JESHI la Polisi linamshikilia Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila kwa tuhuma za uchochezi, akiwataka wananchi wasichangie ujenzi wa maabara katika shule za sekondari nchini.
Kafulila alikamatwa mapema jana asubuhi katika mji mdogo wa Nguruka wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, ambako alikuwa akifanya mikutano ya hadhara, kuelezea sakata la uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Escrow na kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Jafari Mohammed amethibitisha kukamatwa kwa mbunge huyo, ambaye anahojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Kigoma.
Kamanda huyo alisema Kafulila alikamatwa jana asubuhi na askari polisi na kusafirishwa hadi mjini Kigoma, ambako anahojiwa kuhusu matamko ya uchochezi aliyokuwa akitoa kwenye mikutano yake ya hadhara.
Alisema katika mikutano yake, Kafulila aliwataka wananchi kutochangia kwa namna yOyote ujenzi wa maabara katika shule za sekondari na kwamba viongozi watakaokuwa wakifika kwenye maeneo yao kuhamasisha michango na ujenzi wa maabara hizo, wawapige mawe.
“Alichokuwa akifanya Mbunge Kafulila kwa kweli tumeona ni uchochezi na kinaweza kusababisha kuvurugika kwa amani na hivyo tumemkamata tunamshikilia hapa kituo kikuu mjini Kigoma, anahojiwa na maafisa wa juu wa upelelezi wa mkoa,” alisema Kamanda huyo.
Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari, Kamanda Mohammed alisema kwa leo (jana) hawakuwa na maelezo ya ziada ya hatua gani watachukua na kwamba baada ya mahojiano jana, leo wanatarajia kutoa taarifa ni hatua gani zitachukuliwa dhidi yake.
Kafulila aliwasili mkoani Kigoma Jumamosi Desemba 6 mwaka huu, ambapo alihutubia mkutano wake wa kwanza katika uwanja wa Community Centre Mwanga mjini Kigoma kabla ya kuendelea na ziara katika vijiji mbalimbali vya wilaya ya Uvinza.
Katika mikutano yake, Mbunge huyo alikuwa akitumia muda wake mwingi kuelezea sakata la uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, huku akitoa shinikizo kwa serikali kutekeleza maazimio manane yaliyotolewa na bunge kuhusu sakata hilo.
Chanzo;Habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment