BAADHI ya makada
wakongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamesema watamkataa mgombea yeyote
wa urais atakayeonekana kubebwa au kupata upendeleo kwa baadhi ya
vigogo au kundi lolote kwa maslahi binafsi.
Kutokana na mchuano
unaotarajiwa kuwepo kwenye kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM baadaye
mwaka huu, baadhi ya makada wa chama hicho wamehofu kukiukwa baadhi ya
taratibu na kanuni ili kupitisha mgombea kwa ujanja ujanja na kubebana.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti na gazeti hili, makada hao Wamedai kutokana na mazingira
yalivyo kuna kila dalili kuwa baadhi ya watu kutumia nafasi zao au
kujuana kuhakikisha baadhi ya watu wanaibuka washindi kwenye mchuano
huo.
"Tayari kuna tetesi
kwamba familia yenye nguvu na ushawishi kisiasa hapa nchini, inadaiwa
kusuka mpango kabambe kuhakikisha jina la mmoja wa vigogo wanaotajwa
kuchuana kwenye nafasi hiyo linapenya na kuungwa mkono ndani ya vikao
vya CCM hatimaye ‘mtu wao’ ateuliwe na CCM kugombea urais na hatimaye
kurithi nafasi ya Rais wa sasa Jakaya Kikwete, atakapomaliza muda wake
kikatiba Oktoba mwaka huu," alisema mmoja wa makada hao kwa sharti la
jina lake kutochapishwa gazetini.
Alisema zipo taarifa
kuwa familia hiyo sasa inafanya kila linalowezekana ikiwa ni pamoja na
kusaidia kusaka pesa ndani na nje ya nchi ili kumsaidia kada huyo pindi
kipenga cha mbio za urais ndani ya CCM kitakapopulizwa siku za karibuni.
Tayari vigogo wa CCM
katika baadhi ya mikoa, wakiwemo wenyeviti, wamethibitisha kudokezwa
suala hilo na kushawishiwa kuachana na wanachama wengine wenye nia ya
kutaka nafasi hiyo, badala yake wasimame kumuunga mkono kigogo huyo,
kinyume na hapo watakuwa wanapoteza muda wao kwani wengine hawana baraka
zake.
Kigogo mmoja wa CCM kutoka Kanda ya Ziwa mapema wiki hii aliweka wazi suala hilo, huku akiwataka wagombea wengine kutopoteza.
“Mimi nawaheshimu sana
watu wote wanaotajwa tajwa kugombea urais, lakini sina namna kwani
tumeambiwa kuendelea kuwaunga mkono ni kupoteza muda. Familia ya
(anataja) inamtaka (anataja). Tunamuunga mkono huyu kwani ndiye mwenye
baraka hizo,” alikaririwa akisema kada huyo.
Taarifa za uhakika
ambazo gazeti hili linazo, zinaeleza kuwa tayari mikakati kabambe
inafanyika usiku na mchana kuhakikisha jina na sifa za kada huyo
zinamwagwa kila kona nchini, huku mipango mingine ikisukwa kuhakikisha
anapitishwa na vikao vya chama.
Akizungumza na gazeti
hili kwa sharti la kuhifadhiwa jina, kigogo mwingine wa CCM Kanda ya
Ziwa, alipinga vikali hatua hiyo na kuonya kuwa CCM itafanya makosa
makubwa endapo itatoa mwanya kupata mgombea kwa shinikizo la kundi au
mtu kwa maslahi binafsi, matokeo yake yatakigharimu chama hicho.
Alisema katika historia
yake, CCM kimekuwa chama cha umma na viongozi wake wanapatikana
kidemokrasia ambapo huungwa mkono na wanachama wote na kamwe hawatokani
na sababu za urafiki au familia.
Alionya kuwa endapo
suala hilo litabainika haitakuwa ajabu mgombea huyo wa kukataliwa vibaya
na wana CCM jambo litakalokuwa aibu kwa pande zote mgombea huyo.
“Tuwaache wanachama
waamue wanamtaka nani, kama ni kushindana uwepo ushindani sawa mwisho wa
siku tupate mgombea anayekubalika na wengi, hapo tutashinda, kinyume na
hapo itakuwa aibu, chama kitaparaganyika hata kuwapa mwanya wapinzani
kuongoza dola.
Kama kuna watu au mtu
anayejiona anaweza kutengeneza rais wake kwa sababua anazozijua yeye,
anajidanganya, hiyo ni ndoto ya mchana kwa CCM ya leo, demokrasia ndani
ya CCM ya leo ni kubwa, inatisha. CCM ya leo watu wasema ‘hapana’ tena
mchana kweupe bila kumwonea mtu haya. Hatutakubali kamwe genge la watu
au familia kuteka nyara nguvu ya chama kuteua mgombea wake,” alisema
kada huyo.
Aliongeza kwamba CCM
ina hazina kubwa ya viongozi hivyo hakuna sababu suala la uteuzi wa jina
la mgombea urais kutekwa nyara na kundi au familia fulani, wanaotaka
nafasi hiyo waachiwe wapambane kwa usawa vinginevyo atakayekuja kwa
kubebwa atakataliwa.
“Sisi tunasubiri, haya
mambo hayana siri, wakati ukifika yatakuwa wazi, kama kuna aliyebebwa na
chama kimeporwa nguvu ya kutafuta mgombea wake.
Tutajipanga na
kumkataa. Tutawakataa wagombea wote tutakaobaini wamebebwa. Tutawakataa
ili kuwaonesha kuwa chama hakiburuzwi kupata mgombea wake," alisema.
Chanzo:Majira
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment