Home » » PORI LA SELOUS LAWEKWA KWENYE ORODHA YA URITHI WA DUNIA ULIO HATARINI

PORI LA SELOUS LAWEKWA KWENYE ORODHA YA URITHI WA DUNIA ULIO HATARINI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri Maliasli na Utalii,Mh. Lazaro Nyalandu
 
Pori la Akiba la Selous limeingizwa katika orodha ya maeneo ya Urithi wa Dunia yaliyo hatarini. Uamuzi huu umefikiwa katika Mkutano wa 38 wa Kamati ya Urithi wa Dunia unaoendelea jijini Doha-Qatar.
Uamuzi wa kuingiza pori la Selous kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa dunia yaliyo hatarini unalenga kuongeza uelewa wa jamii kitaifa na kimataifa kuhusu matatizo yanayolikabili eneo hilo ili kuwezesha upatikanaji wa misaada ya hali na mali ili kulirejesha katika hadhi yake ya asili.

Taarifa ya msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii, imesema kuwa tangu pori la akiba la Selous lilipowekwa kwenye orodha maeneo ya Urithi wa Dunia, hali yake kwa ujumla iliendelea kuwa nzuri na ya kuridhisha.

Hata hivyo, taaarifa ilieleza kuwa kuanzia mwaka 2010 hali ya pori hilo  pamoja na maeneo mengine nchini yamekumbwa na wimbi kubwa la ujangili, hususani wa Tembo na kuwa  hali hii imesababisha kupungua kwa idadi ya tembo katika mfumo ikolojia wa Selous kutoka tembo 70,000 mwaka 2006 hadi kufikia tembo 13,084 mwaka 2013.

Ilieleza kuwa kupungua kwa idadi ya wanyama katika Pori la Selous kuliilazimu Serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti hali hii ambazo ni pamoja na kuliongezea uwezo wa rasilimali fedha kwa kurejesha utaratibu wa awali wa kubakiza asilimia 50 ya mapato; kuandaa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa kuhifadhi tembo na kuunda vikosi maalum vya pamoja miongoni mwa taasisi za wanyamapori vya kupambana na  ujangili katika kanda 11 nchini.

Pia, kuongeza idadi ya wahifadhi wanyamapori 105 ambao 40 kati yao walipangiwa eneo la kazi la Pori la akiba la Selous pamoja na usaili wa kuajiri wahifadhi wengine 437 umefanyika na kati yao 200 watapangiwa kazi katika pori la akiba la Selous.

Taarifa ilieleza kuwa Vilevile serikali iliongeza idadi ya vitendea kazi yakiwamo magari mapya nane, helikopta moja, ukarabati wa mitambo na magari, kuboresha huduma za jamii kwa watumishi pamoja na kukarabati miundo mbinu ya barabara, nyumba za watumishi na viwanja vya ndege.

Pori la akiba la Selous ni mojawapo kati ya maeneo saba yaliyo kwenye orodha ya Urithi wa Dunia nchini. Maeneo mengine ni Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Magofu ya Kilwa Kisiwani na Magofu ya Songo Mnara, Michoro ya Mimbani ya Kondoa, na Mji Mkongwe Zanzibar.

Malengo makuu na faida ya kuweka eneo kwenye orodha ya urithi wa dunia ni pamoja na kuwa na nguvu ya pamoja kimataifa ya kusimamia uhifadhi wa eneo; kujulikana kimataifa kama kivutio chenye sifa maalum cha utalii; kutumika kwa tafiti mbalimbali za uhifadhi pamoja; na kuvutia misaada ya kimataifa ya kiuhifadhi.

Kamati ya Urithi wa Dunia imeainisha vigezo 10 vinavyowezesha eneo kuorodheshwa kwenye orodha ya urithi wa dunia. Pori la akiba la Selous liliorodheshwa mwaka 1982.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa