma, Sengerema
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa umaskini unaowakabili wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa unasababishwa na ‘udhaifu’ wa serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA taifa, na aliyekuwa mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, na kuongeza kuwa umefika wakati Watanzania waanze kujiandaa kukiangusha chama hicho ifikapo mwaka 2015, au kabla ya hapo.
Akizungumza kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika kwenye vijiji vya Mbugani na Kakobe jimbo la Buchosa, wilayani Sengerema ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za Movement for Change (M4C) za chama hicho, alisema wananchi wa Kanda ya Ziwa wanakabiliwa na maisha magumu kupita kiasi, wakati wanaishi, wanalala, wanatembea na kukalia rasilimali nyingi na za kila aina.
Alisema njia pekee ya kujikomboa na hali hiyo ni kuiangusha CCM katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015..
“Wananchi wa Kanda ya Ziwa amkeni, serikali hii haiwatakii mema katika maisha yenu. Umaskini unawapiga wakati mna kila rasilimali...mna utajiri wa madini, mbuga za wanyama, maziwa na samaki, lakini rasilimali hizi haziwasaidii.
“CHADEMA tumeliona hili, ndiyo maana wabunge wenu wa CCM wanazibwa midomo na serikali kwa kupewa nafasi za uwaziri, ili wawe watetezi wakuu wa serikali na si kuwatetea ninyi. Jiandaeni mwaka 2015 tuiangushe CCM na CHADEMA iingie madarakani kulikomboa taifa hili,” alisema Lema.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa