Mwandishi wetu, Kigoma Yetu
Kukamilika kwa utayarishaji wa mpango shiriki wa rasilimali za maji katika bonde la ziwa Tanganyika unaofanywa na kampuni ya SMEC kutasaidia kuzifanya halmashauri na mamlaka za maji katika bonde hilo kupanga matumizi sahihi kulingana na mahitaji yao.
Hayo yameelezwa na washiriki wa mkutano wa wadau uliokuwa ukipitia taarifa ya awali ya mtaalam mshauri ikieleza kile ambacho mtaalam huyo anatarajia kufanya katika kutayarisha mpango huo.
Afisa maji wa mamlaka ya bonde la ziwa Tanganyika, Chobariko Rubabwa alisema kuwa baada ya kazi ya wataalam hao watakuwa na taarifa sahihi na takwimu za kina za kujua kiwango cha maji kilichopo katika maeneo ya bonde hilo jambo ambalo litawawezesha kujua nini wafanye katika mipango ya matumizi yao ya maji.
Rubabwa alisema mpango huo wa mtaalam huyo mshauri utaeleza jinsi ya matumizi na usimamizi endelevu wa maji ambao utashirikisha wadau mbalimbali vikiwemo viwanda vikubwa na vidogo, wakulima na matumizi ya kawaida ya jamii zinazoishi katika bonde hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa maendeleo ya maji kutoka wizara ya maji alisema kuwa uwepo wa mpango utasaidia kuwaweka wadau pamoja katika kuhifadhi mazingira ya bonde na matumizi endelevu ya rasilimali za maji zilizopo kwenye bonde hilo.
Alisema kuwa kuwepo kwa mkutano huo kutamuwezesha mtaalam mshauri kupata maoni mbalimbali kutoka kwa wadau na uzoefu kutoka katika maeneo yao ili kuona nini kinaweza kufanyika kwa pamoja katika kuweka sawa taarifa za utekelezaji za mpango huo.
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment