![]() |
Kamanda Fraiser Kashai. |
Jeshi la Polisi mkoani Kigoma
linawashikilia askari wake wawili kwa tuhuma za kumpiga na kusababisha
kifo cha mkazi wa kijiji cha Herushingo, wilayani Kasulu, mkoani Kigoma,
Gasper Mussa.
Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, Fraiser Kashai,
aliwataja askari hao kwa waandishi wa habari mjini hapa kuwa ni mwenye
namba NCC 8622 Koplo Peter na G.1236 Konstebo Sunday. Alisema wawili hao
wanadaiwa kumpiga Mussa walipokuwa kwenye kilabu cha pombe usiku wa
Sikukuu ya Krismasi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda Kashai, Mussa
alifariki siku moja baada ya kupata kipigo hicho alipokuwa akipelekwa
hospitalini baada ya kukaa mahabusu kwa siku moja.
Akisimulia tukio
hilo, Kamanda Kashai alisema siku ya tukio, Mussa na askari hao walikuwa
wakinywa pombe katika kilabu cha pombe na wakati wakinywa, ikatokea
vurugu ambapo inadaiwa kusababishwa na Mussa kukataa kulipa pombe
aliyokunywa.
Baada ya Mussa kukataa kulipa, Kamanda Kashai alisema
askari hao ambao kwa sasa wanahifadhiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi
wilayani Kasulu, walianza kumuadhibu kwa kumpiga na baadaye walienda
kumlaza mahabusu.
Hata hivyo, siku iliyofuata, Kamanda Kashai
alisema Mussa alizidiwa ndipo Mkuu wa Kituo cha Polisi Herushingo,
alianza jitihada za kumpeleka Mussa hospitali, lakini alifariki mikononi
mwa polisi kabla ya kufikishwa hospitali.
Alisema baada ya tukio hilo, alituma askari wake kufuatilia kwa undani kujua kile kilichotokea ili wachukue hatua.
Kwa
sasa Kamanda Kashai alisema hatua za kijeshi kwa askari hao
zinaendelea ikiwa ni pamoja na kuwavua hadhi ya kijeshi waliyonayo
kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Katika
tukio lingine Polisi mkoani Kigoma inamshikilia Hassan Shija, mwalimu
wa fani ya umeme katika Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (Veta)
mkoani Kigoma kwa tuhuma za kumpiga mapanga na kumjeruhi mke wake
sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda Kashai alimtaja mwanamke
huyo kuwa ni Rida Mbili ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa
Kigoma ya Maweni na kwamba chanzo cha mgogoro huo ni wivu wa mapenzi.
Chanzo : Zero 99
0 comments:
Post a Comment