Home » » CHADEMA: TUUNGANISHE NGUVU KUING’OA CCM 2015

CHADEMA: TUUNGANISHE NGUVU KUING’OA CCM 2015

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mkoa wa Kigoma, kimevitaka vyama vya upinzani mkoani humo, kuacha malumbano, matusi na kashifa badala yake waunganishe nguvu zao ili kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinang’oka madarakani katika Uchaguzi Mkuu 2015.

Mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, Bw. Ally Kisala, aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Mwanga Community Center, Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Bw. Kisala ambaye ni mwenyekiti wa muda, alisema kuanzishwa kwa chama kipya cha Alliance Transparency For Change (ACT), si sababu ya kuanza kutupiana matusi na lugha za kashifa kwa chama kingine cha upinzani.

Alisema adui mkubwa wa vyama vya upinzani nchini ni CCM; hivyo lazima vyama vya upinzani viunganishe nguvu zao ili kuking’oa chama tawala madarakani.

Kwa upande wake, Katibu wa chama hicho mkoani humo, Rafael Madede, alisema CHADEMA kimeanza harakati za kuhakikisha majimbo yaliyokwenda CCM yanarudi kwa chama chao.

Alisema kuhama kwa waliokuwa viongozi wa chama hicho Wilaya na Mkoa ni njia mojawapo ya kupokezana vijiti na wengine ili waweze kusimamia, kukiongoza chama kwa kuzingatia matakwa ya Katiba.

Bw. Omar Gindi ambaye ni Mratibu wa Vijana wa CHADEMA Mkoa, alishangazwa na watu ambao hawakuziona jitihada zao za kuukomboa mkoa huo na leo hii wanakimbia wakati chama kinakaribia kuingia Ikulu ili kushika dola na kuunda Serikali.

Alisema miradi iliyotekelezwa mkoani humo ni kutokana kelele zilizopigwa na vyama vya upinzani kwani ulikuwa umesahaulika kimaendeleo; hivyo wataendelea kufanya mageuzi ya kweli kwa njia ya amani badala ya kumwaga damu na kusababisha vurugu.

Mkurugenzi wa Mipango na Mafunzo Taifa wa chama hicho, Bw. Benson Kigaila, alitoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kukiunga mkono chama hicho ambapo viongozi wao wana kila sababu ya kuujali Mkoa wa Kigoma ambao umekuwa kinara wa kufanya mageuzi baada ya kuingia kwa vyama vingi nchini

Chanzo;Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa