Na Mwandishi Wetu, Kigoma.
MKURUGEZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma bi Miriam Mbaga amewataka viongozi wa kamati za watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wadau mbalimbali kuweka mikakati endelevu ya kuwasaidia watoto hao kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Alisema hayo hivi karibuni wakati akifunga mafunzo ya ujasiliamali kwa watendaji na viongozi wa kamati za watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika kata za Kazuramimba, Kandaga, Mkongoro, Nguruka, Mkigo, Wilaya mpya ya Uvinza na Kalinzi.
Alisema kuwa lengo la serekali ni kuandaa mpango mkakati ambao utasaidia watoto hao waweze kujitegemea wenyewe kwa kuhakikisha fedha zinazo tolewa na Halmashauri zinatumika ipasavyo.
Aidha ili lengo liweze kufikiwa ni lazima kamati zinazo shughulika na utambuzi wa watoto hao na watendaji kuhakikisha wanasimamia kwa umakini akaunti za watoto ikiwa ni pamoja na kubuni mbinu mbalimbali za kuendelea kutunisha mfuko huo.
“naahidi kuwa kipaumbele kushirikiana na kamati na wadau kutetea haki za watoto ikiwa ni pamoja na kufungua akaunti zote zilizofungwa na ifikie wakati kamati hizo zinakuwa za ustawi wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu”alisema bi Mbaga.
Kwa upande wake mratibu wa MWOCACHI (Women and care of children) bi Zainabu Bilandeka alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha watendaji na kamati za watoto wanakuwa kitu kimoja katika utunzaji na ubunifu wa miradi ili kutunisha mfuko kwa faida ya watoto hao.
Hata hivyo mkufunzi bi. Pamela Kijazi aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanafuata kanuni na miongozo mbalimbali ya utoaji na upokeaji wa fedha na mali mbalimbali zinazo tolewa na Serekali, wadau, mashirika na asasi mbalimbali kwa lengo la kuwasaidia watoto hao.
Bi Kijazi aliwataka watendaji kuhakikisha wanaandaa ripoti mbalimbali zinazohusu taarifa za watoto hao kwa kila robo ya mwaka na mwaka mzima ili kujua takwimu halisi za watoto hao.
0 comments:
Post a Comment