Saa zinahesabika kuukaribisha mwaka mpya wa 2015. Ninaungana na
vijana wenzangu katika kudumisha amani katika kipindi chote cha sikukuu
ili tuweze kusherehekea kwa amani.
Mengi tumeyajadili kwa kipindi chote cha mwaka huu
kwa kushirikiana na Mwalimu Athuman Hayeshi pamoja na mhariri wa makala
za elimu, Abeid Poyo kwa lengo la kuwapa maarifa wanafunzi kwa namna
hii gazetini.
Ninaamini maarifa tuliyokuwa tunayatoa hapa
yamewanufaisha wanafunzi na wapenzi wasomaji wa gazeti hili. Pongezi
nyingi tunazirudisha kwenu mliochangia mada mbalimbalia ambazo
zilijadiliwa hapa.
Wanafunzi walio katika madarasa ya mitihani
wanapaswa kujiwekea malengo yao kuanzia sasa. Watakaoingia kidato cha
pili watambue kwamba masomo yatakapoanza muda wa kusoma ni sasa. Tabia
ya kusoma karibu na mtihani inapaswa kuachwa kwani haiwezi kumsaidia
mwanafunzi kama wengi wao wanavyofikiri.
Wanafunzi wanaoingia kidato cha nne wafikirie
zaidi kwamba wana muda mfupi kutokana na mwaka 2015 kuwa na hekaheka
nyingi ukianza na kura ya maoni, kampeni za uchaguzi, uandikishaji wa
daftari la kupika kura japokuwa haviwezi kuwaathiri katika masomo yao
lakini jambo la kuzingata kwamba wana muda mfupi.
Kwa mwanafunzi ambaye ana kiu ya kusonga mbele
iwapo amepata wastani asioridhishwa nao, ni kukaa chini na kutafakari
kwa kina tatizo lipo wapi. Unaweza kujiuliza iwapo tatizo ni wewe
mwenyewe, je, uweke mikakati gani ili uweze kupiga hatua katika mitihani
ya robo muhula, nusu muhula na ile ya majaribio.
Ratiba ya kujisomea ni jambo la msingi kwa mwanafunzi yeyote. Kila mwanafunzi anafahamu uwezo wake.
Jambo lingine la msingi la kukumbushana kwa
wanafunzi wote, muda ambao mwalimu hayupo darasani siyo muda wa kupiga
soga na kuhadithiana masuala ya mitandaoni au habari zisizo na manufaa
kwako, tumia muda wako vizuri kwa kujisomea.
Kwa mwanafunzi yeyote kusoma isiwe sababu ya
kutoshirikiana na wazazi katika kazi nyingine za nyumbani. Mtoto mwenye
tabia njema anapanga vyema ratiba yake ya shule pia anashirikiana na
familia yake katika kazi zile anazomudu.
Suala la matumizi ya simu au mitandao inaweza
ikawa kikwazo kwa mwanafunzi ambaye hatakuwa msikivu kwa wazazi au
walimu kuhusu kuacha matumizi yasiyofaa. Jiwekee utaratibu wako mwenyewe
hasa kujidhibiti katika matumizi ya simu na mitandao ya kijamii isiyo
na manufaa kwako.
Ifaye simu yako na intaneti kama sehemu ya kukuongezea maarifa kitaaluma siyo vinginevyo.
Epuka makundi yasiyofaa. Mzazi anaweza kukushauri
kuhusu marafiki wa kuwa nao kwa manufaa yako ya baadaye. Siyo kila
rafiki anaweza kukufaa kwani wengine wana mawazo ambayo baadaye unaweza
kujikuta unakwama katika masomo yako kutokana na kuchagua marafiki wenye
ushauri mbaya.
Ni vyema kila mwanafunzi atambue kwamba hatima ya mafanikio yake
ipo mikononi mwake mwenyewe. Malengo na mipango yako mizuri katika
mwaka ujao ndiyo mafanikio yako katika elimu.
Jizatiti, pale ambapo ulilegalega mwaka 2014
rekebisha makosa ya utoro, uvivu wa kuamka mapema, kutofanya mazoezi ya
darasani kwa wakati. Pia futa kauli kwamba ‘nitasoma kesho’ kwani
Waswahili wanasema linalowezekana leo lisingoje kesho
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment