Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
CHAMA cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Mkoa wa Kigoma, kimevitaka vyama vya upinzani
mkoani humo, kuacha malumbano, matusi na kashifa badala yake waunganishe
nguvu zao ili kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinang’oka
madarakani katika Uchaguzi Mkuu 2015.
Mwenyekiti wa chama
hicho mkoani humo, Bw. Ally Kisala, aliyasema hayo juzi kwenye mkutano
wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Mwanga Community Center,
Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Bw. Kisala ambaye ni
mwenyekiti wa muda, alisema kuanzishwa kwa chama kipya cha Alliance
Transparency For Change (ACT), si sababu ya kuanza kutupiana matusi na
lugha za kashifa kwa chama kingine cha upinzani.
Alisema adui mkubwa wa
vyama vya upinzani nchini ni CCM; hivyo lazima vyama vya upinzani
viunganishe nguvu zao ili kuking’oa chama tawala madarakani.
Kwa upande wake, Katibu
wa chama hicho mkoani humo, Rafael Madede, alisema CHADEMA kimeanza
harakati za kuhakikisha majimbo yaliyokwenda CCM yanarudi kwa chama
chao.
Alisema kuhama kwa
waliokuwa viongozi wa chama hicho Wilaya na Mkoa ni njia mojawapo ya
kupokezana vijiti na wengine ili waweze kusimamia, kukiongoza chama kwa
kuzingatia matakwa ya Katiba.
Bw. Omar Gindi ambaye
ni Mratibu wa Vijana wa CHADEMA Mkoa, alishangazwa na watu ambao
hawakuziona jitihada zao za kuukomboa mkoa huo na leo hii wanakimbia
wakati chama kinakaribia kuingia Ikulu ili kushika dola na kuunda
Serikali.
Alisema miradi
iliyotekelezwa mkoani humo ni kutokana kelele zilizopigwa na vyama vya
upinzani kwani ulikuwa umesahaulika kimaendeleo; hivyo wataendelea
kufanya mageuzi ya kweli kwa njia ya amani badala ya kumwaga damu na
kusababisha vurugu.
Mkurugenzi wa Mipango
na Mafunzo Taifa wa chama hicho, Bw. Benson Kigaila, alitoa wito kwa
wakazi wa mkoa huo kukiunga mkono chama hicho ambapo viongozi wao wana
kila sababu ya kuujali Mkoa wa Kigoma ambao umekuwa kinara wa kufanya
mageuzi baada ya kuingia kwa vyama vingi nchini
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment