Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
ABIRIA asiyefahamika jina ametelekeza begi lenye vipande vya meno
ya tembo katika basi la Adventure lifanyalo safari zake kati ya Mpanda
na Kigoma mjini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kigoma, Frasser Kashai, alisema kuwa tukio hilo limetokea jana saa 10
jioni baada ya basi hilo kufika Kigoma mjini na abiria wote kuteremka
ndipo mmiliki wa basi hilo, Hamad Sudi, aligundua kuwepo kwa begi hilo
kwenye buti.
Baada ya kulikagua begi hilo, aligundua kuwa lina vipande vya meno
ya tembo 15 vyenye thamani ya sh 13,836,075 na kuamua kutoa taarifa
katika Kituo Kikuu cha Polisi.
Kwa mujibu wa kamanda, mmiliki wa begi hilo bado hajapatikana na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kuweza kumbaini.
Wakati huo huo, wakazi wawili wa Kigoma mjini wamekamatwa wakisafirisha meno ya tembo vipande 11 kutoka Mpanda kuja Kigoma.
Kamanda Kashai aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni, Gibson Azori (36),
mfanyabiashara na mkazi wa Kigoma mjini na Twaribu Yussuph (36), fundi
magari mkazi wa Mwanga Kigoma mjini.
Kashai alisema saa 11 jioni juzi, askari polisi waliokuwa doria
katika eneo la kizuizi cha Nkwanza, Kata ya Uvinza, Tarafa ya Nguruka,
walipata taarifa toka kwa raia wema kuwa kuna watu kwenye basi la
Adventure linalotoka Mpanda kwenda Kigoma walikuwa na meno ya tembo.
Askari hao baada ya kupata taarifa hizo walifanikiwa kuwakamata
watuhumiwa hao katika kizuizi hicho wakiwa na vipande hivyo 11 vya meno
ya tembo vyenye thamani ya sh 10,758,000.
Watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara upelelezi wa awali utakapokamilika.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment