Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KLABU
ya Azam FC imesema kuanzia sasa uwanja wao wa Azam Complex uliopo
Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam unaweza kutumika hata kwa
mechi za usiku baada ya kukamilika kwa kufungwa taa za kisasa.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu wa Klabu hiyo,
Idrissa Nassor, akisema kazi hiyo imefanywa na mafundi kutoka nchini
China waliofunga taa za kuuwezesha uwanja huo kutumika hata usiku, iwe
mechi au mazoezi.
“Sasa naweza kusema uwanja wetu upo tayari kwa kuchezwa mechi zozote
ziwe za kitaifa au kimataifa kwa nyakati za usiku baada ya zoezi la
kufunga taa za kisasa kukamilika,” alisema Nassor.
Alisema kilichobaki ni kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
kuangalia uwezekano wa baadhi ya mechi kuchezwa usiku, lakini akiongeza
kuwa hafikirii kama litawezekana kutokana na miundombinu ya nchi.
Kuhusu maandalizi ya timu kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu, Nassor
alisema wamepanga kupiga kambi nje ya nchi, lakini hilo litangoja hadi
Agosti, baada ya wachezaji wote kuripoti kwa vile ligi hiyo imesogezwa
hadi Septemba 20, badala ya Agosti 24.
“Hatuwezi kuweka kambi nje tukiwa na timu nusu, unajua kuna wachezaji
wapo timu ya taifa, Taifa Stars na nyota wa kigeni nao wakiwa katika
timu zao za taifa, hivyo tutaingia kambini baada ya kampeni ya Afcon,”
alisema kiongozi huyo.
Azam imeshaongeza nyota kadhaa wakiwemo Frank Domayo na Didier
Kavumbagu (Yanga) na Leonel Saint-Preux raia wa Haiti katika mkakati wa
kujazia maeneo yaliyopwaya kuelekea katika mbio za kutetea ubingwa wa
Ligi Kuu ya Bara na ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment