Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Zitto Kabwe.
Kufuatia hatua hiyo, Prof. Kitila ameandika katika mtandao wa
kijamii kuwa hajaandaliwa kisaikolojia kupeperusha bendera ya chama
hicho katika nafasi ya urais na jukumu hilo wapewe viongozi wengine
waandamizi.
Tofauti na ilivyozoeleka kwa wagombea kwenda na wafuasi wao Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuchukua fomu za kugombea urais, kwa upande wa
ACT – Wazalendo, Katibu Mkuu, Samson Mwigamba, jana alikwenda Nec
kumchukulia fomu Prof. Kitila ambaye inadaiwa viongozi wakuu wa chama
hicho wamekutana naye kwa mazungumzo ya kumshawishi akubali kupeperusha
bendera ya chama hicho kuelekea Ikulu.
Mapema asubuhi jana Prof. Kitila alifika ofisi za chama hicho
Kijitonyama na kuondoka na majira ya saa 5:00 asubuhi wafuasi zaidi ya
100 wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali walivamia ofisi hiyo na
kumbana Mwigamba kuwaeleza kwanini chama hicho kinachelewa kuweka wazi
mchakato wa mgombea wake wa urais.
Habari zinasema kuwa licha ya Prof. Kitila kutokuwapo kwenye kikao
cha Kamati Kuu (CC) kilichopitisha uamuzi wa kumtaka apeperushe bendera
ya chama hicho katika nafasi ya urais, lakini ulipitishwa uamuzi wa
kwamba abebe jukumu hilo zito.
Wakati Kamati Kuu kiamua hivyo, hadi jana alasiri hapakuwapo na
makubaliano na Prof. Kitila, lakini viongozi wakuu wa chama walikuwa
kwenye mazungumzo naye.
Akizungumza na Nipashe jana, Mwigamba alisema alichukua fomu hiyo
saa 4:00 asubuhi, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Kamati Kuu
iliyokutana Agosti 15, mwaka huu.
Alisema pamoja na azimio hilo, Kamati Kuu ilipitisha majina ya
wagombea ubunge nchi nzima, wagombea udiwani na kupokea ripoti ya
wataalamu washauri juu ya ushiriki katika harakati za uchaguzi wa rais.
“Baada ya kupokea taarifa na mapendekezo yao tukajiridhisha kwa
mustakabali wa taifa, chama kinahitaji kusimamisha mgombea urais, ndipo
nilipoagizwa kwenda kuchukua kwa sababu muda unaenda zianze kujazwa ili
Ijumaa ambayo ndiyo siku ya mwisho zirudishwe,” alisema Mwigamba.
Alisema Kamati Kuu imeamua hivyo kwa kuwa Prof. Kitila ni
mwadilifu, mzalendo wa kweli, anaweka mbele maslahi ya Taifa na kwamba
ana sifa zote za kuliongoza taifa na mgombea mwenza atakuwa ni Mwandishi
wa habari mkongwe, Hawra Shamte.
Hata hivyo, Hawra, alipoulizwa kuhusu maamuzi hayo ya Kamati Kuu,
alisema hana taarifa zozote na kwamba hadi jana jioni hakuarifiwa
chochote.
Alisema wakati mgombea huyo anakutana na viongozi wakuu wa chama
hicho, fomu hiyo itaendelea kusambazwa mikoani ili kusaka wadhamini na
kwamba walianza kufanya hivyo jana.
“Tofauti yetu na wengine hatutakuwa na ziara kwenye kusaka
wadhamini, nimeenda na wanachama wengine watatu kuchukua fomu na sikuwa
na msururu wa watu na hivyo hivyo kwenye kusaka wadhamini itakuwa kimya
kimya,” alisema Mwigamba.
Alipoulizwa juu ya utayari wa Prof. Kitila kupeperusha bendera
hiyo, alisema: “Hatuna wasiwasi, tunaamini atakubali uamuzi wa Kamati
Kuu, anajua ni wajibu kubeba jukumu chama kinapomuhitaji.”
Aidha, Mwigamba alisema kama itashindikana kwa Prof. Kitila, ni
lazima chama hicho kisimamishe mgombea mwingine katika nafasi hiyo.
KITILA: SINA MAANDALIZI
Katika kundi la mtandao wa kijamii la chama hicho la Whatsaap,
lijulikanalo kama ACT Taasisi Imara, Prof. Kitila aliandika taarifa ya
kuwashukuru wanachama na viongozi kwa imani yao kwake, lakini alisema
hawezi kubeba jukumu hilo.
“Naomba niwashukuru nyote kwa imani kubwa mliyonayo juu yangu
katika kukiwakilisha chama katika nafasi ya urais, naishukuru Kamati Kuu
kwa imani yake kwangu hata kufikia hatua ya kupitisha azimio la
kuniomba kugombea urais kwa chama chetu. Jana CC (Kamati Kuu) ilituma
ujumbe maalum nyumbani kwangu kwa ajili ya kuzungumza na familia na
jamaa zangu juu ya ombi hilo,” alisema katika andiko hilo na kuongeza:
“Nimekuwa nikitafakari tangu Alhamisi nilipoombwa rasmi kutafakari
uwezekano wa mimi kugombea baada ya juhudi zetu za kutafuta mgombea
kushindikana. Nimefanya mawasiliano mapana ndani ya familia, chama,
chuoni ninapofanyia kazi, kanisani kwangu na kwa watu na taasisi
mbalimbali ninazohusiana nazo.”
Alisema baada ya tafakari na mawasiliano mapana (consultations),
ameona hana utayari na maandalizi ya maana ya kisaikolojia, kifamilia na
kisiasa kumuwezesha kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao.
“Najua nimewaangusha sana katika uamuzi wangu huu, lakini naamini
kwamba mtaheshimu uamuzi wangu na kwamba hamtaacha kuthamini mchango
wangu katika chama kwa sababu ya kukataa kugombea urais,” alisema na
kuongeza:
“Nasikitika kwa tuhuma ambazo baadhi ya wanachama wetu wanarusha
katika mitandao ya kijamii na sehemu nyingine. Nathamini na kuheshimu
haki ya wanachama kuonyesha hasira kwa jambo wasilolipenda…nawasihi
wanachama wajizuie kuzusha mambo yatakayochochea chuki ndani ya chama na
kukatishana tamaa.”
Aidha, alishauri wanachama wengine waandamizi waombwe wachukue
jukumu hilo na kuwataja kuwa ni Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo na Katibu
Mkuu, Mwigamba na kwamba wakati hayo yakitafakariwa wasisahau malengo
mapana ya chama waliyojiwekea katika uchaguzi huo.
Alisema mafanikio waliyofikia ni kuweka wagombea ubunge na udiwani kata na majimbo mengi nchini.
Mwigamba alipoulizwa juu ya taarifa hiyo, alijibu: “Sina simu ya
whatsaap ila naenda kwenye kikao hadi leo (kesho) nitawapa taarifa.”
WAFUASI WAKUSANYIKA
Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na wanachama na wafuasi wa
ACT-Wazalendo yalikuwa na ujumbe wa ‘wamenunuliwa’ na mgombea wa
Chadema, Edward Lowassa ili wasisimamishe mgombea urais.
Wafuasi hao walikaa kwa saa nne nje ya ofisi hizo wakiimba nyimbo mbalimbali.
Mabango mengine yalisomeka: “Viongozi hatuwaelewi mmekaa muda
mrefu bila kutuambia mgombea urais ni nani wakati muda unaisha, kama
hamsimamishi mgombea ni bora mfunge ofisi, tusijihusishe tena na siasa,
liko wapi azimio la Tabora?”
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment