Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Dream
Success Enterprises, waasisi wa Tuzo ya Shujaa Kati Yetu, wamewatunuku
tuzo Saed Kubenea, David Kafulila na Vick Mtetema kwa mchango wa kazi
zao zilizotukuka katika maendeleo na ujenzi wa taifa.
Kubenea, mwandishi wa habari za uchunguzi, mmiliki wa mtandao wa MwanaHALISI Online na gazeti la MwanaHALISI lililosimamishwa na serikali kwa muda usiojulikana ametunukiwa tuzo ya “Uwazi na Ukweli.”
Naye Kafulila, mbunge wa Kigoma Kusini
(NCCR – Mageuzi), ametunukiwa tuzo ya “Maono Mapevu,” huku Mtetema,
akitunukiwa tuzo ya “ubunifu.”
Mtetema ni murugenzi mtendaji wa shirika
la Under The Same Sun, linalofanya kazi za utetezi kwa watu wenye
ulemavu wa ngozi (albino).
Kafulila ametunukiwa tuzo hiyo kutokana
na kuibua na kusimamia ufisadi wa zaidi ya Sh. 300 Bilioni katika
Akaunti ya Tegeta Escrow, ndani ya Bunge la Jamhuri.
Tuzo hizo zinalenga katika kuleta mapinduzi ya kimaadili na kifikra nchini.
Akizungumza wakati akikabidhi tuzo hizo
jijini Dar es Salaam, mwasheria mkuu wa kwanza nchini, Jaji Mark Bomani,
alisema ni heshima kubwa kwake kutoa tuzo kwa Kubenea, Kafulila na
Mtetema, kutokana na machango wao mkubwa kwa taifa.
“Ni watu makini. Wanafanya kazi nzuri kwa
taifa lao. Kubenea amefanya kazi nzuri. Gazeti lake ni moja ya magazeti
yanayoandika na kusema ukweli bila kuogopa, kujipendekeza, kutoonea
wala kupendelea. Hicho ndicho kinachohitajika,” amesema Jaji Bomani.
“Kafulila ni mbunge kijana, lakini ametoa
mchango mkubwa katika kutetea rasilimali za taifa kwa kufichua maovu
yanayoendelea serikalini. Kazi ambayo inahitaji uelewa, umakini, ujasiri
na kusema kweli,” ameeleza.
Naye Mtetema, Jaji Bomani amesema,
amejitolea kutetea na kuzungumzia kwa undani suala la mauji ya Albino,
hali inayotia moyo mapambano hayo.
Amesema, “Wote ambao wamejitahidi
kufikisha ujumbe kwa wananchi, lazima wapongezwe na kupewa tuzo kwa
jitihada zao. Juhudi kubwa ifanyike kuwasaka wengine mabao wamejitahidi
kufichua maouvu ili nchi iwe ya amani.
“Tumezoea kuona watu wakitunukiwa Tunu za
taifa kila mwaka katika sherehe za Muungano au Uhuru. Hiyo haitoshi.
Hizo ni kazi za serikali. Lazima na watu nao wawe na vyombo vyao ambavyo
vinawatambua watu ambao wasingetambukika huko serikalini,” amesema.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa
tuzo, Kubenea amesema, “…nikiri kwamba nilishutuka sana nilipopata
taarifa ya kutunukiwa tuzo hii.”
Alisema, “tuzo hii, ni faraja kwangu.
Sijutii kuwa mkweli. Gazeti langu la MwanaHALISI limefungiwa na
serikali. Jingine linaweza kufungiwa kesho. Karamu yangu inaweza
kuvunjwa. Mdomo wangu unaweza kuzibwa, lakini sitanyamaza.”
Ameifananisha jina la tuzo hiyo la “Uwazi
na Ukweli” na kauli ya serikali ya awamu ya tatu ambayo amesema,
“…baadae iligeuka na kuficha ukweli na kukumbatia usiri.”
“Nyumba zote za serikali zimeuzwa katika
kipindi ambacho serikali hii, ilikuwa madarakani. Mgodi wa Kiwila,
nyumba za serikali kwa wasiostahaili na kwa bei ya kutupwa, mashamba ya
mkonge, ufisadi katika Benki Kuu ya Tanzania na Benki (NBC).
Kwa upande wake Kafulila amesema,
“…nimejisikia fahari kubwa kuwa miongoni mwa watu ambao wamechangia
chochote katika taifa letu, hata kupewa tuzo hii. Nikifa kesho duniani
wanangu, wajukuu, ndugu zangu na watu wengine watanikumbuka kwamba
nilifanya chochote.”
Naye Kafulila amesema, “taifa letu lina
tatizo kubwa la watu kukosa uadilifu na kujaa uoga. Hii inatokana na
ukosefu wa bidii na maarifa….nachoweza kuwaahidi watu, nitaendelea
kuwatumikia. Nakwenda kugombea tena. Nikishidwa, nikishinda sitoacha
kutumikia nchi yangu.”
Kwa upande wake, Vicky Mtetema amesema,
“….ni heshima kubwa kutunukiwa hii tuzo. Vitendo vya albino kuuwawa
vinakithiri wakati huu wa uchaguzi. Naomba nimteue David Kafulila awe
baba na kuwasemea watu wenye albinism bungeni,”
Mtetema amemtaka Kafulila kama
atafanikiwa kuchaguliwa katika Bunge la 11 kuhakikisha kunakuwepo na
sera ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), Sheria ya kuwaondoa
wanganga wanaopiga ramli na mazingira mazuri kwa Albino.
Joshua Lawrence, afisa mikakati toka
Dream Success Enterprises amesema maendeleo ya taifa lolote duniani
hutengenezwa na raia na viongozi wenye habari, maarifa na maono sahihi.
Na ili kufanikisha hayo, uhuru wa kupata habari ndani ya muktadha ni
muhimu kuwepo.
“Na, hili linawezekana tu pale raia
wanaopewa uhuru wa kuogelea ndani ya bahari ya fikra huru, huku muktadha
wa sheria zinazolinda kingo za uhuru huo ukiwa ni kuzinawilisha fikra
pevu na kuzinyong’onyeza fikra bwete, wala si vinginevyo,” amesema
Lawrence.
Amesema hiyo ni awamu ya pili tuzo hizo
kutolewa. Awamu ya kwanza ilikuwa 22 Disemba, mwaka 2014 ambapo Mdhibiti
na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh
alitunukiwa.
Chanzo:Mwanahalisi
0 comments:
Post a Comment