Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KUFUNGULIWA vyumba vya upasuaji katika vituo vya afya zaidi ya 15
mkoani Kigoma na kupatiwa vifaa mbalimbali kwenye vituo hivyo kumeanza
kutimiza lengo la mkoa huo kupunguza vifo vya wajawazito na watoto
wakati wa kujifungua.
Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma, Dk Fadhili Kibaya, alisema hayo
wakati wa kupokea seti 10 za Ombwe (Vacuum Extraction) zenye thamani ya
Sh milioni 34.5 zilizotolewa na Shirika la World Lung Foundation
zinazosaidia mjamzito mwenye matatizo kujifungua bila kufanyiwa
upasuaji.
Dk Kibaya alisema kuwa, tangu kuanza kuboresha kwa vituo hivyo vya
afya katika kipindi cha miaka minne iliyopita, wajawazito 18,281
wamejifungulia kwenye vituo hivyo na kati yao 1613 wamefanyiwa upasuaji.
Alisema, kuongezeka kwa wajawazito kujifungulia katika vituo rasmi
vya utoaji huduma kumewezesha kupunguza vifo vyao kutoka 49 mwaka 2014
na kufikia vifo 39 mwaka jana.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa mkoa huu, John Ndunguru,
alilishukuru shirika la World Lung Foundation, kwa programu yake ya
kuboresha vituo vya utoaji huduma mkoani humu, ambayo imesaidia katika
kutekeleza mipango ya serikali na malengo ya milenia katika kupunguza
vifo vya wajawazito na watoto wakati wa kujifungua.
Hata hivyo, alisema kuwa ujio na ongezeko kubwa la wakimbizi
vimefanya baadhi ya huduma ambazo zilizapangwa kwa Watanzania katika
huduma za afya kuelekezwa kwa wakimbizi na ameomba serikali ya Burundi
kudumisha amani nchini mwao ili kupunguza wimbi la wakimbizi nchini.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la World Lung Foundation, Dk Nguke
Mwakatundu alisema kuwa licha ya kufunguliwa kwa vyumba vya upasuaji
katika vituo mbalimbali vya afya mkoani humo, kukabidhiwa kwa vifaa
hivyo kutawezesha wajawazito wenye matatizo kujifungua kwa kutumia vifaa
hivyo badala ya kufanyiwa upasuaji.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment