Na Emmanuel J. Matinde wa Kigoma yetu Blog
Kigoma
Tuesday June 5, 2012
Mbunge wa Jimbo la Muhambwe Mkoani Kigoma Bw. Felix Mkosamali amevamiwa na kupigwa na kundi la vijana wanaodaiwa kuwa wapinzani wake Kisiasa
Bw. Felix Mkosamali amekutwa na mkasa huo Juni 3 mwaka huu, majira ya saa 11jioni katika kijiji cha Kagezi akiwa njiani kurejea mjini Kibondo akitokea katika Kijiji cha Kumsenga alikokwenda kuhani msiba nyumbani kwa mzee Gunga kwenda Kibondo mjini
Akielezea tukio hilo amesema kabla ya kushambuliwa yeye pamoja na baadhi ya wafuasi wake, walisimamishwa na watu aliodhani kuwa walikuwa na nia ya kumsalimia lakini wakati alipoteremka kusalimiana nao ghafla watu hao walianza kumshambulia kwa ngumi, mateke na mawe
“Nilishambuliwa na watu ambao walikuwa na lengo la kunidhuru na wakavunja kioo cha nyuma cha gari langu na cha mbele kimepata mpasuko”, alisema Mkosamali.
“Inaonekana ni tukio ambalo lilikuwa limepangwa na ni vijana wachache ambao wamepandikizwa na maadui zangu wa kisiasa hasa pale ambapo tunaeleza ukweli juu ya ubadhirifu ambao unafanywa na baadhi ya wanasisaa, hapo ndipo ambapo baadhi ya watu sasa wanapandikiza vijana ili watutupie mawe”, aliongeza Mkosamali.
Aidha bw.Mkosamali alisema katika tukio hilo yeye hakudhurika sana ila dereva wake aliumizwa ambapo ilibidi aende kutibiwa katika hospitali ya wilaya ya Kibondo na baadaye kuruhusiwa.
Amesema hatua ambayo ameichukua mpaka sasa kuhusiana na tukio hilo ni kutoa taarifa polisi kwa ajili ya taratibu za kisheria kufuatwa.
Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoani Kigoma kamishina msaidizi wa polisi Frasser Kashai amethitisha kutokea kwa tukio na jeshi la polisi tayari limeanza kuwafuatilia waliohusika ili waweze kukamatwa na kupelekwa katika vyombo vya sheria ili washitakiwe kwa kosa walilotenda.
0 comments:
Post a Comment