Home » » SILAHA TATU ZA KIVITA ZASALIMISHWA KIGOMA

SILAHA TATU ZA KIVITA ZASALIMISHWA KIGOMA

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma,SSP Kihenya wa Kihenya akionyesha silaha zilizosalimishwa na Mkazi mmoja wa Kijiji cha Nyankwi kilichopo katika Kata ya Busunzu Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma alietambulika kwa jina la Tora Muhoza (42).

NA Pardon Mbwate na Felister Elias, wa Jeshi la Polisi Kigoma


Mkazi mmoja wa Kijiji cha Nyankwi kilichopo katika Kata ya Busunzu Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma Bw. Tora Muhoza(42), amesalimisha silaha moja ya kivita aina ya SMG ikiwa na sirasi mbili kwenye magazine yake.

Silaha hiyo yenye namba BA 178645 ilisalimishwa kwa Mtendaji wa Kata ya Busunzu na baadaye kukabidhiwa kwa Jeshi la Polisi.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma SSP Kihenya wa Kihenya, amesema kuwa kusalimishwa kwa silaha hiyo kunatokana na msako mkali unaoendeshwa na Jeshi hilo baada ya muda uliotolewa na serikali wa kusalimisha silaha kumalizika.

Kamanda Kihenya amesema kuwa pamoja na kumalizika kwa muda huo, lakini Jeshi la Polisi limeacha kumchukulia hatua mwananchi huyo kutokana na kuamua kujitokeza hadharani kwa hiari kuisalimisha silaha hiyo kwa mtendaji wa kakta hiyo.

Katika kuhakikisha kuwa hali ya amani na utulivu inaendelea kudumu mkoani Kigoma, Jeshi la Polisi limeendelea kufanya operesheni ya kupambana na vitendo mbalimbali vya kihalifu vikiwemo vya kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake, Kamanda Kihenya amesema kuwa hiyo ni silaha ya tatu kusalishwa mkoani humo katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Amesema pamoja na kusalishwa kwa silaha hizo aina ya SMG pamoja na risasi kadhaa, Polisi pia imewakamata watuhumiwa 11 waakiwemo wa makosa ya unyang’anyi wa kutumia nguvu.

Jeshi la Polisi mkoani humo limeendelea kutoa wito kwa wananchi mkoani humo kuendelea kutoa ushirikiano kwa Polisi mara wanapobaini kuwepo kwa makundi ya wahalifu ama mhalifu mmoja mmoja ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kigoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa