Home » » MAADHIMISHO YA SIKU YA MAKAZI DUNIANI

MAADHIMISHO YA SIKU YA MAKAZI DUNIANI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itajumuika na Ulimwengu wote kuadhimisha Siku ya Makazi Duniani, tarehe 02 Oktoba, 2017 – Karimjee Hall, ambapo Wadau mbalimbali wanategemewa kujumuika katika hafla hiyo, itakayoambatana na Maonyesho. 

Siku ya Makazi Duniani huadhimishwa duniani kote kila Jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba. Lengo kuu la maadhimisho haya ni kutoa mwongozo kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutafakari kwa pamoja masuala yanayohusu makazi ulimwenguni kwa kuangalia changamoto mbalimbali zilizopo na kushirikishana mbinu na mikakati ya kupambana nazo. 

Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Makazi Duniani – UN-HABITAT hutoa mwongozo kupitia kauli mbiu ambayo huongoza tafakari hiyo duniani kote. Mwaka huu maadhimisho hayo, ambayo ni ya 32 yanafanyika kwa kuongozwa na Kauli Mbiu isemayo “Housing Policies”: Affordable Homes: Tafsiri ya kauli mbiu hiyo ni “Sera za Nyumba: Nyumba za Gharama Nafuu: Kauli mbiu hii inaelekeza kutafakari namna tunavyoweza kutunga Sera za Nyumba katika nchi zetu zinazojielekeza kutatua changamoto ya upatikanaji wa nyumba, hususan za gharama nafuu ili kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini waweze kumudu kujenga, kununua ama kupanga. 

Madhumuni ya Maadhimisho ya Siku ya Makazi kufuatana na kauli mbiu ya mwaka huu Oktoba, 2017 ni kuhakikisha kuwa Sera zetu za Nyumba na Makazi zinazingatia yafuatayo: 

· Kuwa na Nyumba na Makazi bora yenye huduma za msingi za jamii toshelezi (Inclusive housing and social services),

· Kuwa na mazingira salama ya kuishi kwa wananchi wote, hususan wenye mahitaji maalum wakiwemo watoto, vijana, wanawake, wazee na wenye ulemavu (A safe and healthy living environment for all — with particular consideration for children, youth, women, elderly and disabled),

· Upatikanaji wa usafiri na nishati endelevu zenye gharama nafuu (Affordable and sustainable transport and energy),

· Kukuza, kulinda na kuhifadhi maeneo ya wazi mijini (Promotion, protection, and restoration of green urban spaces),

· Upatikanaji wa maji safi na salama ya kunywa na mfumo thabiti wa uondoshaji majitaka (Safe and clean drinking water and sanitation),

· Uwepo wa hewa safi na ya kutosha (Healthy air quality),

· Kuwepo fursa za ajira (Job creation) ,

· Kuimarisha upangaji miji na kuboresha makazi duni (Improved urban planning and slum upgrading),

· Kuwepo na mfumo thabiti wa usimamizi wa taka (Better waste management)

Kaulimbiu iliyotolewa kwa mwaka huu, pia inahimiza nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutumia ngazi zote za Serikali pamoja na wadau wote muhimu kutafakari nanma ya kuibua mikakati ya kuwezesha uwepo wa nyumba bora na za gharama nafuu katika nchi zao ikiwa ni utekelezaji wa mojawapo ya Agenda Mpya ya Makazi Duniani iliyoidhinishwa Quito, Oktoba, 2016 na Malengo Endelevu ya Milenia. 

Chimbuko la maadhimisho hayo ni Azimio Namba 40/202 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa mwezi Desemba mwaka 1985 na kuanza kuadhimishwa rasmi mwaka 1986. 

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa