Tungo ni neno au kikundi cha maneno ambacho hudokeza taarifa fulani ambayo huweza kuwa kamili au isiyo kamili.
Tungo hujengwa na vipashio vidogovidogo kama vile
mofimu, kirai, sentensi. Msingi wa tungo huanzia katika neno. Tungo neno
huundwa na vipashio vidogo zaidi ya neno ambavyo ni mofimu au fonimu.
Mfano a-na-kimb-i-a.
Tungo kirai ni kipashio cha kimuundo chenye neno
moja au zaidi lakini kisicho na muundo wa kiima - kiarifu. Mfano; Kijana
mtanashati, kitoto kichanga.
Kirai huwa ni kipashio cha kimuundo
kisichokamilika; yaani ni kipashio kisichokuwa na muundo wa kiima –
kiarifu kama zilivyo sentensi ambazo zinahusisha mtendaji wa tendo na
tendo linalotendwa. Pia, kirai huainishwa kimuundo kulingana na neno kuu
la kirai husika.
Kirai ni tungo, yaani ni aina mojawapo ya tungo, aina nyingine za tungo ni neno, kishazi na sentensi.
Kirai huweza kutokea upande wowote wa kiima au kiarifu katika sentensi.
Aina za virai ni kama ifuatavyo; Kirai nomino
(KN), chenyewe neno lake kuu ni nomino. Ni kirai ambacho muundo wake
umekitwa kwenye nomino.
Kirai kitenzi (KT) ni kirai ambacho kimekitwa katika kitenzi au katika uhusiano wa kitenzi na neno au mafungu mengine ya maneno.
Kirai kivumishi (KV) muundo wake umekitwa katika kivumishi. Kwa kawaida muundo huu huwa ni wa kivumishi na neno.
Kirai Kielezi (KE) haielekei kukitwa kwenye
uhusiano wa lazima baina ya neno kuu la Kielezi isipokuwa miuundo
inayohusika hapa ni ya maneno ambayo hufanya kazi pamoja katika lugha
kama misemo, neno au maneno yanayofuata neno lililotangulia yakifafanua
zaidi neno hilo.
Virai viunganishi (KV) muundo wake umekitwa katika uhusiano na neno kuu la kwanza ambalo huwa kivumishi.
Mathalan, kishazi ni tungo yenye kitenzi ambacho
chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji
au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea chenyewe.
Namna ya kubaini vishazi; Kishazi hupatikana katikaa au ndani ya
sentensi. Lazima kishazi kiwe na kitenzi, sehemu yoyote ya sentensi
isiyo na kitenzi, haiwezi kuwa kishazi. Kishazi huru hutawaliwa na
kishazi kikuu na kishazi tegemezi hutawaliwa na kishazi tegemezi.
Baadhi ya vishazi huweza kujitegemea kama sentensi
hata vikiondoshwa katika muktadha wa sentensi kuu. Kishazi kinachoweza
kujisimamia kama sentensi huitwa kishazi huru kikiwa ndani ya sentensi
kuu na huitwa “sentensi sahili” kikiwa sentensi inayojitegemea.
Kishazi kwa kawaida, hasa kishazi huru huwa na
kitenzi kimoja kikuu. Kitenzi hicho huweza kuandamana na kitenzi
kisaidizi. Pia, kitenzi katika kishazi huweza kuwa kitenzi kishirikishi.
Tofauti ya kishazi na sentensi ni kwamba kishazi
hupatikana ndani ya sentensi lakini sentensi hujisimamia kimuundo na
kimaana. Kishazi huwa na kiarifu kimoja na kiima kimoja, lakini sentensi
huweza kuwa na kiima kimoja.
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment