Home »
» Machali ahoji wizi wa dawa hospitalini
Machali ahoji wizi wa dawa hospitalini
|
|
MBUNGE wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), amehoji
kama serikali imedhamiria kukomesha tabia ya uzembe na wizi
unaosababisha ukosefu wa dawa katika hospitali nyingi nchini.
Pia mbunge huyo alihoji kama serikali ipo tayari kuipatia madaktari
wa kutosha Hospitali ya Wilaya ya Kasulu ambayo ina upungufu mkubwa wa
madaktari na madaktari waliopo wamekuwa wakikataa wenzao wasipelekwe
kwa kuhofia kuchukua nafasi zao.
“Changamoto nyingi za ukosefu wa dawa zinatokana na wizi na uzembe wa
watendaji. Serikali iko tayari kuhakikisha jambo hilo linakoma mara
moja?” alihoji Machali.
Katika swali la msingi, mbunge huyo alitaka kujua mpango wa serikali
wa kuongeza watumishi kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kasulu ambayo
wastani wa watumishi wa afya ni 600, lakini kwa mujibu wa taarifa ya
Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO), watumishi waliopo ni 186.
Akijibu maswali hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia, alisema serikali inapeleka
watumishi katika maeneo yote kadiri wanavyopatikana kulingana na
mahitaji.
Alisema serikali inatambua upungufu wa watumishi wa sekta ya afya
nchini na kuongeza kuwa imeweka mkakati maalumu wa kuajiri wahitimu
wote wanaomaliza vyuo vya afya.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa sasa ina watumishi 359 wa
kada mbalimbali za afya wakiwamo madaktari na wauuguzi wanaotoa huduma
za afya kwenye Wilaya ya Kasulu.
Alisema Hospitali ya Wilaya ina watumishi 206, vituo vya afya vina watumishi 52 na zahanati zina watumishi 101.
“Kwa kuzingatia umuhimu wa watumishi wa kada za afya katika mwaka wa
fedha 2012/2013 serikali ilitoa kibali cha kuajiri watumishi 41 wa
sekta ya afya ambapo hadi Oktoba mwaka huu watumishi 28 wa kada za afya
wamesharipoti katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu,” alisema
Ghasia.
CHANZO;TANZANIA DAIMA
|
|
0 comments:
Post a Comment