JESHI la Polisi mkoani hapa limeombwa kuwa wakali katika kusimamia
sheria za barabarani na kuepuka kupokea rushwa ili kupunguza ajali
ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa
Kigoma, David Lyamongi, ambako alibainisha kuwa ajali nyingi
zinazotokea barabarani ni kwa sababu ya uzembe wa madereva kutokufuata
sheria za barabarani.
Alisema kuwa, kosa moja linalofanyika barabarani husababisha vifo vya
watu wengi, hivyo Jeshi la Polisi halina budi kuwa wakali kwa wote
ambao hawafuati sheria, liwachukulie hatua kali itakayowafanya wajutie
makosa yao.
“Nchi jirani ya Uganda ni kosa kubwa kabisa kwa dereva au abiria
kuvunja sheria za barabarani, kwani hatua ni kali na huchukuliwa pale
pale bila kusubiri taratibu nyingine,” alisisitiza Lyamongi.
Akizungumzia ajali zinazosababishwa na pikipiki (Bodaboda), Lyamongi
alisema ni kundi ambalo sasa linakuja kasi kwa kuongoza ajali, vifo na
majeruhi, kutokana na watumiaji wa vyombo hivyo kutofuata sheria za
barabarani ikiwamo kutovaa kofia ngumu (Helmet), kwa dereva na abiria
wake.
“Kila mmoja hapa ameshashuhudia kifo au vifo ambavyo vinatokana na
ajali za pikipiki, dereva na abiria wanapoteza maisha kutokana na
kutokuvaa kofia, hivyo nawaomba madereva na abiria wote wa pikipiki
wasipuuze kuvaa kofia kabla ya kuanza safari, kwani huzuia vichwa
kuumia mara ajali inapotokea,” alisema.
Hata hivyo, Lyamongi aliwataka wananchi kutambua jukumu la kulinda
sheria za barabarani si la Jeshi la Polisi pekee, bali Watanzania wote
kuacha kufanya vitendo vinavyohatarisha maisha wanapokuwa barabarani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Usalama Barabarani mkoani hapa, Kamishna
Msaidizi (ACP), Michael Deleli, alisema kuwa ajali za barabarani
zimekuwa kero na hatari kubwa katika maendeleo ya Taifa, kwani wananchi
wengi wanapoteza maisha na wengine kubaki na ulemavu wa kudumu
kutokana na uzembe wa baadhi ya madereva.
Alisema kuwa, Jeshi la Polisi linayatumia maadhimisho haya ya wiki ya
usalama barabarani ili kufikisha ujumbe maalumu kwa watumiaji wote wa
barabara, pia kutoa elimu lengo likiwa ni kuwahamasisha na kuwakumbusha
wajibu wa kila mmoja anapokuwa barabarani ili kuepuka ajali.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment