Home » » MAHARUSI WANUSURIKA KIFO ZIWA TANGANYIKA

MAHARUSI WANUSURIKA KIFO ZIWA TANGANYIKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WATU zaidi ya 64 wakazi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, wamesadikiwa kufa maji Ziwa Tanganyika baada ya mitumbwi waliokuwa wakisafiria kuzama majini kutokana na uzito uliosababishwa na kuzidisha abiria.
Akifafanua tukio hilo, Kaimu Mwenyekiti wa Wavuvi Mwalo wa Kibirizi, Sendwe Ibrahim, alisema majira ya  saa  9:00 alasiri juzi, alipewa tarifa ya kuzama kwa mitumbwi hiyo miwili.
Alisema kuwa mitumbwi iliyozama ni maalum kwa kuvulia samaki na dagaa tu, ila juzi ilikodiwa kwa ajili ya kusafirisha maharusi na wasindikizaji ambao walitoka kuoa Kijiji cha Mwandiga Kigoma Vijijini na walikuwa wakielekea Kijiji cha Kigale kwa bwana harusi ndipo wakakutwa na janga hilo.
“Mtumbwi wa kuvulia samaki hubeba abiria 20 tu, wao walikuwa zaidi ya 70, mbaya zaidi mashine hazikuwa na uwezo wa kuhimili uzito na zilikuwa mbovu, kisheria  abiria wanatakiwa kupanda maboti husika si mitumbwi,” alisema Ibrahim.
Ibrahimu, alisema awali maharusi hao na wasindikizaji walipanda mitumbwi eneo la Kijiji cha Kalalangabo ambako si rasmi kwa kupakia abiria, kwani kisheria walitakiwa waende Kibirizi kupanda boti la abiria, pia walishauriwa na wakazi wa mwambao wa ziwa kuwa wathamini maisha yao, waachane na kauli ya Mungu kapanga.
Tanzania Daima ilifika Hospitali ya Rufaa Maweni Manispaa ya Kigoma Ujiji na kuzungumza na majeruhi, Bibi harusi, Mariamu Juma (18), aliyelazwa chumba namba tano, ambaye alisema kuwa chanzo ni mitumbwi husika kukumbwa na wimbi, huku akikiri idadi kubwa ya watu takribani 80 walipanda katika mitumbwi hiyo.
“Nahisi harusi yangu ina mkosi kugharimu maisha ya wapendwa, hata sijui umri wa mume wangu Shabani Hussein, kwani yeye ni mzima na ameruhusiwa kwenda nyumbani, hata siamini kama nimenusurika, nashukuru Mungu kwa kuniokoa,”  alisema.
Baadhi ya walionusurika, Zabibu Issa na Salama Masu, kwa nyakati tofauti walikiri kupigwa na wimbi la maji, ambako mtumbwi ulishindwa kuhimili kutokana na uzito mkubwa na kudai furaha waliyokuwa nayo ya kumchukua bi harusi iliwafanya wasiwaze kama wangekutwa na dhahama hiyo.
Muuguzi wa zamu katika wodi  namba tano, Haika Masula, alisema wamepokea majeruhi 10 na maiti tatu ikiwemo ya mwanamke mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Salama Juakali na watoto walio chini ya miaka mitano wawili.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Kamishina Msaidizi (ACP), Jafari Mohamed, alisema walionusurika ni 20 ambako 11 wapo hospitali ya rufaa ya Maweni na maiti tatu zimepokelewa.
Kamanda Mohamed, aliwaonya wananchi waachane na vitu rahisi ambavyo vinagharimu uhai, kwani kimsingi mitumbwi waliyopanda haikusajiliwa na haijulikani idadi halisi wa wahanga husika, ambako wangetumia vituo mtambukwa ingekuwa rahisi kujua majina yao.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa