Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), imemtaka Rais Jakaya Kikwete kumfukuza kazi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa maelezo kuwa ameshindwa kuwachukulia hatua wahusika wa kashfa mbalimbali za ufisadi zinazoendelea kuiandama nchi na kusababisha wafadhili kusitisha misaada.
Kambi hiyo imesema kutokana na hali hiyo, inamtaka Rais Kikwete kuunda serikali upya, vinginevyo itaanza maandalizi ya kuwasilisha bungeni hoja ya kutokuwa na imani na Rais mwenyewe.
Tamko hilo lilitolewa kwa vyombo vya habari jana na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, mkoani Kigoma katika ziara yake ya kutembelea mikoa ya Kanda ya Maghribi na Kati.
Mbowe alitoa taarifa hiyo baada ya kutoa kauli mbalimbali kuhusiana na kashfa za ufisadi ukiwamo ukwapuaji wa Dola za Marekani milioni 200 (Sh. bilioni 320) kutoka akaunti ya Tegeta Escrow kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Kigoma.
Mbowe alisema hatua ya Rais Kikwete kumfukuza kazi Waziri Mkuu na kuunda upya Baraza la Mawaziri ndiyo hatua itakayokuwa suluhisho la matatizo yanayoendelea kuiandama nchi.
Alisema katika tamko hilo kwamba Baraza la Mawaziri linaonekana kushindwa kazi ya kumsaidia Rais na kwamba limeshindwa kumshauri Rais Kikwete kwenye suala la mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya nchi.
Alisema kwamba Baraza la Mawaziri lilitakiwa kumsaidia Rais ili uwe mchakato wenye kuzingatia maridhiano na mwafaka wa kitaifa.Alisema hilo halikufanyika na kusababisha nchi kuonekana imekosa uongozi wa kisiasa.
“Ufisadi unasababisha hospitali kukosa dawa, yaani hatuna fedha za kulipa deni MSD (Bohari Kuu ya Dawa) ili wananchi wapate dawa?” alihoji na kuongeza:
“Tunazo fedha tena matrilioni za kujiibia sisi wenyewe kwa sababu viongozi wanawajibika na mifuko yao zaidi. Mawaziri hao hao ndiyo wanatuhumiwa kwenye ufisadi huu,” alisema Mbowe katika taarifa yake.
Alisema kwamba huduma muhimu za msingi kwa jamii kama elimu, maji, umeme nyingine zinayumba na ni mbovu au hakuna kabisa katika maeneo mengi, lakini ufisadi umewekwa mbele.
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment