Home » » OPERESHENI PAMOJA DAIMA ILIYOFANYIKA KIGOMA

OPERESHENI PAMOJA DAIMA ILIYOFANYIKA KIGOMA


Viongozi wa Chadema walipokuwa Kigoma kwenye Operersheni Pamoja Daima

Wakazi wa Kigoma waliojitokeza kwenye mkutano wa Operesheni Pamoja Daima.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimepasua ngome ya mbunge wake, Zitto Kabwe na kuzidi kujiimarisha kisiasa katika jimbo la Kigoma Kaskazini.
Timu ya viongozi wa CHADEMA wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Said Issa Mohamed, Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano, John Mnyika iliwasili jana na kuitikisa Kigoma kwa mikutano ya M4C Operesheni Pamoja Daima.
Hamasa ya wananchi wa Kigoma hususan katika Kata ya Mikongolo iliyoko katika jimbo la Kigoma Kaskazini, ilijionyesha wazi baada ya timu hiyo kupokewa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wakiimba nyimbo za kukisifu chama hicho huku wakilazimika kutembea umbali wa kilometa 3 kwenda eneo la mkutano kutokea mahali ilipotua helkopta.
Kutokana na umati wa wananchi kuwa mkubwa, watumiaji wengine wa barabara wakiwemo waliokuwa wakiendesha magari, walilazimika kusimama pembeni mwa barabara kupisha msafara huo wa viongozi, huku nderemo, vifijo pamoja na ishara za salamu za chama hicho, zikitawala.
Wakihutubia katika maeneo mbalimbali ya mkoani hapa wakianzia wilayani Uvinza (Nguruka), Kigoma Kaskazini (Mikongolo na Kagunga) na Kigoma mjini, viongozi hao wameendelea kuzungumzia ajenda za operesheni hiyo ambayo ni pamoja na masuala ya mchakato wa katiba mpya, umuhimu wa Watanzania kudai kuboreshwa kwa daftari la wapiga kura, matumizi ya rasilimali za nchi kwa faida ya wananchi na hali ya ugumu wa maisha ambayo wamekuwa wakiihusisha na uongozi mbovu unaosimamia sera zilizoshindwa.
Akizungumza katika mikutano iliyofanyika jana katika maeneo mbalimbali ya Kigoma wakianzia wilayani Uvinza (Nguruka), Kigoma Kaskazini (Mikongolo na Kagunga) na Kigoma mjini, Makamu Mwenyekiti Mohamed alisema kuwa lengo la operesheni hiyo ya CHADEMA awamu hii ni kuwatembelea wananchi nchi nzima ili kujadiliana nao masuala hayo muhimu kwa taifa.
Mbali ya kuwashukuru wananchi na hususan wanachama wa CHADEMA mkoani Kigoma kwa kuendelea kusimama na kukipenda chama chao, Makamu Mwenyekiti huyo alisema kuwa wameamua kuwa sauti ya Watanzania wanyonge katika masuala yanayohusu mustakabali wao, hivyo hawataruhusu mtu yeyote, awe mwanachama au kiongozi, kukiyumbisha chama kwa maslahi binafsi.
“Chama chenu kimetambua kuwepo kwa hila na njama za kutaka kukisambaratisha. Kuna watu waliingia kwenye chama hiki kwa ajili ya malengo ya kukisambaratisha, bahati nzuri kwetu na bahati mbaya kwao ni kwamba mbinu hizo zimefeli kwa sababu zimebainika,” alisema Mohamed huku akionekana kuungwa mkono na watu wa Mkongolo.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati Kuu, Lema, aliwaasa Watanzania kuwa ili nchi yao ikombolewe kuondokana na watu aliodai ni wakoloni weusi wanaofanya kazi kwa mwavuli wa CCM, kunahitajika chama kimoja chenye nguvu ambacho kitasimama imara kwa ushirikiano na wananchi wenyewe.
Lema pia alitumia fursa ya mikutano ya jana kukemea propaganda za udini ambazo zimekuwa zikienezwa mkoani humo na nchi nzima kwa ujumla zikitumiwa na baadhi ya wanasiasa wanaofilisika na kuishiwa hoja kama ngao ya kujikinga kila wanapotuhumiwa usaliti na kukosa uadilifu katika masuala ya uongozi.
“Ndugu zangu wana wa Kigoma naomba msishiriki katika dhambi ya udini inayopandwa na baadhi ya watu wachache wasioitakia mema nchi yetu. Hii dhambi haitatibika kamwe, kaeni mbali na uovu huu. Wanaoupanda wana malengo yao…achaneni nao. Tujadilini mambo ya msingi yanayotukabili sote kama Watanzania,” alisema Lema.
Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano, Mnyika, alisisitiza kwamba chama hicho kitaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kinidhamu kwa wanachama wake hususan kwa viongozi ambao watabainika kwenda kinyume na taratibu za chama hicho.

1 comments:

Anonymous said...

Kaka umeandika habari kwa kuonyesha upande uliopo.Mbona hujasema kwa nini timu ya OPM M4C haikwenda kwenye ..... inayoaminika kwa Zitto???.

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa